Jul 10, 2022 02:49 UTC
  • Jumapili tarehe 10 Julai 2022

Leo ni Jumapili tarehe 10 Dhulhija 1443 Hijria sawa na tarehe 10 Julai 2022.

Leo tarehe 10 Dhilhaji ni sikukuu ya Idul Adh'ha, moja kati ya sikukuu kubwa za Kiislamu. Katika siku hii mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu waliokwenda Makka huchinja mnyama kutekeleza amri ya Mola kwa ajili ya kujikurubisha kwake na kuhuisha kumbukumbu ya Nabii adhimu, Ibrahim (as). Mwenyezi Mungu SW alijaribu imani na ikhlasi ya Nabii huyo kwa kumwamuru amchinje mtoto wake kipenzi, Ismail (as), naye akatii na kujitayarisha kuitekeleza. Alimlaza chini na kuanza kukata shingo yake lakini kisu kilikataa kuchinja; ndipo Mwenyezi Mungu alipomtumia mnyama wa kuchinja badala ya mwanawe, Ismail. Tukio hili lenye ibra na mafunzo tele linawafunza wanaadamu somo la kujitoa mhanga, kujisabilia kwa ajili ya Allah, kushinda matamanio na matakwa ya nafsi na kusalimu amri mbele ya amri za Mwenyezi Mungu SW. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu kote duniani kwa mnasaba wa sikukuu hii kubwa.

Siku kama ya leo miaka 1148 iliyopita, wavuvi wa Norway walivumbua kisiwa cha Iceland kilichopo kaskazini mwa bara la Ulaya na karibu na ncha ya kaskazini. Kisiwa hicho kiliingia katika udhibiti wa Norway mwaka 1261 Miladia na karne moja baadaye, Denmark ikazidhibiti nchi mbili zote yaani, Iceland na Norway. Hatimaye mwaka 1944 Iceland ilifanikiwa kupata uhuru kamili kutoka kwa mkoloni Mdenmark.

Bendera ya Iceland

Miaka 281 iliyopita ardhi ya Alaska iligunduliwa na mvumbuzi wa Kidenmark kwa jina la Vitus Bering. Mvumbuzi huyo aligundua ardhi ya Alaska inayopatikana kaskazini magharibi mwa Canada akiwa katika safari yake kuelekea Urusi. Hadi kufikia mwaka 1867 eneo tajiri kwa mafuta la Alaska lilikuwa sehemu ya mamlaka ya Urusi ya Kitezari. Hata hivyo mwaka huo Urusi iliiuzia Marekani ardhi ya Alaska kwa kiasi cha dola milioni saba, eneo ambalo leo hii linahesabiwa kuwa jimbo la 49 la Marekani.

Vitus Bering

Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, Italia ilijiunga rasmi na Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia. Kipindi hicho Waziri Mkuu wa Italia alikuwa ni Benito Mussolini ambaye pia alikuwa kiongozi wa chama cha Ufashisti nchini humo. Kuingia Italia katika vita hivyo hakukumsaidia chochote Hitler, licha ya kwamba kulikuwa na taathira kubwa ya ongezeko la uharibifu. Hadi kipindi cha miaka mitatu, Italia ilikuwa imepata hasara kubwa katika sekta tofauti, huku Benito Mussolini akiuzuliwa madarakani na mfalme wa wakati huo wa Italia mwezi Disemba mwaka 1943, kufuatia kudhibitiwa na waitifaki ardhi ya kusini mwa nchi hiyo.

Benito Mussolini

Siku kama ya leo, miaka 82 iliyopita, Jemedari Henri Petain Waziri Mkuu wa muda na afisa wa ngazi za juu wa jeshi la Ufaransa, alichukua uongozi baada ya Ufaransa kushindwa na Wanazi wa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia. Kwa mujibu wa mkataba wa vita uliosainiwa na nchi mbili hizo tarehe 22 Juni 1940, eneo la kaskazini mwa Ufaransa, ukiwemo mji wa Paris lilibaki chini ya himaya ya jeshi la Manazi wa Ujerumani.

Henri Petain

Katika siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, visiwa vya Bahamas huko Amerika ya Kati vilipata uhuru kutoka Uingereza na siku kama ya leo hufahamika visiwani humo kama siku ya taifa. Visiwa vya Bahamas viligunduliwa mwaka 1492 na mvumbuzi wa Ulaya Christopher Columbus na kuwa chini ya himaya ya Uhispania. Visiwa vya Bahamas vilipata uhuru mwaka 1973 na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Visiwa hivyo viko kaskazini mwa Cuba na kusini mashariki mwa Marekani.

Na tarehe 10 Dhulhija miaka 7 iliyopita katika sikukuu ya Idil Adh'ha ardhi tukufu ya Mina huko Saudi Arabia ilikuwa machinjio ya maelfu ya mahujaji wa Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu kutokana na azembe wa maafisa na wasimamizi wa Hija wa Saudia. Siku hiyo ilishuhudia tukio baya zaidi katika historia ya ibada ya Hija. Tukio hilo lilitokea majira ya saa 3 asubuhi wakati baadhi ya mahujaji walipokuwa wakielekea eneo la Jamarat kumpiga mawe Shetani. Ghafla maafisa wa Saudi Arabia walifunga barabara za kuelekea eneo hilo na kukatokeo msongamano mkubwa kupita kiasi wa maelfu ya mahujaji, suala lililosababisha vifo vya zaidi ya mahujaji 7 kutoka nchi mbalimbali duniani. Mahujaji 464 wa Iran pia waliaga dunia katika tukio hilo ambazo lilidhihirisha tena uzembe na kutokuwa na uwezo wa kusimamia vyema ibada ya Hija wa serikali ya Saudia.  

Maafa ya Mina