Iran yazalisha asilimia 98 ya dawa inazohitajia
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.
Shirika la Dawa na Chakula la Iran (FDA) limesema asilimia 98 ya dawa zilizoko nchini zinazalishwa na wataalamu wa taifa hili, na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ni miongoni mwa nchi 20 duniani zinazojizalishia dawa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu.
Bahram Daraei, Mkuu wa Shirika la Dawa na Chakula la Iran amesema hayo hivi karibuni katika mahojiano na kueleza kuwa, mafanikio haya yamepatikana licha ya mifumo ya dawa na matibabu ya Jamhuri ya Kiislamu kuwa chini ya vikwazo.
Daraei amenukuliwa na shirika la habari la IRNA akisema hayo na kuongeza kuwa, Marekani inaihadaa dunia kwamba vikwazo vyake havilengi bidhaa za kibinadamu kama dawa.
Afisa huyo wa Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taifa hili lilifanikiwa kuzalisha aina sita za chanjo ya kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO-19, na kwa utataribu huo likafanikiwa pakubwa dhidi ya janga la Corona ambalo linaendelea kusumbua baadhi ya nchi mpaka sasa.
Kadhalika amepongeza mfumo wa afya wa nchi hii, ambao uliundwa na serikali kwa ajili ya kusimamia usambazaji wa dawa kote nchini, jambo ambalo limesaidia kudhibiti magendo ya dawa.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kuwa, vikwazo vya Marekani vinazuia kufikishwa vifaatiba, dawa, teknolojia na ushirikiano wa Iran na taasisi za kifedha za kimataifa, na kuitaja jinai hiyo kama ugaidi wa kimatibabu.
Teknolojia ya nano yatia fora Iran
Kwingineko, Taarifa ya Makao Makuu Maalum kwa ajili ya Maendeleo ya Nanoteknolojia nchini Iran imesema Bidhaa za "nanoteknolojia" za Iran sasa zitauzwa katika nchi 47 ambazo zimetuma maombi ya kupokea bidhaa hizo.
Taasisi hiyo imeongeza kuwa: Bidhaa na huduma za nanoteknolojia katika nyanja mbalimbali za ujenzi, optoelectroniki, dawa, afya na tiba, vitambaa na nyanja nyingine za teknolojia zinasafirishwa katika nchi 47 zilizoomba.
Iran ni miongoni mwa nchi tajika katika uga wa teknolojia ya nano katika ngazi ya kimataifa, na wanateknolojia Wairani wameweza kurekodi mafanikio muhimu katika uwanja huo.
Sekta hii, kwa msaada na uwezo wa wataalamu wa ndani ya nchi, imeweza kuharakisha njia yake ya maendeleo na kufanya bidhaa na huduma zake kuwa na ufanisi Iran na kimataifa.
Kwa mujibu wa ripoti ya Makao Makuu Maalum kwa ajili ya Maendeleo ya Nanoteknolojia katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Sayansi na Teknolojia, bidhaa na huduma za nanoteknolojia za makampuni ya Iran yanayotumia maarifa katika nyanja mbalimbali za ujenzi, optoelectroniki, dawa, afya na tiba, nguo na teknolojia nyinginezo zimesafirishwa katika nchi 47 ambazo zimeomba bidhaa hizo. Kati ya nchi zilizoomba bidhaa hizo ni pamoja na Uturuki, Iraq, Lebanon, Afghanistan, Georgia, Syria, Russia, Pakistan, Tajikistan, India na Kazakhstan.
Kiasi kikubwa zaidi cha mauzo ya nano ya Iran ni kwa Uturuki yenye thamani ya dola milioni 13, Iraq yenye thamani ya dola milioni 12 na Lebanon yenye thamani ya dola milioni 3.4 mtawalia. Afghanistan, Georgia na Syria ndizo zinazofuata.
Sehemu kubwa zaidi ya mauzo ya nje ya bidhaa za nano za Iran inahusiana na sekta ya ujenzi, ambayo inachukua asilimia 53%.
WHO yasema janga la COVID-19 halijaisha
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema watu hawapaswi kujisahau wala kuchukulia janga la COVID-19 kama limeisha duniani kwani bado lipo na linaendelea kuuawa mamilioni ya watu.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 25 jijini Geneva Uswisi Dkt Tedros amesema “Hatuwezi kusema tunajifunza kuishi na COVID-19 wakati watu milioni moja wamekufa na COVID-19 mwaka huu pekee.”
Amewaambia waandishi wa habari kuwa miaka miwili na nusu ya janga la COVID-19 duniani “tuna nyenzo zote tunazohitaji za kuzuia vifo vinavyotokana na janga hili.”
Ametoa wito kwa serikali zote ulimwenguni kuimarisha juhudi zao za kutoa chanjo kwa wahudumu wote wa afya, wazee, na wengine walio katika hatari kubwa zaidi, mbinu hii ikiwa ni moja katika njia za kuweza kufikia utoaji wa chanjo ya COVID-19 kwa asilimia 70 kwa watu wote.
Akipongeza juhudi za kuendelea kutoa chanjo Mkuu huyo wa WHO ameseme “Inafurahisha kuona kwamba baadhi ya nchi zilizokuwa na viwango vya chini zaidi vya chanjo sasa zinainuka hususan barani Afrika.”
Ameongeza kuwa "Inafurahisha sana kuona kwamba utoaji chanjo unazingatia makundi yanayohitajika kupewa kipaumbele huku nchi nyingi zikipiga hatua ya kuvutia katika kutoa chanjo kwa asilimia 100 ya wafanyakazi wa afya na asilimia 100 ya wazee.”
Hata hivyo Dkt. Tedros amesema bado mengi zaidi yanahitajika kufanywa ili kutokomeza janga hilo la Afya ulimwenguni.
Maabara inayotembea inayotembea Tanzania
Wadau wa elimu nchini Tanzania wamebuni maabara inayotembea ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi katika shule za msingi na secondary ambazo zina uhaba wa vifaa vya masomo ya sayansi kwa lengo la kufundishia kwa vitendo na kuwahamasisha kuyapenda masomo hayo.
Hatua hiyo inalenga kufikia lengo namba 4 la malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa linalohimiza elimu bora yenye usawa na kukuza fursa za kujifunza maishani kwa wote ifikapo mwaka 2030.
Bilauri za vioo, plastiki, mapulizio, Box, chupa za maji, na karatasi laini (Tissue) ni miongoni mwa vifaa vya kufundishia masomo ya biolojia, chemia na fizikia ambavyo kwa kawaida hupatikana majumbani na madukani, lakini sasa vimegeuzwa matumizi maeneo ya shule na kugeuka kuwa mkombozi kwa wanafunzi wa shule za msingi na secondary nchini Tanzania.
Wilson Kamunye, ni mwakilishi wa Shirika la sayansi duniani upande wa bara la Africa, ambaye ndiye aliyebuni maarifa haya kwa kutafuta uwepesi huu kwa wanafunzi kushiriki katika masomo ya sayansi kwa kubuni njia hii ya kufundishia masomo hayo kwa kutumia vifaa rahisi ambavyo wakati mwingine huvibeba na kwenda katika shule za msingi na secondary nchini Tanzania.
Wilson ameamua kutumia njia hii ya Maabara inayosafiri, ambapo huchukua vifaa vyake na kwenda katika shule nchini Tanzania ambazo zina changamoto ya upungufu wa vifaa vya sayansi hivyo kutumia nafasi yake kuwafundisha wanafunzi kwa vitendo zaidi.
Kwa mujibu wa Kamunye hii ni Maabara inayofika katika maeneo mbalimbali kwa kuchukua vifaa vyepesi vinavyobebeka na vinavyopatikana kwa urahisi katika maeneo mengi na kuviweka katika sehemu maalumu ya kutunzia kisha kuondoka navyo hadi katika eneo ama shule husika.
Malengo ya Kamunye ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wa Tanzania na mataifa ya Afrika wanasoma masomo ya sayansi kwa vitendo ili kupata wanasayansi mahiri hapo baadaye.
Hata hivyo vyombo hivyo hubebwa katika makontena ya kubebea vifaa na kufikisha huduma katika maeneo ambayo hayana maabara ili kuweka urahisi wa kufundisha watoto.
Kwa miaka mingi nchini Tanzania kumekuwa na upungufu wa maabara katika shule za msingi na upili hali ambayo imekuwa ikisababisha wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kuishia kukariri na kupata majaribio ya vitendo kwa kiasi kidogo.
Baadhi ya shule hususan zile za upili zimekuwa zikienda kuazima vifaa vya kufanyia majaribio katika shule jirani ili kuwezesha wanafunzi kusoma kwa vitendo hali inayowafanya wengine kuishia njiani na kuamua kusoma masomo ya sanaa.
Baadhi ya shule za msingi zinazomilikiwa na serikali hazima maabara ya masomo ya sayansi hivyo huishia tu kuona vifaa hivyo kwenye michoro ya vitabu wakisubiria watakapofika shule ya upili ndipo waanze kuviona kwa uhalisia na kujifunza matumizi yake.
Kwa mujibu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tamisemi katika mwaka wa fedha 2018/19 ilijenga maabara 165 za masomo ya sayansi katika shule mbalimbali nchini huku ikitaka kila shule inayofundisha masomo ya sayansi kuwa na maabara tatu za masomo ya Fizikia, Kemia na Baiolojia.
Naam na kwa habari hiyo kuhusu maabara inayotembea Tanzania ndio tunafika mwisho wa makala yetu ya sayansi na teknolojia.