Nov 10, 2022 14:51 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (33)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 33 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitazungumzia akhlaqi za kiutamaduni katika Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Moja ya vielezi vya kuyatathmini mataifa ni tamaduni na staarabu zao. Kwa sababu hiyo, kila taifa linapokuwa na ustaarabu na utamaduni mkongwe na wa kale zaidi, ndivyo linavyokuwa na nafasi na hadhi ya juu zaidi.

Kwa mtazamo huu na kwa kuzitalii nyaraka na ushahidi thabiti na usio na shaka wa historia, tunaweza kusema kuwa, Mitume wa Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa waasisi wa tamaduni na staarabu za mwanzo za jamii ya wanadamu. Na sababu ni kwamba, akthari yao walidhihiri na wakatangaza na kueneza dini zao katika kaumu na mataifa ambayo kabla ya kudhihiri wao, jamii za mataifa na kaumu hizo hazikuwa na misingi ya kiutamaduni inayoridhisha.

Moja ya mifano mashuhuri na ya wazi zaidi inayotoa taswira ya hali hiyo katika historia ya tamaduni na staarabu ni wa zama za kubaathiwa na kupewa Utume Nabii Muhammad SAW. Zama ambazo katika historia zimesajiliwa kwa anuani ya zama za ujahilia; ikiwa na vielelezo vya ujinga na ujahili, ufisadi na maovu, ubaguzi na upendeleo wa kidhalimu, kujikweza na kujitukuza kwa sababu za kikoo na kikabila, kujilimbikizia mali na utajiri, kuabudu masanamu, kushamirisha utumwa, kuwagawa watu kimatabaka, kukosekana uadilifu, kushupalia dhulma na uonevu na kupora haki za wanyonge.

Bwana Mtume SAW alidhihiri katika zama na mazingira hayo; na katika kuendeleza harakati zilizoanzishwa na Mitume wengine wa Mwenyezi Mungu waliotangulia, akaanzisha mapinduzi makubwa na ya msingi na kuleta mageuzi ya kujenga ustaarabu mpya.

Ni jambo la kutafakarisha mno kwamba katika jamii ambayo hakukuwepo ndani yake athari yoyote ya elimu na usomaji vitabu, huku akthari ya watu wake wakiwa hawana ujuzi wowote wa kusoma na kuandika wala kutambua kalamu ni kitu gani, aya ya mwanzo ambayo aliteremshiwa Bwana Mtume na Malaika wa wahyi katika pango la Hira ilihusu kusoma na kuandika, kama alivyosomewa aya hiyo hadi ya tano ya Suratul A'alaq kwa kuambiwa: " Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui.

Hakuna shaka kuwa, kama Bwana Mtume SAW angeanzisha mapinduzi yake ya kiutamaduni katika nchi zilizoendelea na kustaarabika, lisingekuwa jambo la kushangaza; lakini kuweza kufanya hivyo katika umma wa watu waliokuwa wameghariki kwenye dimbwi la ujinga, ambapo kwa kutumia mwanga wa wahyi alioteremshiwa alifanikiwa kujenga jamii yenye utamaduni na ustaarabu mkubwa na kuufanya Ulimwengu wa Kiislamu, kama wanavyokiri wanafikra wa Magharibi na wataalamu wa ulimwengu wa Mashariki, kitovu cha utamaduni na ustaarabu wa dunia kwa karne kadhaa wa kadhaa, hilo ni jambo ambalo limewastaajabisha na kuwashangaza wengi.

Aya ya pilii ya Suratul-Jumua inalielezea hilo kama ifuatavyo: "Yeye ndiye aliye mpeleka Mtume kwenye watu wasio jua kusoma, awasomee Aya zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri".

Inatosha kujua tu kwamba neno elimu limetajwa mara 775 ndani ya Qur'ani; kufikiri mara 479 na kutumia akili mara 49, mbali na kuashiriwa mara kadhaa wa kadhaa watu wenye hekima wanaotafakari.

Lakini ukiachilia mbali hayo, na kwa ajili ya kuwafanya watu watambue hekima za uumbwaji wa vitu vingi na vyenye siri kubwa vya ulimwengu, Mwenyezi Mungu Mtukufu ameviapia vitu hivyo ikiwemo ardhi na mbingu, usiku na mchana, bahari n.k; na kuwataka wajuzi na weledi wa mambo watafiti hadi kwenye anga za mbali na kwenye vina vya chini kabisa vya bahari ili waweze kugundua maajabu ya ulimwengu wa maumbile na kumtambua zaidi na zaidi Yeye Mola Mwenye Hekima, Mlezi na Muumba wao; na kwa kufanya hivyo wabainikiwe na uhakika huu kwamba, chochote chenye ukubwa zaidi ya vitu vyote, na chochote kilicho kidogo zaidi ya kila kitu, kimeumbwa kwa hekima ya Mwenyezi Mungu na kwa lengo maalumu.

Bwana Mtume SAW, ambaye hakuwahi kuhudhuria darsa au masomo kwenye madrasa, chuo au kwa mwalimu yeyote yule; huku dhati na nafsi yake ikiwa inang'ara kwa nuru ya elimu na hekima za mbinguni alizotunukiwa na Mola wake, alikuwa kila mara akiwashajiisha masahaba zake kwa aya za wahyi alizokuwa akiteremshiwa, juu ya kutafuta na kujifunza elimu. Siku moja mtukufu huyo aliingia msikitini akawakuta watu wamekusanyika pamoja kwenye makundi mawili. Kundi moja lilikuwa la watu waliokuwa wameshughulika kufanya ibada na watu wa kundi la pili walikuwa wameshughulika kusomeshana na kujadiliana juu ya masuala ya elimu. Bwana Mtume alifurahi kwa kuwaona masahaba zake wako katika hali ile na akaongezea kwa kusema: makundi yote mawili yana thamani, lakini mimi nimetumwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuwafunza watu na kuwaongezea ujuzi na uelewa wao." Baada ya kunena hayo, alielekea na kukaa kwenye kundi la watu waliokuwa wanajadiliana kuhusu masuala ya elimu. (Dastan Rastan).

Bwana Mtume SAW, ambaye alitumwa na Mwenyezi Mungu Mjuzi na Mwenye hekima ili kuja kuwafundisha watu kitabu na hekima, mbali na sira ya mwenendo wake, alijitahidi pia kila mara kutoa miongozo ya kuongeza uelewa wa watu katika jamii na kudumisha hisia za kupenda elimu ndani ya nafsi zao. Mtukufu huyo alikuwa akiwaambia watu: "Yeyote anayepiga hatua ya kwenda kutafuta elimu, Mwenyezi Mungu humwelekeza kwenye njia ya peponi, Malaika humkunjulia mbawa zao kwa furaha na wakazi wa ardhini, mbinguni na samaki wa baharini humuombea maghufira. (Usulul-Kafi, Kitabu cha Sura ya Elimu)

Moja ya sifa maalumu iliyopo katika utamaduni wa akhlaqi za kutafuta elimu wa Uislamu unaoifanya dini hiyo izipiku na kuzishinda njia nyingine za kifikra ni ikhlasi ya tauhidi anayokuwa nayo mtu katika mwenendo wa kujifunza elimu na kuwafunza wengine. Sababu ni kuwa baadhi ya watu hutafuta elimu kwa ajili ya kujipatia utajiri na madaraka, na kuna watu wanaofanya hivyo kwa madhumuni ya kujipatia umaarufu. Lakini katika utamaduni wa Kiislamu, pamoja na kwamba elimu inawapa watu nguvu na uwezo na kuwaletea mali na utajiri, lakini kwa Muislamu, harakati zake zote za kutafuta elimu zinatakiwa zifanyike kwa nia moja tu ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Anapokuwa hivyo, huwa kama alivyosema Bwana Mtume SAW ya kwamba: "kuwafundisha wengine elimu kwa lengo la kupata radhi za Mwenyezi Mungu ni amali njema, kujifunza elimu ni ibada, mazungumzo ya kielimu ni sawa na kuleta tasbihi, kuitumia elimu ni jihadi, kumfunza asiyejua ni sadaka na kwa anayestahiki humkurubisha mtu kwa Mwenyezi Mungu. (Biharul-Anwar). Na kwa Hadithi hiyo ya Bwana Mtume SAW niseme pia mpendwa msikilizaji kwamba, sehemu ya 33 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 34 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/