Dec 27, 2022 02:27 UTC
  • Jumanne tarehe 27 Disemba 2022

Leo ni Jumanne tarehe 3 Jumadithani 1444 inayosadifiana na tarehe 27 Disemba 2022.

Siku kama ya leo miaka 1433 iliyopita alikufa shahidi Bibi Fatima al Zahra, binti mtukufu wa Mtume wetu Muhammad (saw) na mke wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Alizaliwa miaka mitano baada ya kubaathiwa Nabii Muhammad (saw) na mtukufu huyo akampa jina la Fatima. Alipewa malezi na wazazi wake wawili yaani Bibi Khadija na Mtume wa Mwenyezi Mungu na kupata maarifa aali ya dini kutoka kwa baba yake. Bibi Fatima alifikia daraja za juu za ukamilifu wa kiroho na kimaanawi ndani ya nyumba ya wahyi na ufunuo. Baada ya kuolewa na Imam Ali bin Abi Twalib ambaye alikuwa kielelezo halisi cha takwa na uadilifu, Bibi Fatima alikuwa na nafasi kubwa na alitoa mchango wa aina yake katika jamii ya Kiislamu. Alikuwa dhihirisho la uchamungu, ukarimu, kujitolea, subira, kujipinda katika ibada na kuwasaidia watu wote na alilea watu adhimu kama Imam Hassan na Hussein (as).

Siku kama ya leo miaka 785 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria alifariki dunia Abu Bakr Muhammad bin Ahmad maarufu kwa jina la Ibn Sayyidun-Naas, faqihi, mtaalamu wa hadithi, mwanahistoria na msomi wa fasihi wa Andalusia au Hispania ya leo. Mwanazuoni huyo alifariki dunia nchini Tunisia. Ibn Sayyidun-Naas alizaliwa mwaka 597 Hijiria katika viunga vya mji wa Seville (Ishbilia) huko Uhispania na kuanza kujishughulisha na masomo. Abu Bakr Muhammad bin Ahmad alifundisha kwa miaka mingi katika eneo hilo na kulea wanafunzi wengi. Msomi huyo alitabahari pia katika taaluma ya mashairi na fasihi; na mashairi yake mengi yanamsifu Mtume Muhammad (saw). Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni kile cha Sira na Maisha ya Mtume Muhammad (saw).

Miaka 200 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Louis Pasteur, tabibu na mwanakemia wa Kifaransa. Akiwa shuleni Louis Pasteur alisoma kwa bidii na jitihada kubwa. Baada ya kumaliza masomo yake alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika kemia na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Strasbourg huku akijihusisha uhakiki na utafiti kuhusiana na masuala mbalimbali ya kielimu. 

Louis Pasteur

Katika siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ulianzishwa. Miongoni mwa yaliyokuwa malengo muhimu ya mfuko huo, ni kuandaa nafasi zaidi za ajira, udhibiti wa thamani ya sarafu za kigeni na kuhakikisha kwamba, kunakuweko ukuaji wenye uwiano katika masoko ya kimataifa. Makao Makuu ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa yako mjini New York Marekani.

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, kufuatia kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, mkataba wa kihistoria wa kuigawa Peninsula ya Korea ulitiwa saini mjini Moscow. Mkataba huo ulitiwa saini na wawakilishi wa nchi tatu za Uingereza, Marekani na Umoja wa Sovieti. Kwa mujibu wa mkataba huo, Peninsula ya Korea ambayo hadi katika zama hizo ilikuwa nchi moja ikagawanywa katika sehemu mbili. Kwa utaratibu huo, kukatokea nchi mbili za Korea ya Kaskazini na Kusini mgawanyiko ambao ungalipo hadi leo.

Katika siku kama ya leo miaka 15 iliyopita Bi Benazir Bhutto kiongozi wa Chama cha Wananchi cha Pakistan (PPP) aliuawa kwa kufyatuliwa risasi na mlipuko wa bomu uliofanywa na magaidi huko Rawalpindi kaskazini mashariki mwa Pakistan. Mbali na Bi Benazir Bhutto, watu wengine karibu 20 wafuasi wa chama cha PPP waliuawa pia katika mlipuko huo. Bhutto alikuwa Waziri Mkuu wa Pakistan kwa mara ya kwanza mwaka 1988 baada ya kuenguliwa madarakani serikali ya kijeshi iliyokuwa ikiongozwa na Jenerali Muhammad Zia ul Haq.

Bi Benazir Bhutto

Na katika siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha hujuma kubwa na ya pande zote dhidi ya Ukanda wa Gaza magharibi mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wakazi wa eneo hilo waliwakasirisha viongozi wa Kizayuni kutokana na kupambana kwao kishujaa dhidi ya uchokozi na mashambulizi ya Wazayuni na pia hatua yao ya kuiunga mkono serikali halali ya Palestina iliyokuwa ikiongozwa na harakati ya Hamas. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Ukanda wa Gaza ukawekwa chini ya mzingiro wa kiuchumi wa utawala haramu wa Israel kwa karibu mwaka moja na nusu kabla ya mashambulizi hayo, mzingiro ambao unaendelea kuwasababishia Wapalestina wa eneo hilo matatizo chungu nzima kama vile ukosefu wa chakula na dawa.

Mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza

 

Tags