Jumapili, 25 Aprili, 2021
Leo ni Jumapili tarehe 12 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1442 Hijria mwafaka na tarehe 25 Aprili 2021 Miladia.
Siku kama ya leo yaani mwezi 12 Ramadhani kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia ni siku ambayo Nabii Issa Ibn Maryam AS aliteremshiwa kitabu kitukufu cha Injili. Neno Injili ni la Kigiriki na lina maana ya bishara. Jina hilo limetajwa mara 12 katika Qur’ani Tukufu na kitabu hicho kinaitambua Injili kuwa ni kitabu cha Mwenyezi Mungu SWT chenye sheria na kanuni za mbinginu. Hata hivyo kitabu kinachojulikana hivi sasa kwa jina la Injili si kile kilichoteremshwa kwa Nabii Issa Masih bali ni riwaya na kumbukumbu zilizokusanywa na wanafunzi wake baada ya Yeye kupaa mbinguni. ***
Miaka 1441 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 12 Ramadhani mwaka wa Kwanza Hijria, muda mfupi baada ya Mtume Mtukufu Muhammad (SAW) kuhamia Madina akitokea Makka, aliunga udugu baina ya Muhajirina na Ansar. Muhajirina ni watu ambao walihama na Mtume (SAW) kutoka Makka kwenda Madina na Ansar ni Waislamu wa mjini Madina waliowakaribisha na kuwanusuru Muhajirina katika mji huo. Kwenye sherehe hiyo ya kuunga udugu wa Waislamu, Mtume (SAW) alimtangaza Ali bin Abi Talib (AS) kuwa ndugu yake hapa duniani na Akhera. ***
Tarehe 12 Ramadhani miaka 845 iliyopita, alifariki dunia Ibn Jawzi, faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi katika karne ya 6 Hijria. Ibn Jawzi alizaliwa mwaka 510 Hijria na kufanya safari nyingi kwa ajili ya masomo. Mbali na kubobea katika masuala ya elimu ya fiq'hi na hadithi, alikuwa mtaalamu katika uwanja wa kutoa mawaidha na hata akaweza kuaminiwa na maulamaa wakubwa wa zama zake. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi na mashuhuri zaidi ni Al Muntadhim na Mawaidhul Muluk. ***
Katika siku kama ya leo miaka 529 iliyopita, serikali ya mwisho ya Kiislamu barani Ulaya ilisambaratika huko Granada. Baada ya kudhihiri dini ya Uislamu na kupanua mamlaka yake katika maeneo ya Asia na kaskazini mwa Afrika, jeshi la Waislamu liliingia kusini magharibi mwa Ulaya kupitia lango bahari la Jabal Tariq (Gibraltar) na kulitawala eneo hilo kwa kipindi cha karne 8. Eneo hilo ambalo kwa sasa linaitwa Uhispania, wakati huo lilijulikana kwa jina la Andalusia. Katika kipindi cha ustawi wa ustaarabu wa Kiislamu eneo la Granada lilikuwa kituo kikuu cha ustaarabu huo na makao makuu ya kueneza Uislamu hususan barani Ulaya. Dola la Kiislamu la Andalusia liliangushwa kupitia njia ya kueneza ufuska na maovu baina ya watawala na makhalifa wa wakati huo. ***
Miaka 123 iliyopita katika siku kama ya leo, serikali ya Marekani ilitangaza vita dhidi ya Uhispania. Kabla ya hapo, Marekani ilikuwa imeitaka Uhispania ilipatie ufumbuzi suala la Cuba kupitia njia za amani. Baadhi ya Wacuba kwa miaka mingi walikuwa wakipigania mamlaka ya kujitawala na mara kadhaa walifanya majaribio ya mapinduzi na kuendesha mapigano ya silaha. Kulipuka manowari ya kijeshi ya Marekani ya Maine katika maji ya Cuba, kilikuwa kisingizio kizuri kwa Marekani cha kuingia katika vita dhidi ya Uhispania. Katika vita hivyo vilivyoanza tarehe 25 Aprili hadi Agosti 12 mwaka 1898 vilimalizika kwa kushindwa Uhispania; na kwa mujibu wa mkataba wa Paris ardhi za Ufilipino, Ouerto Rico, Guam na Cuba zipatiwa Marekani.***
Katika siku kama ya leo ya tarehe 12 Ramadhani miaka 99 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sheikh Mahdi Khalisi, faqihi na mujtahidi mkubwa wa zama hizo. Ayatullah Khalisi alizaliwa huko Kadhimiya nchini Iraq mwaka 1277 Hijiria na akiwa kijana alijishughulisha na kuamrisha mema na kukataza maovu sambamba na kustahamili shida nyingi kipindi cha masomo na kutafuta elimu. Katika kipindi cha Vita vya Kwanza vya Dunia, msomi huyo akishirikiana na baadhi ya mujtahid wa Iraq, alianzisha mapambano dhidi ya uvamizi wa wakoloni Waingereza nchini humo. Baada ya muda alirejea nchini Iran na kujishughulisha na kazi ya ualimu na kufunza elimu za kidini. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo mkubwa ni Kifayatul Usuul na Anawinul Usul. ***
Miaka 50 iliyopita katika siku kama ya leo, takribani Wamarekani laki mbili walifanya maandamano mjini Washington wakiendeleza upinzani wao dhidi ya mashambulizi ya nchi hiyo huko Vietnam. Maandamano hayo yalikuwa miongoni mwa vielelezo vikubwa vya upinzani wa wananchi wa Marekani dhidi ya siasa za kichokozi za serikali ya nchi hiyo huko Vietnam. Katika vita vya Vietnam vilivyoanza mwaka 1964 Marekani ilituma askari laki tano nchini humo ambako makumi ya maelfu miongoni mwao waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Kwa sababu hiyo wananchi wa Marekani walizidisha upinzani dhidi ya vita hivyo na mwaka 1975 Marekani ililazimika kufunga virago na kuondoka Vietnam kutokana na mashinikizo ya ndani na ya kimataifa na kushindwa mara kwa mara jeshi la nchi hiyo katika medani za vita.***
Na siku kama ya leo miaka 41iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Ordibehesht mwaka 1359 Hijiria Shamsia, Marekani ilishambulia kijeshi ardhi ya Iran kwa kutumia helikopta na ndege kadhaa za kivita. Serikali ya Marekani ilifanya mashambulizi hayo baada ya kushindwa njama zake mbalimbali za kutaka kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu wa Iran. Lengo la mashambulio hayo lilikuwa ni kutaka kuwakomboa majasusi wake waliotiwa mbaroni wakati wa kutekwa ubalozi wa Marekani hapa nchini uliokuwa pango la kijasusi. Licha ya kuweko mipango makini, kutumiwa vyombo vya kisasa kabisa na mazoezi mengi yaliyofanywa katika eneo linalofanana na hilo ili kuhakikisha operesheni hiyo inafanikiwa, lakini mashambulizi hayo yalikatishwa na tufani kubwa ya mchanga iliyotokea Tabas na kupelekea kuanguka baadhi ya ndege, kushika moto helikopta za Marekani na kufa baadhi ya askari wa nchi hiyo huku waliobakia wakiikimbia ardhi ya Iran. ***