Dec 05, 2022 02:47 UTC
  • Jumatatu tarehe 5 Disemba mwaka 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 10 Jumadil Awwal 1444 Hijria sawa na Disemba 5 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 152 iliyopita, aliaga dunia Alexandre Dumas mwandishi mtajika wa Kifaransa. Mwandishi huyo ambaye ni mashuhuri pia kwa jina la Dumas Baba baada ya kumaliza masomo yake aliajiriwa katika ofisi moja ya kiwanda kama katibu kutokana na kuwa na hati nzuri.

Alexandre Dumas

Katika siku kama ya leo miaka 148 iliyopita, Iran ilijiunga na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu. Jitihada za awali za Iran kutaka kujiunga na shirika hilo zinarejea nyuma katika kipindi cha utawala wa Mfalme Nassereddin Shah Qajar. Katika kipindi cha utawala wake, Disemba 1874 Iran iliukubali mkataba uliopasishwa Geneva Uswisi, lakini licha ya kupita miaka kumi tangu isaini mkataba huo, utawala wake haukuchukua hatua yoyote ile ya kuasisi taasisi au jumuiya ambayo itatekeleza hati ya mkataba huo hapa Iran.

Miaka 121 iliyopita katika siku kama ya leo,  alizaliwa Walt Disney shakhsiya mashuhuri wa sekta ya filamu za watoto. Disney alizaliwa katika mji wa Chicago huko Marekani. Walt Disney alihitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Havard na kutunukiwa shahada ya udaktari katika sayansi ya uchoraji na uchongaji (Fine Art). Disney alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha sanaa ya filamu za katuni. Mara kadhaa alitunukiwa tuzo za Oscar katika uwanja huo wa kutengeneza filamu za katuni. Miongoni mwa kazi muhimu za Walt Disney ni Snow White, The Seven Dwarfs, Polar Bears.

Walt Disney

Siku kama ya leo miaka 9 iliyopita alifariki dunia shujaa wa mapambano ya ukombozi na kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela akiwa na umri wa miaka 95. Mandela alizaliwa mwaka 1918 na alitumia zaidi ya nusu ya umri wake akipambana na utawala wa kibaguzi nchini kwake. Utawala wa wazungu wabaguzi ulimfunga jela kwa kipindi cha miaka 27 hadi mfumo wa ubaguzi wa rangi ulipofutwa mwaka 1990. Mwaka 1994 wananchi wa Afrika Kusini walimchagua Nelson Mandela kuwa Rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo. Baada ya kushika hatamu za uongozi, Mandela aliamiliana vyema na watala wa zamani wa mfumo wa ubaguzi wa rangi na hata wale waliomfunga jela na kumtesa. Mwenendo huo wa kusamehe ulizidisha umashuhuri na kupendwa shujaa huyo, na mwaka 1993 alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel. Kitabu mashuhuri zaidi cha shujaa huyo wa Afrika ni kile chenye kumbukumbu zake alichokipa jina la: "Njia Ndefu ya Kuelekea kwenye Uhuru".

Mzee Nelson Mandela

Na leo Disemba 5 ni Siku ya Kimataifa ya Wahisani ambao hujitolea kwa hali na mali kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wengine. Kutenda wema na kufanya hisani ni suala ambalo halihusu, dini, taifa, wala kaumu makhsusi. Hata hivyo Uislamu ambayo ni dini ya mwisho ya Mwenyezi Mungu, umehimiza zaidi kutenda wema na hisani na kuwataja wahisani na watenda wema kwamba ni vipenzi vya Mwenyezi Mungu. Sehemu ya Aya ya 195 ya Suratul Baqara inasema: Na fanyeni wema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wahisani.

 

Tags