Ufufuo na Safari ya Kurejea kwa Allah (6)
Assalamu Aalaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Hamjambo na karibu tena kuwa nasi katika makala ya Ufufuo na Safari ya Kurejea kwa Mola Muumba. Katika kipindi cha wiki iliyopita tulianza kuzungumzia hakika ya mauti na kifo na ajal au kifo ambacho wakati wake hauakhirishwi au kubadilika na kile ambacho yumkini wakati na ajal yake ikabadilika au ajal muallaq. Kipindi chetu leo kitakamilisha maudhui hiyo.
Kama bado mnakumbuka tulisema kuwa kifo ni kanuni jumla kwa ajili ya viumbe vyote na kwamba hakuna kiumbe kitakachobakia hai milele katika dunia hii. Mwenyezi Mungu SW anasema katika aya ya 185 ya Suratu Al Imran kwamba: Kila nafsi itaonja mauti. Na bila ya shaka mtapewa ujira wenu kamili Siku ya Kiyama. Vilevile anasema katika aya za 34 na 35 za Suratu Al Anbiyaa kwamba: Nasi hatukumjaalia mwanaadamu yeyote kabla yako kuwa na maisha ya milele. Basi je! Ukifa wewe, wao wataishi milele? Kila nafsi itaonja mauti; na tunakujaribuni kwa mtihani wa shari na kheri. Na kwetu Sisi mtarejeshwa.
Tulisema kuwa kifo hakina maana ya kuangamia na kutoweka kabisa bali ni kuhama kutoka katika dunia hii finyu na kuelekea katika ulimwengu mwingine mpana zaidi. Tulifananisha dunia hii na fuko la uzazi la mama ambapo kichanga hukua na kupata viungo vya mwili na sifa za kumuwezesha kuishi katika dunia pana na kubwa zaidi ya fuko la uzazi baada ya kutoka katika ulimwengu huo finyu na mdogo na kusisitiza kuwa, kama kichanga hicho ndani ya dunia ya fuko la uzazi, hakitakuwa na maisha katika dunia nyingine itakuwa ni upuuzi na kichekesho kutayarishwa na kupewa viungo na sifa nyinginezo.
Baada ya utangulizi huo tulizungumzia maana ya mauti yenyewe katika mtazamo wa wasomi na wataalamu wa elimu mbalimbali. Wako waliosema kuwa, mauti ni kusimama harakati za ubongo, moyo na hisia tano katika mwili wa mwanadamu na kwamba kifo kina maana ya kuangamia kwa mwili. Mkabala wa wasomi hao wa biolojia kuna wanafalsafa ambao wao waliamini kuwa, mauti ni matokeo ya kutengana nafsi au roho na mwili wa mwanadamu baada ya mwili kupatwa na uharibifu. Kwa upande wake Qur'ani Tukufu imeyaeleza mauti kuwa ni kuchukuliwa roho au nafsi ya mwanadamu na kupelekwa sehemu nyingine ya juu na kamili zaidi. Vilevile wafasiri wa Qur'ani kwa kutegemea aya za kitabu hicho zinazosema kuwa, mauti si kutoweka na kuangamia, wanasema kuwa roho au nafsi ndiyo hakika ya mwanadamu kwa sababu watu wote tunashuhudia kwamba, mwili wa mwanadamu huchakaa na kuhiliki na mwishowe kuwa udongo lakini kile kinachobakia na ambacho ndiyo asili na hakika ya kiumbe ni nafsi na roho yake ambayo huhamishwa na kupelekwa katika ulimwengu mwingine. <<<< >>>>
Tumesema kuwa ajal na mauti ya mwanadamu ni aina mbili. Kuna ajal na mauti ambayo mwanadamu hawezi kuyaakhirisha, na kifo na mauti yanayoshurutishwa na jambo jingine.
Mauti au kifo ni kituo na hatua ya mwisho ya maisha ya hapa duniani na mwanzo wa maisha ya ulimwengu wa Akhera. Kifo au umauti hutokea wakati uliopangwa na Mwenyezi Mungu, na hakuna anayejua wakati wa kutokea kwake isipokuwa Yeye Muumba wa uhai na mauti Subhanahu Wataala. Mwenyezi Mungu katika aya ya 2 ya Suratu al An'am anasema: 'Yeye ndiye aliyewaumba kwa udongo; kisha akapitisha muda; na muda maalumu uko kwake'. Kwa mujibu wa aya hii tukufu ya Qur'ani, kuna aina mbili za mauti. Aina ya kwanza ni mauti au kifo cha kawaida ambacho huitwa 'Ajal Mahtuum'. Aina hii ya kifo kamwe haiwezi kuharakishwa au kucheleweshwa muda wa kutokea kwake. Aina nyingine ya mauti au kifo ni ile ya kabla ya wakati huo mahtuum na usioweza kubadilishwa, ambao huitwa 'Ajal Muallaq'. Mfano wa kifo hicho ni kama kile kinachotokea kutokana na ajali, maradhi na matukio mengineyo. Ili kuweka wazi zaidi suala hili tunatoa mfano wa fanusi au kandili. Iwapo tutawasha fanusi au kandili iliyojaa mafuta na baadaye tukataka kuizima kandili hiyo tunaweza kutumia njia mbili. Moja kati ya njia hizo ni kuiacha iendelee kuwaka hadi mafuta yatakapomalizika na kisha kuzimika yenyewe katika mazingira na hali ya kawaida kutokana na kumalizika mafuta yake. Njia ya pili ni kuzima kandili na taa hiyo kabla ya kumalizika mafuta yake, kuanguka chini na kuzimika au kukumbwa na kimbunga na upepo mkali na kuzima. Vivyo hivyo maisha ya mwanadamu na kifo. Ama huwaka na kuendelea hivyo hadi pale mafuta yaliyowekwa humo yanapomalizika na kuisha, au huzima kabla ya mafuta yake kuisha kutokana na matukio mbalimbali kama kimbunga na upepo mkali, kuzimwa na mwanadamu au kitu kingine. Kuzima kwa aina ya kwanza ndiko kunakoitwa mauti mahtuum yasiyoweza kuakhirishwa kwa sababu ya kumalizika kabisa mafuta yaliyowekwa ndani ya kandili na fanusi, na kule kwa aina ya pili ndiko kunakotajwa kuwa ni kifo muallaq au kinachoshurutihwa na jambo jingine kama upepo na kimbunga au suala jingine.
Ili kuweka wazi zaidi aina hizo mbili za kifo tunatoa mfano mwingine wa tunda. Tunda lolote linalokuwa mtini hudondoka lenyewe na kuanguka chini wakati linapokomaa na kuiva kikamilifu. Hata hivyo wakati mwingine tunda hilo huanguka mapema zaidi kutoka mtini kabla ya kukomaa na kuiva kutokana na matukio kama vile kuvuma upepo mkali au matukio mengine. Vivyo hivyo kwa kifo au mauiti ya kabla ya wakati. Hata hivyo inatupasa kusisitzia hapa kuwa aina zote mbili za mauti na kifo hutokea kwa irada na matakwa ya Mwenyezi Mungu SW.
Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kwamba, matendo na mienendo ya mwanadamu ina taathira katika kuainisha aina ya kifo chake. Vifo vingi vya wanadamu hutokea kwa ajal muallaq au kifo kilichoshurutishwa na cha mapema. Kwa maana kwamba, baadhi ya mambo huwa sababu ya mauti na kifo kutokea mapema. Kwa mfano iwapo mtu hatakuwa makini kuhusu vyakula anavyotumia au hakutunza vyema mwili wake kwa kula vitu visivyo salama kwa mwili, umri wake unaweza kuwa mfupi. Kinyume chake kama atalinda usalama na uzima wa mwili na chakula chake, yumkini angeishi umri mrefu zaidi. Hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu zinaeleza kuwa, baadhi ya vitendo viovu kama kupuuza na kudharau haki za baba na mama, kuwasumbua wazazi wawili, ukatili, kukata udugu, dhulma na kuwakandamiza watu wengine ni miongoni mwa mambo yanayopunguza na kufupisha umri wa mwanadamu. Imepokewa kutoka kwa Imam Jafar Swadiq (as) kwamba amesema: Idadi ya watu wanaofariki dunia mapema kutokana na kutenda dhambi na maasi ni kubwa zaidi kuliko ya wanaofariki dunia kutokana na kumalizika umri wao waliopangiwa, na idadi ya watu wanaoishi umri mrefu kutokana na kutenda wema na ihsani ni kubwa zaidi. Hata hivyo inatupasa kuelewa kuwa, taathira ya matendo hayo ya mja hufanyika katika duara la ajal muallaq na si katika duara la ajal mahtuum. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.