Jumatano tarehe 12 Mei 2021
Leo ni Jumatano tarehe 29 Ramadhani 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 12 Mei 2021.
Siku kama ya leo miaka 794 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa mwanazuoni mahiri wa Kiislamu katika mji wa Hillah huko Iraq, Ayatullah Jamaluddin Hassan bin Yusuf mwenye lakabu ya Allamah Hilli. Awali alisoma kwa baba yake na mjomba wake na akiwa katika rika la ujana alikuwa tayari amefanikiwa kufikia daraja za juu za elimu katika taaluma kama fikihi, usul fiqhi, hadithi na kadhalika. Alisoma falsafa, nujumu, fiqhi, hadithi na teolojia kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama Khaja Nasiruddin Tusi. Mbali na kulea wanafunzi wengi, Allamah Hilli pia alisifika kwa uchamungu na kuipa mgogo dunia. Ameandika vitabu vingi vya thamani vinavyokadiriwa kufikia 120 na miongoni mwa vitabu hivyo ni Tadhkiratul Fuqahaaa, Irshadul Adh'han, na Kashful Murad. Alimu huyo aliaga dunia mwaka 726 Hijria.
Miaka 635 iliyopita, alifariki dunia Nassirddin Muhammad maarufu kwa jina la Ibn Furat, faqihi, mwanahistoria na khatibui wa nchini Misri. Ibn Furat alizaliwa mjini Cairo mwaka 735 Hijiria na kuanza masomo yake akiwa kijana mdogo. Msomi huyo alijikita sana katika masuala ya historia, kiasi cha kumfanya aandike vitabu mbalimbali katika uwanja huo. Miongoni mwa athari muhimu za Ibn Furat ni kitabu cha ‘Taarikhud-Duwal wal-Muluuk’, ambacho kinazungumzia historia na matukio ya karne ya sita hadi ya nane Hijria.
Siku kama ya leo miaka 201 iliyopita, alizaliwa Florence Nightingale, mwanzilishi wa uuguzi wa kisasa huko Florence nchini Italia. Nightingale aliyejulikana kwa jina mashuhuri la 'mwanamke mwenye taa mkononi' alikuwa muuguzi na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Alipewa lakabu ya 'mwanamke mwenye taa mkononi' kutokana na uvumilivu wake mkubwa na kujinyima usingizi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa nyakati za usiku. Alifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali nyingi nchini Uingereza. Kazi hiyo aliyoifanya kwa miaka mingi bila kuchoka ilimdhoofisha sana kimwili kwa kadiri kwamba, alipofuka macho mwishoni mwa umri wake, na hatimaye aliaga dunia tarehe 13 Agosti 1910.
Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, Berlin mji mkuu wa Ujerumani iligawanywa katika sehemu mbili za Mashariki na Magharibi. Kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia kati ya nchi nne zilizoikalia kwa mabavu Ujerumani, mji huo uligawanywa na kudhibitiwa na Russia, Ufaransa, Uingereza na Marekani. Muda mfupi baadaye mji huo ulizingirwa na Urusi ya zamani. Harry Truman rais wa wakati huo wa Marekani alichukua uamuzi wa kuvunja mzingiro na udhibiti huo wa Urusi. Katika kutekeleza hatua hiyo Marekani ilikaribia kupigana vita na Urusi. Matokeo mengine ya mgogoro huo ilikuwa kugawanywa Ujerumani katika sehemu mbili za Ujerumani Magharibi na Mashariki.
Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, na kwa mujibu wa azimio nambari 278 la Umoja wa Mataifa nchi ya Bahrain ilijitenga na ardhi ya Iran. Kabla ya kudhihiri Uislamu, nchi hiyo ndogo iliyo katika Ghuba ya Uajemi ilikuwa katika utawala wa Iran na baada ya kubuniwa utawala wa Kiislamu ikawa inadhibitiwa na makhalifa wa Kiislamu. Mwanzoni mwa karne ya 7 Hijiria kwa mara nyingine tena nchi hiyo iliunganishwa na Iran na baada ya hapo ikawa chini ya himaya ya Uingereza. Licha ya hayo Iran iliendelea kudai udhibiti na utawala wake kwa Bahrain na kulalamikia vikali hatua ya Uingereza ya kuitawala nchi hiyo.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, yaani tarehe 22, Ordibehesht, mwaka 1364 Hijria Shamsia, makumi ya watu waliuawa shahidi na kujeruhiwa kutokana na shambulizi la bomu lililofanywa na kundi la kigaidi la Munafiqiin (MKO) mjini Tehran. Mripuko huo mbali na kusababisha uharibifu mkubwa, uliteketeza kikamilifu jengo moja la ghorofa mbili na karakana ya ufumaji nguo katika barabara ya Naser Khosro na kuua watu 9. Watu wengine 45 walijeruhiwa. Katika hujuma hiyo ya kigaidi, magaidi wa MKO walitumia bomu lililokuwa na mada za milipuko za TNT zilizokuwa na uzito wa pauni 50. Kundi hilo la kigaidi limekuwa likifanya mashambulizi ya aina hii hapa nchini kwa shabaha ya kupiga vita mfumo wa utawala wa Kiislamu na kudhoofisha usalama wa taifa. Mauaji hayo ya kinyama kwa mara nyingine tena yaliidhihirishia dunia jinai za kutisha za kundi la kigaidi la MKO linaloungwa mkono na madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Na miaka 13 iliyopita, katika siku kama ya leo, tetemeko lenye ukubwa wa 7.9 kwa kipimo cha Rishta, liliukumba mji wa Sichuan ulioko kusini magharibi mwa China. Katika tetemeko hilo la kutisha watu wapatao 87,000 walifariki dunia na wengine laki tatu na 80,000 kujeruhiwa. Tukio hilo la kutisha liliwaacha mamilioni ya watu bila makazi.