Ijumaa, 7 Januari, 2022
Leo ni Ijumaa tarehe 4 Jamadithani 1443 Hijria sawa na Januari 7 mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya Kiislamu na mtarjumi wa Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kijapani Toshihiko Izutsu. Alizaliwa tarehe 4 Mei 1914 katika mji wa Tokyo na mwaka 1960 alipata shahada ya uzamivu katika taaluma ya lugha na kuanza kufunza lugha na falsafa yake. Toshihiko Izutsu alitunukiwa nishani ya juu kabisa ya elimu kutoka kwa mfalme wa Japan na ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni "Historia ya Fikra za Kiislamu", tarjumu ya kitabu cha "al Mashair" cha Mulla Sadra na vilevile tarjumu ya kitabu cha "Fihi Maa Fiih" cha Maulawi kwa lugha ya Kijapan.

Katika siku kama hii ya leo miaka 36 iliyopita Suleiman Khater aliyekuwa miongoni mwa polisi wa mpakani wa Misri katika jangwa la Sinai alikufa shahidi akiwa jela. Suleiman Khater mwezi Oktoba mwaka 1985 aliwaangamiza Wazayuni wengi katika kulalamikia hatua ya serikali ya Misri ya kusaini hati ya mapatano ya Camp David kati yake na utawala wa Kizayuni. Serikali ya Misri ilimtia mbaroni polisi huyo na kuamuru ahukumiwe kifungo cha maisha jela.

Tarehe 7 Januari miaka 43 iliyopita dikteta wa Cambodia Pol Pot alikimbia nchi kufuatia mashambulizi ya jeshi la Vietnam dhidi ya nchi hiyo. Pot alikuwa kiongozi wa kundi la Khmer Rouge lililokuwa muungaji mkono mkubwa wa fikra za kimao na serikali ya China. Sifa kuu ya serikali ya Pol Pot ilikuwa kutumia mabavu dhidi ya raia, kuwahamishia kwa nguvu vijijini na kufuta kabisa athari zote za utamaduni na ustaarabu asilia. Pol Pot na kundi lake na Khmer Rouge waliua watu wanaokadiriwa kuwa milioni moja na nusu hadi mbili hususan raia wenye asili ya Vietnam katika kipindi cha chini ya miaka mitatu ya utawala wake huko Cambodia. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana jeshi la Vietnam likachukua hatua za kuiondoa madarakani serikali ya Pol Pot.

Tarehe 17 Dei miaka 44 iliyopita wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano makubwa kote nchini wakilalamikia kuchapishwa makala iliyomvunjia heshima mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Ruhuullah Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu. Maandamano hayo yalizidisha vuguvugu na kasi za Mapinduzi ya Kiislamu kuelekea katika ushindi. Utawala wa Shah ambao ulikuwa ukifahamu vyema ushawishi na uungaji mkono mkubwa wa Imam Khomeini miongoni mwa wananchi, ulikuwa ukidhani kwamba kumvunjia heshima Imam Khomeini kungeweza kupunguza kiwango cha mapenzi na uungaji mkono mkubwa wa wananchi wa shakhsia huyo. Katika kufanikisha lengo hilo, gazeti la Ittilaat lililokuwa likitolewa mjini Tehran liliandika makala ya kumvunjia heshima Imam Khomeini katika toleo lake la mwezi Dei mwaka 1356 Hijria Shamsiya. Hata hivyo makala hiyo ilikuwa kama cheche ya moto iliyochochea zaidi harakati za mapinduzi na hatimaye tarehe 22 mwezi Bahman mwaka 1357, utawala kibaraka wa Shah ukang'olewa madarakani kwa mapambano ya wananchi wa Iran.

Miaka 79 iliyopita yaani mnamo tarehe 7 mwezi Januari mwaka 1943 aliaga dunia Nikola Tesla mwanafikia mzaliwa waYugoslavia. Nikola alizaliwa mwaka 1857 na alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza masomo ya fizikia wakati akiwa shuleni. Msomi huyo wa Kiyugoslavia alifanya tafiti na uvumbuzi wake mwingi katika uwanja wa nishati ya umeme na kupata mafanikio makubwa. Umeme mbadala au Altenative electricity unahesabiwa kuwa miongoni mwa uvumbuzi wa Nikola Tesla. Mwanafikizia huyo alikipa jina lake la Tesla, kifaa kinachotumika kupimia kiwango na mtiririko wa sumaku yaani (magnetic flux).

Katika siku kama ya leo miaka 68 iliyopita Sayyid Mujtaba Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika utawala wa Shah hapa nchini. Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.

Miaka 86 iliyopita katika siku kama hii ya leo, wanawake wa Kiirani walipigwa marufuku kuvaa vazi la Kiislamu la aina yoyote kufuatia amri ya Ridhakhan Pahlavi. Ridhakhan alitoa amri hiyo baada ya kutekelezwa mpango wa kubadili mavazi ya wanaume nchini Iran. Mpango huo ulitekelezwa kwa lengo la kufuta thamani za Kiislamu na badala yake kuiga utamaduni wa Kimagharibi. Ridhakhan alitekeleza mpango huo wa kupiga marufuku vazi la hijabu kwa wanawake wa Kiislamu nchini Iran baada ya safari yake nchini Uturuki na kufuata nyayo za Kemal Atatürk Rais wa wakati huo wa Uturuki aliyekuwa na mielekeo ya Kimagharibi ambaye aliwapiga marufuku wanawake wa nchi hiyo kuvaa mavazi ya Kiislamu.
