Oct 22, 2021 00:26 UTC
  • Ijumaa tarehe 22 Oktoba mwaka 2021

Leo ni Ijumaa tarehe 15 Rabiul Awwal 1443 Hijria sawa na tarehe 22 Oktoba 2021.

Katika siku kama ya leo miaka 115 iliyopita, Paul Cezanne mchoraji maarufu wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 67. Alikuwa na shauku na mapenzi makubwa na fani ya uchoraji tangu akiwa mdogo, lakini kutokana na msisitizo wa baba yake aliingia Chuo Kikuu na kusoma taaluma ya sharia. Hatimaye akiwa na umri wa miaka 24, baba yake alimruhusu kuendelea na masomo katika taaluma ya uchoraji. Mwanzoni mabango ya uchoraji ya Paul Cezanne hayakupata wafuasi wengi na athari zake za uchoraji zilikabiliwa na ukosoaji mkubwa. Mwenendo huo uliendelea hadi alipofikisha umri wa miaka 50 ambapo hatua kwa hatua alianza kupata umashuhuri kutokana na kuuza mabango yake ya uchoraji.

Paul Cezanne

Tarehe 30 Mehr miaka 69 iliyopita, Dakta Hussein Fatimi, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Dakta Musadiq, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Iran wakati huo alitangaza habari ya kukatwa uhusiano wa kisiasa kati ya Iran na Uingereza. Uamuzi huo ulikabidhiwa kwa balozi mdogo wa Uingereza mjini Tehran, baada ya kuidhinishwa na baraza la mawaziri. Dakta Fatimi alisema Tehran imeamua kukata uhusiano na Uingereza kutokana na upuuzaji wa serikali ya London kwa matakwa ya wananchi wa Iran ya kujipatia haki zao, hususan katika uwanja wa kutaifisha sekta ya mafuta. Dakta Fatimi aliwataka viongozi wa London wabadili siasa zao kuhusiana na Iran.

Dakta Hussein Fatimi

Miaka 65 iliyopita katika siku kama hii ya leo, mawaziri wakuu wa Ufaransa, Uingereza na utawala wa Kizayuni wa Israel walichunguza mpango wa kuivamia Misri katika kikao cha siri kilichofanyika Ufaransa. Ufaransa na Uingereza ziliazimia kuukalia kwa mabavu mfereji wa Suez baada ya kupoteza maslahi yao haramu katika eneo hilo, kufuatia tangazo lililotolewa na Rais Gamal Abdulnasir wa Misri mwaka 1957 la kutaifisha mfereji huo.

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, aliaga dunia Arnold Joseph Toynbee mwanahistoria mtajika wa Uingereza. Alizaliwa mwaka 1889. Toynbee alikuwa akifundisha taaluma ya Historia ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha London. Msomi huyo ameandika vitabu vingi katika uga wa historia na baadhi ya vitabu vyake ni A Study of History, Change and Habit, Choose Life na Civilization on Trial.

Arnold Joseph Toynbee