Akhlaqi Katika Uislamu (35)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 35 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitaendelea kubainisha nukta nyingine za mafunzo ya akhlaqi za dini tukufu ya Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.
Katika sehemu iliyopita ya 34 tulionyesha jinsi elimu na imani zisivyoweza kutenganishwa katika mfumo wa kiutamaduni wa Uislamu na tukabainisha kuwa kama elimu na imani zitaweza kwa pamoja kuvifikia vilele vya ujuzi na utaalamu unaompatia mwanadamu saada, fanaka na ukamilifu wa kiutu, katika hali hiyo, maulamaa na wataalamu watatekeleza ipasavyo jukumu na masuulia hasasi na mazito waliyonayo kwa jamii ya wanadamu; na katika hali hiyo hawatatekwa na vivutio vya kupita vya wenye utajiri wa mali na nguvu za madaraka; jambo ambalo litawawezesha kutoa mchango unaostahiki katika nyuga zote za maisha ya watu.
Sifa nyingine maalumu ya akhlaqi za kiutamaduni za Uislamu wa asili ni kuwafunza wafuasi wake kwamba, ili kuongeza uelewa, utambuzi na ufahamu wa mambo; watalii, wasome, wasikilize na kutathmini kwa umakini mkubwa fikra na mitazamo mbalimbali, kisha wachague kufuata iliyo bora zaidi kati ya hiyo bila kufanya taasubi au kuathiriwa na fikra mgando za inadi na ukaidi. Huu ni ushahidi wa wazi na ithibati tosha kwamba, mfumo wa akhlaqi za kiutamaduni wa dini tukufu ya Uislamu unashajiisha uhuru wa rai na fikra ili kuwajenga na kuwaongezea watu elimu na ujuzi wa mambo.
Katika kuwaenzi na kuwasifu watu wenye sifa hiyo ya kutumia akili na busara na kutalii fikra na mitazamo mbalimbali bila ukereketwa, taasubi au kuwa na mgando wa kifikra, Mwenyezi Mungu Mola Mjuzi na Mwenye hekima amemhutubu Mtume wake, Nabii Muhammad SAW kama inavyoeleza aya ya 17 na 18 za Suratu-Zumar ya kwamba: "Na wale wanao jiepusha na ibada potovu, na wakarejea kwa Mwenyezi Mungu, watapata bishara njema. Basi wabashirie waja wangu. Ambao husikiliza maneno, wakafuata lilio bora yao. Hao ndio alio waongoa Mwenyezi Mungu, na hao ndio wenye akili."
Kuna nukta muhimu kadhaa za kutafakari kuhusiana na maneno haya ya wahyi. Moja ni kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu anawapa bishara watafutao ukweli, ambao wana utayari na uwezo wa kusikiliza maneno na kauli zozote zile; ikimaanisha kwamba, anawatazama kwa jicho maalumu la rehma watu wa aina hiyo wenye fikra huru; na hiki ni kielezi na kipimo muhimu kinachopasa kutumiwa katika taasisi za watafiti ili waweze kubaini hakika na ukweli wa kielimu bila kuathiriwa na hisia za chuki zisizo na sababu juu ya fikra na rai fulani.
Nukta nyingine iliyomo katika aya hizi ni kuwa, watu walio huru kifikra hufanya uhakiki na uchunguzi wa kina juu ya rai, mitazamo na fikra mbalimbali, kisha huchagua iliyo bora zaidi kati yao, kwa sababu huwa hawana fikra mgando, taasubi na ukereketwa wa kibubusa juu ya mambo. Nukta yenye kutoa mguso maalumu hapa ni jinsi aya zinavyotuonyesha kuwa, bila kupitia yeyote au chochote, Mwenyezi Mungu Mwenyewe ndiye anayewaongoza watu hao kufikia uongofu wa kubaini haki na ukweli na kuwaepusha na kufuata njia pogo ya kuwapotezea muda na fursa za kuifahamu kweli.
Na nukta ya mwisho ya kutafakari katika aya hizi ni kwamba, Mwenyezi Mungu analitaja kundi la watu walio na utayarifu wa kusikiliza maneno, rai na fikra yoyote na hatimaye kufuata iliyo bora zaidi, kwamba hao ni watu wenye hekima, kwa kuwa na uwezo wa kina wa kupima na kutafakari mambo. Hakuna shaka kuwa, watu wenye sifa hizi, ambao daima huwa na idili na hima kubwa ya kuujua ukweli, hufanya juhudi za kuongeza upeo wa elimu na uelewa wao ili waweze kuangaziwa na mwanga mpya wa ujuzi na utaalamu wa mambo.
Moja ya njia kuu za kumfikisha mtu kwenye lengo hilo tukufu ni kuwa na kiu ya kujifunza na kuwa na uelewa mkubwa zaidi wa ubunifu na mafanikio ya kielimu yaliyofikiwa na watafiti na wahakiki mbalimbali duniani.
Kuhusiana na suala hilo, Bwana Mtume SAW amesema: "Aliye mjuzi zaidi katika watu ni yule (achotaye kutoka kwenye hazina ya elimu za watu wengine) na kuongezea katika elimu yake". Amali Saduq 4/27
Kama tulivyotangulia kueleza, moja ya njia kuu na ya kivitendo ya kumfanya mtu awe huru kifikra katika kufahamu na kubaini haki na ukweli ni kuweka kando misimamo ya ukereketwa na taasubi inayomtia upofu wa kushindwa kuyatafakari mambo kwa kina na kuishia kufuata fikra potofu.
Ili kumuepusha mtu mwenye busara na kiu ya kujua ukweli asije akaangukia kwenye lindi la njia potofu, Imam Ali (AS) anamtanabahisha kwa kumwambia: "Yakubali (maneno ya) haki yatokayo kwa wafuataji njia ya batili, na yakatae (maneno ya) batili (na yasiyo na mantiki) yatokayo kwa wafuataji njia ya haki. Na jitahidi kuchunguza kauli zitolewazo na wengine (ili ubanikiwe na haki)". Biharul- Anwar, 2/ 96
Mwongozo huu wa hekima wa Imam Ali (AS) ni dhihirisho kamili la mtu kuwa huru kifikra kwa maana yake halisi, kwa sababu unaonesha kwamba, kipimo cha kufuata maneno na fikra ni kuwa kwake ya haki na mantiki, si muelekeo wake wa kidhahiri tu usio na msukumo wala mashiko ya kimantiki.
Bwana Mtume Muhammad SAW ameizungumzia kwa sura nyingine maudhui hii aliposema: "Maneno ya hekima ni kipoteo cha muumini, basi popote akipatapo, yeye hustahiki zaidi kuwa nacho". Biharul-Anwar 2/99/58.
Ni mantiki na ndivyo inavyotarajiwa, kwamba wakati mtu anapopotelewa na kitu cha thamani, hatoacha kufanya kila jitihada usiku na mchana na kuchukua kila hatua inayolazimu mpaka akipate. Kwa mtu muumini, aliye na imani itokanayo na uelewa wa misingi ya fikra na matendo anayofanya, maneno ya hekima ni kipoteo chenye thamani kubwa zaidi kwake. Kwa hivyo anapokikuta popote pale na kwa mtu yeyote yule hapati raha wala utulivu mpaka ahakikishe amekipata. Imam Ali (AS) ambaye anasifika mbele ya kila mtu kwa kauli na semi zake za hekima ametuusia katika moja ya maneno yake ya hekima yanayofanana na tuliyonukuu kutoka kwa Bwana Mtume SAW, kwa kusema: "Hekima ni kipoteo cha muumini, kwa hiyo hufanya juhudi za kukipata, hata kama kitakuwa mikononi mwa mtu mnafiki". Nahjul-Balagha/hekima ya 80.
Mpendwa msikilizaji, hitimisho la mazungumzo yetu ya leo linatufikisha kwenye nukta ya msingi na mantiki ya kwamba, hakuna njia yoyote ya kifikra inayoufikia Uislamu katika kumfanya mwanadamu awe huru kifikra; na hii ndio njia bora ya kumfikisha mwanadamu kwenye utambuzi na uelewa wa haki na ukweli na kumlinda na machaguo ghalati na potofu. Na kwa maelezo hayo, niseme pia kwamba, sehemu ya 35 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 36 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/