Alkhamisi tarehe 15 Julai 2021
Leo ni Alkhamisi tarehe 4 Dhilhija 1442 Hijria wa na Julai 15 mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Tir 1318 Hijria Shamsia, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mji wa Mash'had ulioko kaskazini mashariki mwa Iran. Baada ya kumaliza masomo katika shule ya sekondari, alijikita zaidi katika masomo ya kidini kutoka kwa baba yake, na kupiga hatua kubwa ya kielimu katika kipindi kifupi. Ayatullah Khamenei alielekea Qum kwa masomo ya juu ya kidini na kupata fursa ya kunufaika na elimu kutoka kwa maulamaa wakubwa katika mji huo, kama vile Imam Ruhullah Khomeini, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai katika masomo ya fiqh, usululi na falsafa. Akiwa bado kijana, Sayyid Khamenei alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi dhidi ya utawala kibaraka wa Shah hapa nchini, na mara kadhaa alitiwa mbaroni, kutumikia vifungo na hata kupelekwa uhamishoni. Baada ya kufariki dunia Imam Khomeini MA mwaka 1368 Hijria Shamsia, Baraza la Wanachuoni linalomchagua Kiongozi Mkuu wa Iran, lilimchagua Ayatullah Khamenei, wakati huo akiwa rais wa nchi, kuwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita yaani tarehe 15 Julai mwaka 1944, jeshi la Marekani lilianza kuishambulia Japan kwa maelfu ya mabomu katika kipindi cha Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulio hayo ya mabomu ya Marekani yaliendelea hadi Japan iliposalimu amri. Tukio hilo chungu licha ya kusababisha makumi ya maelfu ya wananchi wasio na hatia wa Japan kuuawa kwa halaiki, lilipelekea pia zaidi ya viwanda elfu tatu vikubwa kwa vidogo kuharibiwa kabisa.
Katika siku kama ya leo miaka 53 iliyopita yaani tarehe 24 Tir mwaka 1347 Hijria Shamsia, Ismail Balkhi mwanamapambano na mwanafikra wa Kiafghani aliuawa shahidi mjini Kabul. Alizaliwa katika kijiji kimoja kaskazini mwa Afghanistan. Alianza kusoma kwa bidii masomo ya dini tangu akiwa mdogo na kipindi fulani alifanya safari nchini Iran na Iraq, lengo likiwa ni kujiendeleza zaidi kielimu. Ismail Balkhi alikuwa akiendesha mapambano dhidi ya udikteta na daima alikuwa akiwashajiisha wananchi Waislamu wa Afghanistan kupambana na tawala dhalimu. Kutokana na harakati hizo, shahidi Balkhi alikuwa chini ya mashinikizo ya watawala wa wakati huo wa Afghanistan, na kwa miaka kadhaa alifungwa jela.
Siku kama ya leo miaka 11 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Tir 1389 Hijria Shamsia, kwa akali watu 27 waliuawa na wengine 169 kujeruhiwa kwenye milipuko miwili ya mabomu iliyotokea katika mji wa Zahedan, ulioko kusini mashariki mwa Iran. Milipuko hiyo ilitokea mkabala na Msikiti Mkuu wa Zahedan, wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib (as) mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Muhammad (saw). Kikundi cha kigaidi kilichojulikana kwa jina la Jundullah, ndicho kilichotekeleza shambulio hilo la kigaidi.