Aug 04, 2022 06:41 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhruri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yangu kuwa nyote hamjambo na mko tayari kujiunga nasi katika kipindi kingine cha Sibtain katika Qur'an na Hadithi hii ikiwa ni sehemu ya 39 katika mfululizo wa vipindi hivi ambavyo huzungumzia sifa na fadhila za wajukuu wawili wa Mtume Muhammad (saw) ambao si wengine bali ni Imam Hassan na Hussein. Karibuni…

Ndugu wasikilizaji, Hassan na Hussein bila shaka wanatokana na kizazi kilicho safi na bora zaidi katika jamii ya wanadamu kwa kutilia maanani kwamba ni wajukuu wa Mtume Mtukufu (saw) na miongoni mwa wanawe bora zaidi waliotokana na Imam Ali na binti yake Mtume, Fatwimah (as). Huu ni uamuzi na uteuzi uliofanywa na Mwenyezi Mungu mwenyewe na kwa msingi huo ni heshima na shani kubwa waliopewa watukufu hao kama tulivyotangulia kuona katika vipindi vilivyopita. Uteuzi huo ni fahari kubwa kwetu sisi Waislamu na hasa Mashia wa watukufu hao kutokana na ukweli kwamba sisi ni wafuasi na majani ya mti huo wa Kishia, ambao tumeshikamana na matawi yake kama alivyotutaka tufanye Mtume mwenyewe (saw).

**********

Ndugu wasikilizaji, kama mtu atajipata amepotea jangwani kwenye usiku mkubwa na  kuamua atazame mbinguni ili apate kuongozwa na nyota zilizopo angani, bila shaka iwapo hatakuwa na taasubi wala ubishi usio na msingi ataona huko nyota mbili zenye nuru kubwa ambazo anaweza kunufaika nazo katika kumuelekeza anakotaka kwenda, na hivyo kumfanya afikie lengo lake bila ya kuwa na shaka wala hofu.

Sheikh Swadouq anannukuu Jabir bin Abdallah al-Ansari katika kitabu chake cha Maani al-Akhbar kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Aalihi wa sallam) alisema: Tafuteni njia yenu kupitia jua, na ikiwa litatoweka, tafuteni njia yenu kupitia mwezi, na kama mwezi utatoweka itafuteni kupitia nyota ya Zuhura, na ikiwa nyota ya Zuhura itatoweka, basi itafuteni njia yenu kupitia nyota mbili za Farqad. Wakauliza: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Nini maana ya jua, mwezi, Zuhura na Farqad? Akasema: Mimi ni jua, mwezi ni Ali, Zuhura ni Fatwimah na Farqad ni Hassan na Hussein.

Sheikh Tuosi Pia anamnukuu Sahaba mtukufu Jabir al-Answari katika kitabu cha Aamali akisema kwamba siku moja Mtume Mtukufu (saw) aliwaswalisha swala ya Fajr (alfajiri) na baada ya swala hiyo akawa anazungumza nao kwa kuwaambia: 'Enyi watu! Mtu anayepoteza jua na ashikamane na mwezi, na anayepoteza mwezi na ashikamane na nyota mbili za Farqad.' Hapo Jabir ambaye alikuwa na masahaba wengine Abu Ayyub a-Answari na Anas bin Malik wakamuuliza: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, nini maana ya jua? Akajibu: 'Ni mimi.' Kisha Jabir akasema Mtume aliwatolea mfano kwa kuwaambia: 'Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu alituumba na kutufanya mfano wa nyota za mbinguni. Kila mara mojawapo inapotoweka nyingine hudhihiri. Hivyo mimi ni jua ambapo iwapo nitaondoka basi shikamaneni na mwezi.' Tukauliza: Basi mwezi ni nani? Akajibu Mtume (saw): 'Ni ndugu, wasii, waziri, mlipa-deni langu na baba wa wanangu na khalifa wangu katika Aali zangu, ambaye ni Ali.' Tukauliza: Je, ni nani nyota hizi mbili za Farqad? Akajibu: 'Ni Hassan na Hussein.' Akanyamaza kidogo na kisha kusema: 'Hawa pamoja na Fatwimah ambaye ni ua langu, ndio Aali na Ahlu Bayt wangu. Wako pamoja na Qur'ani na Qur'ani iko pamoja nao, na wala viwili hivi havitatengana hadi vitakaponifikia kwenye Hodhi.'

**********

Ndugu wasikilizaji, Mtume Mtukufu wa Mwenyezi Mungu (saw) hakuaga dunia na kutuacha humu duniani bila kutubainishia misingi yote muhimu ya maisha na dini sahihi ya Mwenyezi Mungu tunayopasa kuifuata katika maisha yetu ya kila siku ili kupata radhi za Muumba wetu. Miongoni mwa misingi hiyo muhimu ni suala la itikadi sahihi ambayo inajumuisha suala zima la Uimamu. Hakufafanua misingi ya uongozi na uimamu tu bali alitaja wazi majina ya watu waliofaa na waliochaguliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Maimamu wa Umma wa Kiislamu baada ya kuaga dunia Mtume Mtukufu (saw). Miongoni mwa Maimamu hao watoharifu na maasumu ni wajukuu wawili wa Mtume Hassan na Hussein (as).

Miongoni mwa masuala muhimu yaliyobainishwa na kufafanuliwa wazi na Mtume ni kuhusu utukufu wa Ahlu wake wema (as). Hafidh bin Asakir ad-Dimashki as-Shafi' anasema katika kitabu chake mashuhuri cha Tarikh Madinat Dimashk akimnukuu Zaid bin Aslam kutoka kwa baba yake kwamba Omar bin al-Khattab alisema: 'Fatemeh, Ali, Hassan na Husein kwenye Pepo wako sehemu inayoitwa "Khatirat al-Quds" chini ya kuba jeupe, ambalo paa lake ni Kiti cha Enzi cha Mwenyezi Mungu.'

Hii ni katika hali ambayo Muhammad bin Abu al-Qassim at-Tabari ananukuu Hadithi hiyo hiyo na wapokezi hao hao lakini kwa maneno yanayotofautiana kidogo katika kitabu chake cha Bisharat al-Mustafa Lishiat al-Murtadha ambapo Mtume (saw) ananukuliwa akisema: 'Fatemeh, Ali, Hassan na Hussein wako Peponi sehemu inayoitwa "Khatirat al-Quds" chini ya kuba jeupe, ambalo paa lake ni Kiti cha Enzi cha Mwenyezi Mungu.'  Ni kuba la utukufu, na Mashia wetu wako upande wa kulia wa Mwingi wa Rehema, Mwenye Baraka na Utukufu.

Nam wasikilizaji wapenzi, watukufu hawa wako kwenye kilele cha utukufu, na walipewa ukhalifa na uimamu kutokana na sifa na fadhila zao aali. Sifa na fadhila hizo ndizo zilizowafanya wapate kufikia daraja hilo la juu la ubora, utukufu na ustahiki wa kuongoza Umma wa Kiislamu. Itakuwaje kinyume na hivi ilihali wanatokana na Mtukufu Mtume (saw)?! Kwa maelezo hayo na kutokana na maneno aliyoyatamka wazi Mtume kuhusiana na Ahlu Bayt wake tena kwa amri ya Mwenyezi Mungu, ni wazi kuwa kila mtu anayezingatia mambo kwa insafu na mwamko atathibitisha bila kusita kwamba watukufu hao ndio waliostihiki kuwaongoza Waislamu baada ya kuaga dunia Mtume (saw).

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji la ziada hatuna ila kukuageni kutoka hapa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka mjini Tehran, tukitumai kwamba tumenufaika sote kwa pamoja na yale tuliyoyasikia katika kipindi cha leo. Basi hadi juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.