Feb 07, 2022 07:13 UTC
  • FAINALI YA AFCON 2022, FEB 7

Hujambo mpenzi mwanaspoti natumai u mzima wa afya. Kipindi chetu cha leo kitaangazia tu kumalizika kwa mashindano ya soka ya mataifa ya Afrika (AFCON) 2022 yaliyofanyika huko Cameroon....karibu....

Misri ambao ni mabingwa mara saba wa Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON, Jumapili usiku walishuka dimbani kuvaana na Senegal kwenye fainali ya mashindano hayo ya kieneo iliyopigwa katika Uwanja wa Olembe jijini Yaounde nchini Cameroon. Senegal ambao walipoteza katika fainali ya AFCON mwaka 2019 dhidi ya Algeria, walijitosa uwanjani wakiwa na azma ya kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya kuzidiwa pia ujanja kwenye fainali ya 2002 nchini Mali. Na kweli, mgaagaa na upwa, hali wali mkavu eti..au labda ni dua yao ilikubaliwa na wakavuna ushindi japo kwa mbinde? Fainali ya AFCON Jumapili ilikuwa ya aina yake kwa sababu iliwakutanisha ana kwa ana Sadio Mane wa Senegal na Mohamed Salah wa Misri ambaye pia anakipiga Liverpool ya Uingereza. Mashabiki wengi wa soka waliita fainali hiyo ngoma kati ya Salah na Mane. Timu hizo mbili zilikabana koo katika dakika 90 za ada, na 30 za nyongeza, lakini bado wakatoshana nguvu kwa kutoa sare tasa. Kwa msingi huo walilazimika kujitosa kwenye upigaji matuta, na hapo ndipo Wasenegali wakaibuka na ushindi wa mabao 4-2. Mane ambaye alikuwa amepoteza penati dakika saba baada ya kuanza ngoma baada ya mwenzake kupigwa kiatu katika sanduku la hatari, alilazimika kufidia makosa yake kwenye upigaji penati wa kutafuta bingwa wa kandanda Afrika, na hatimaye akafanikiwa kutikisa nyavu katika pigo la mwisho lililowanyanyua vitini mashabiki.

Mashabiki wa soka wa Senegal

 

Maskini Mo Salah machozi yalimlengalenga baada ya fursa yake ya kupiga mkwaju wake wa penati kumponyoka hivi hivi akitazama, kwani tayari mkwaju wa mwenzake Mohamed Abdelmonem ulikuwa umeshagonga mwamba, huku ule wa Mohanad Lasheen ukipanguliwa na kipa Edouard Mendy. Wachambuzi wa spoti wamekosoa uamuzi wa Misri kumweka Salah kuwa mpigaji penati nambari 5, na wamelifananisha hilo la uamuzi wa Ureno wa kumweka Cristiano Ronaldo kuwa mpigaji penti nambari 5 walipochuana na Uhispania katika fainali za Kombe la Euro mwaka 2012. Kama alivyobaki kung'ata kidole Ronaldo karibu mwongo mmoja uliopita kwenye fainali hizo za Ulaya, Salah naye Jumapili alibaki tu kutazama timu yake ikiangukia pua. Maelfu ya mashabiki wa Senegal waliokuwa wamefurika ndani na nje ya uwanja huo, waliripuka kwa shangwe, hoi na vigelegele wakisherehekea ushindi huo. Mafarao walifikaje hapa? Mlinda lango Mohamed Abou Gabaski ndiye aliibuka shujaa wa Misri baada ya kupangua penalti mbili na kusaidia kikosi chake kuididimiza Cameroon mabao 3-1 na kufuzu kwa fainali ya duru ya 33 ya Kombe la Afrika (AFCON) mwaka huu. Mshindi wa mechi hiyo iliyosakatwa Alhamisi usiku aliamuliwa kupitia penalti baada ya pande zote mbili kuambulia sare tasa ndani ya dakika 120. Misri walifuzu kwa nusu-fainali baada ya kukomoa Morocco kwa mabao 2-1 jijini Yaounde. Senegal nao walifuzu kwa fainali ya AFCON baada ya kuisasambua Burkina Faso mabao 3-1 mnamo Jumatano usiku. Fowadi Sadio Mane wa Liverpool alipachika wavuni bao la tatu la Senegal na kufikia rekodi ya Henri Camara aliyekuwa mfungaji bora wa muda wote wa Masimba wa Teranga kwa magoli 29. Abdou Diallo na Idrissa Gueye walifungulia Senegal ukurasa wa mabao katika dakika za 70 na 76 mtawalia kabla ya Burkina Faso kurejea mchezoni kupitia kwa fowadi Blati Toure.

Kwa ushindi huo, Rais Macky Sall wa Senegal ametangaza Jumatatu hii kuwa siku ya mapumziko nchi nzima ili wapate kufurahia na kusherehekea ushindi huo wa kwanza kwa nchi hiyo katika historia ya AFCON. Rais Sall amekatiza safari yake rasmi ya kikazi ya kuitembelea Comoro, ambao ungekua mkondo wa mwisho wa safari zake za kieneo. Tarai alikuwa ameshazitembelea Misri na Ethiopia, lakini ushindi huo wa Senegal umemrudisha mbio Dakar.

Kabla ya kitimutimu hicho cha fainali, wenyeji Cameroon walitoka nyuma kwa mabao 3-0 na kulazimishia Burkina Faso sare ya 3-3 katika muda wa kawaida kabla ya kuwazidi maarifa kwa penalti kwa kufunga mabao 5-3 katika mchuano wa kutafuta mshindi nambari tatu wa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) mnamo Februari 5. Burkina Faso waliwekwa kifua mbele kwa mabao 3-0 kupitia mabao ya Steve Yago, kipa Andre Onana aliyejifunga na Djibril Ouattara. Hata hivyo, Cameroon walichuma nafuu kutokana na wingi wa mashabiki wao wa nyumbani na kurejea mchezoni kupitia kwa Stephane Bahoken katika dakika ya 71 kabla ya nahodha Vincent Aboubakar kufunga mabao mawili ya haraka katika dakika za 85 na 87 mtawalia. Ililazimu mshindi wa mechi kutafutwa kupitia mikwaju ya penalti naye Blati Toure wa Burkina Faso akapoteza mkwaju wake.

Burkina Faso waliondoka uwanjani kwa masikitiko makubwa ikizingatiwa kwamba walitamalaki kipindi kizima cha kwanza na kujiweka katika nafasi ya kudhibiti mechi kufikia dakika ya 49. Cameroon walifunga penalti zao zote. The Indomitable Lions waliokuwa wanawinda taji la AFCON kwa mara ya sita, walifungua kampeni zao za Kundi A kwa kutandika Burkina Faso mabao 2-1 kabla ya kuipepeta Ethiopia 4-1 na kusajili sare ya 1-1 dhidi ya Cape Verde. Waliibandua Comoros katika hatua ya 16-bora kwa mabao 2-1 kabla ya kucharaza Gambia 2-0 kwenye robo-fainali. Meza ya Ulimwengu wa Michezo inawapa kongole Wasenegali kwa kuibuka kidedea, na vilevile kwa mshindi wa pili, Misri na mwenyeji Cameroon aliyefunga orodha ya tatu bora.

..................................TAMATI........................