May 09, 2021 21:05 UTC
  • Jumatatu tarehe 10 Mei 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 27 Ramadhani mwaka 1442 Hijria sawa na tarehe 10 Mei mwaka 2021.

Miaka 882 iliyopita katika siku sawa na ya leo Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Arabi, arif na msomi mkubwa wa Kiislamu alizaliwa huko Andalusia huko kusini mwa Uhispania ya leo. Ibn Arabi alifanya safari nyingi katika baadhi ya nchi na miji ikiwemo Tunisia, Makka na Baghdad na kila alipofika aliheshimiwa na kukirimiwa. Alikuwa msomi hodari na baadhi ya duru zinasema kuwa ameandika vitabu na risala zaidi ya 500. Miongoni mwa kazi zake kubwa ni vitabu vya "Tafsir Kabir", "al Futuhatul Makkiyyah" na "Fususul Hikam".

Siku kama ya leo miaka 332 iliyopita aliaga dunia Allamah Muhammad Baqir Majlisi, mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu. Allamah Majlisi aliandika vitabu vingi wakati wa uhai wake ambavyo hii leo ni marejeo ya Waislamu. Katika kipindi cha uhai wake Allamah Muhammad Baqir Majlisi alifanya hima kubwa kuhakikisha kuwa Swala za Ijumaa na jamaa zinatekelezwa. Vilevile alifanya juhudi za kuasisi shule za masomo ya kidini na kueneza Hadithi za Mtume Muhammad (saw) na Ahlul Bait zake watoharifu. Idadi ya vitabu vilivyoandikwa na Allamah Muhammad Baqir Majlisi imetajwa kuwa zaidi ya 600 na mashuhuri zaidi ni kile kinachojulikana kwa jina la Biharul Anwar. Vitabu vingine mashuhuri vya msomi huyo ni Hayatul Quluub, Ainul Hayat na Zadul Maad.

Allamah Muhammad Baqir Majlisi

Katika siku kama ya leo miaka 46 iliyopita kundi linalopigania uhuru wa Sahara Magharibi liliasisi Harakati ya Kupigania Uhuru ya Polisario. Harakati hiyo ilikaribishwa na wakazi wa eneo hilo na ikaanzisha mapambano dhidi ya wakoloni wa Kihispania hadi wakoloni hao walipoondoka Sahara mwaka 1975. Hata hivyo serikali ya Uhispania ilikabidhi mamlaka ya eneo hilo kwa serikali za Morocco na Mauritania. Mauritania ililazimika kuondoka Sahara Magharibi kutokana na mapambano makali ya Polisario na hali mbaya ya ndani ya nchi hiyo. Morocco iliendelea kukabiliana na wapigania uhuru wa Polisario hadi mwaka 1991 ambapo mapigano kati ya pande hizo mbili yalisitishwa chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa. Eneo hilo lingali linakaliwa na Morocco.

Bendera ya Jamhuri ya Kiarabu ya Sahara Magharibi

Miaka 32 iliyopita katika siku kama ya leo, Dakta Sayyid Jawad Mustafavi mwandishi, mhakiki na mhadhiri wa zama hizi wa kiirani alifariki dunia.  Awali alisoma masomo ya kidini sambamba na kufanya utafiti katika fani mbalimbali katika uwanja huo. Jawad Mustafavi alibobea mno katika elimu za kidini. Baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran aliteuliwa kuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha elimu za dini mjini Mash'had. Aidha msomi huyo hakuwa nyuma katika uga wa kualifu vitabu. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni al-Kashif na Miftaful al-Wasail.

Dakta Sayyid Jawad Mustafavi

Tarehe 10 Mei miaka 27 iliyopita yaani tarehe 10 Mei 1994, Nelson Rolihlahla Mandela aliapishwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini baada ya kupita zaidi ya karne tatu za utawala wa makaburu wachache nchini humo. Chama cha African National Congress (ANC) kilijipatia viti 252 kati ya jumla ya viti 400 vya Bunge la Afrika Kusini, kwenye uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia na wa kihistoria nchini humo. Baada ya kuchaguliwa, Rais Mandela alimteua Thabo Mbeki kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na FW de Klerk kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Afrika Kusini.

Nelson Rolihlahla Mandela