Aug 03, 2021 20:23 UTC
  • Jumatano tarehe 4 Agosti mwaka 2021

Leo ni Jumatano tarehe 24 Dhulhija 1442 Hijria sawa na Agosti 4 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1433 kwa mujibu wa nukuu mashuhuri ya kihistoria Mtume Muhammad (SAW) akiwa pamoja na binti yake Bibi Fatima (AS), mkwewe Ali bin Abi Twalib (AS) na wajukuu wake wawili Hassan na Hussain (AS) waliondoka mjini Madina kwenda kufanya mdahalo na viongozi wa Wakristo wa eneo la Najran juu ya dini ya kweli. Tukio hilo linaelezwa na Mwenyezi Mungu SW katika aya za 60 na 61 za sura ya Aal Imran. Wakati viongozi wa Najran walipoona Mtume amekuja katika mdahalo huo akiwa na watu wanne tu wa Nyumba yake tukufu walipigwa na mshangao na kuelewa kwamba, dua ya mtukufu huyo ya laana kwa atakayesema urongo itakubaliwa. Katika hali hiyo askofu wa Najran alisema: "Ninaziona nyuso ambazo iwapo zitamuomba Mwenyezi Mungu aung'oe mlima mkubwa zaidi mahala pake basi dua yao itajibiwa papo hapo. Kwa msingi huo si sahihi kufanya mdahalo na watu hawa watakatifu kwani yumkini kizazi chetu chote kikaangamia." Baada ya hapo askofu huyo wa Najran alimuomba Mtume (SAW) kufanya suluhu na kusamehe. Tukio hilo la kihistoria lilidhihirisha haki na ukweli wa dini tukufu ya Kiislamu na utukufu na nafasi aali ya Ahlubait wa Mtume Muhammad (SAW).

Miaka 229 iliyopita alizaliwa Percy Bysshe Shelley malenga wa Uingereza. Percy alianza kupenda taaluma ya fasihi tangu utotoni na kuonyesha kipawa kikubwa katika uwanja huo. Alikuwa mfuasi na muungaji mkono wa thamani za upendo, urafiki na uhuru na sababu hiyo ndiyo iliyomfanya avutiwe na Mapinduzi ya Ufaransa ambayo ndio kwanza yalikuwa yametokea. Percy Bysshe Shelley aliaga dunia mwaka 1822 akiwa na umri wa miaka 30 baada ya boti yake kuzama katika Bahari ya Mediterrania.

Percy Bysshe Shelley

Miaka 216 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa William Rowan Hamilton mwanahisabati na mtaalamu wa elimu ya fizikia wa Ireland alizaliwa.  Alikuwa na kipaji cha hali ya juu kiasi kwamba akiwa na umri wa miaka 13 alikuwa amejifunza lugha 12 za dunia zikiwemo Kiarabu na Kifarsi. William Rowan Hamilton taratibu akaanza kuwa na mapenzi makubwa na elimu za fizikia na hisabati. Aidha alifanikiwa kuanzisha baadhi ya kanuni na mifumo muhimu katika elimu hizo. Akiwa na umri wa miaka 22 Hamilton alikuwa tayari ni mwalimu wa elimu ya nujumu. Msomi huyo aliaga dunia 1865. 

William Rowan Hamilton

Katika siku kama ya leo miaka 146 iliyopita, aliaga dunia Hans Christian Andersen mwandishi wa vitabu vya watoto wa nchini Denmark. Alizaliwa mwaka 1805 na tangu akiwa mdogo alikuwa na mapenzi makubwa na visa. Baada ya kuaga dunia baba yake, Hans Christian Andersen akiwa na umri wa miaka 11 aliacha shule na kuanza kufanya kazi. Baada ya kuingia katika maonyesho na michezo ya kuigiza ya kifalme, hali yake ya maisha iliboreka na hivyo akaamua kuendelea na masomo. Mwandishi huyo wa Kidenmark awali alianza kujihusisha na utungaji mashairi na kuandika visa na simulizi. Hata hivyo baadaye Andersen aliondokea kuwa na mapenzi makubwa na visa vya watoto na alionyesha kipaji kikubwa alichokuwa nacho katika uwanja huo.

Hans Christian Andersen

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, vikosi vilivyokuwa na mrengo wa utaifa nchini Uturuki vikiongozwa na Mustafa Kemal Ataturk vilianza kuwashambulia wanajeshi wa Ugiriki waliokuwa wameikalia kwa mabavu nchi hiyo. Baada ya kusambaratika utawala wa Othmania katika Vita vya Kwanza vya Dunia, ardhi asili ya utawala huo yaani Uturuki iliangukia mikononi mwa tawala waitifaki. 

Kemal Ataturk

Katika siku kama ya leo miaka 91 iliyopita, alizaliwa katika mji wa Mash'had Iran Ayatullah Sayyid Ali Sistani fakihi, alimu na marjaa taqlidi wa Kishia.  Alianza kujifunza Qur'an akiwa na miaka 5 na akiwa na umri wa miaka 11 alianza kusoma masomo ya kidini ya utangulizi baada ya kutakiwa na baba yake kufanya hivyo. Baadaye alielekea katika mji wa Qum kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Baadaye Ayatullah Sistani alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini mjini Najaf Iraq. Hii leo Ayatullah Sistani si tu kwamba, anahesabiwa kuwa marjaa mkubwa zaidi nchini Iraq bali amekuwa pia na nafasi muhimu katika kuleta umoja, mshikamno na utulivu katika nchi hiyo ya Kiarabu. 

Ayatullah Sayyid Ali Sistani

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita Marekani ilishindwa katika vita vya baharini vilivyozishirikisha meli za kivita za Marekani na Vietnam ya Kaskazini katika Ghuba ya Tonkin inayopatikana kwenye bahari ya China ya Kusini. Mikwaruzano hiyo ya kijeshi iliipa Marekani kisingizio cha kuingia vitani moja kwa moja na Vietnam ya Kaskazini. Wakati huo Washington ilikuwa ikiiunga mkono kwa pande zote Vietnam ya Kusini dhidi ya ile ya Kaskazini. Wanajeshi wa Marekani waliingia vitani moja kwa moja kupigana dhidi ya Vietnam ya Kaskazini.

Vietnam