Jan 08, 2023 11:01 UTC
  • Hakika ya Uwahabi 7

Moja ya itikadi zinazowapelekea Mawahabi kuharamisha ujenzi wa majengo na makuba kwenye makaburi ya Manabii na Maimamu watukufu (as) na kuwakufurisha Waislamu wanaozuru maeneo hayo matakatifu pamoja na kuwatuhumu kuwa ni washirikina ni fikra zao potofu kuhusiana na suala zima la tawassul, au kwa ibara nyingine kutawasali na mawalii wa Mwenyezi Mungu.

Bismillahir Rahmanir Raheem, tunaanza kipindi hiki kwa jina la Mwenyezi Mungu ambaye hakuna hakika nyinyine ya kweli na ya asili humu duniani isipokuwa Yeye. Salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya wanaotafuta hakika na ukweli ambao licha ya makelele na fitina zote zinazoenezwa ulimwenguni dhidi yao lakini hilo haliwaathiri bali wameazimia kufanya kila linalowezekana ili kufikia sauti ya ukweli na hakika inayotuliza nyoyo.

Katika kipindi kilichopita tulisema kwamba kwa mtazamo wa Mawahabi, ujenzi wa mijengo na makuba kwenye makaburi ya Manabii na Maimamu (as) ni haramu lakini tukaona kuwa itikadi hiyo potofu inapingana wazi na Aya na mafundisho ya Qur'ani Tukufu na miongozo ya viongozi wa dini. Katika kipindi hiki tunatazamia kujadili itikadi nyingine isiyo sahihi ya pote hilo la Mawahabi, itikadi ambayo huenda ikawa inatokana na uharamishaji wao wa ujenzi wa majengo kwenye makaburi ya mawalii na viongozi watukufu wa dini.

************

Moja ya itikadi zinazowapelekea Mawahabi kuharamisha ujenzi wa majengo na makuba kwenye makaburi ya Manabii na Maimamu watukufu (sa) na kuwakufurisha Waislamu wanaozuru maeneo hayo matakatifu pamoja na kuwatuhumu kuwa ni washirikina ni fikra zao potofu kuhusiana na suala zima la tawassul, au kwa ibara nyingine kutawasali na mawalii wa Mwenyezi Mungu. Kwa mtazamo wa Mawahabi, mtu anayetawasali na viongozi wa dini na kuwaomba msaada huwa amewafananisha na kuwasawazisha na Mwenyezi Mungu na hivyo kuwa na waabudiwa wawili.

Image Caption

 

Muhammad bin Abd al-Wahhab, muasisi wa madhehebu ya Uwahabi huko Saudi Arabia anasema kwa uwazi kabisa kwamba: “Iwapo mtu atamuabudu Mwenyezi Mungu usiku na mchana, na kisha kwenda kwenye kaburi la Mtume au walii wa Mwenyezi Mungu na kumuomba (kumtaka amkidhie haja fulani), kwa hakika huwa amejichagulia miungu miwili na hajashuhudia kwamba hakuna mungu ila Mungu Mmoja pekee." Anaamini kwamba Mwislamu wa kweli ni mtu ambaye si tu hafanyi tawasuli kwa mawalii wa Mwenyezi Mungu, bali pia lazima ajibari na kujitenga na watu kama hao na kuwaona kuwa ni makafiri! Anaandika: "Uislamu wa mtu haukubaliki, isipokuwa akiwachukia wale wanaojikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kupitia watu wema na kuwaona kuwa ni makafiri." Muhammad bin Abd al-Wahhab anaona kuwa inajuzu kumwaga damu za watu hawa, na cha ajabu zaidi anadai kwamba madhehebu zote za Kiislamu zinaafikiana juu ya suala hilo, wakati ushahidi uliopo unathibitisha kinyume kabisa cha madai yake hayo yasiyo na msingi.

************

Dakta Muhammad Tahir al-Qadiri, mwanachuoni wa madhehebu ya Hanafi wa Pakistani, anaandika katika kitabu kinachooitwa "Atikadi ya Tawassul" kwamba: "Tawassul ni suala ambalo limethibitishwa na maandiko ya wazi ya Qur'ani Tukufu na hadithi sahihi na nyingi za Uislamu ambapo Waislamu walio wengi wamekuwa wakiitekeleza tangu zama za kale hadi leo.....”

Miongoni mwa wanazuoni wa Kisunni kama Ibn Majah, Haythami, Muttaqi Hindi na wengineo kadhaa wamenukuu Hadithi ambazo wamezitaja kuwa ni sahihi na ambazo haziwezi kufafanuliwa vingine isipokuwa kuamini kujuzishwa kwa tawassul. Kwa mfano, Uthman bin Hanif mmoja wa masahaba wa Mtume Mtukufu (saw), amenukuliwa akisema maneno yenye madhumuni yafuatayo: “Kipofu mmoja alikuja kwa Mtume (SAW) na kumwambia: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Muombe Mwenyezi Mungu anijaalie afya. Mtukufu Mtume (saw) akamjibu: Ukitaka, nitaomba, na ukitaka pia, subiri, na subira kwako ni bora. Akasema: Omba. Mtume akamwambia: Tawadha vizuri na uswali rakaa mbili, na baada ya hapo omba dua hivi: Ewe Mwenyezi Mungu! Ninakuomba kupitia Nabii wako ambaye ni Nabii wa rehema na ninakuelekea Wewe kupitia kwake ili unitimizie haja yangu. Ewe Mwenyezi Mungu! Mfanye kuwa mwombezi wangu." Hassan bin Ali Saqqaf, mmoja wa wanazuoni wa madhehebu ya Shafii kutoka Jordan, anaashiria riwaya hiyo hiyo na kusema: "Kutawassal hakuna maana ya kumwabudu mtu uliyetawassal naye." Kwa maelezo hayo na kinyume na madai ya Mawahabi, madhehebu mengi ya Kiislamu yanaona kwamba kutawasali na kutafuta msaada kutoka kwa Mtume (saw) na Maimamu Maasumina wa Kiislamu (as) ni jambo linaloruhusiwa na linalooana kikamilifu na Tauhidi.

*******************

Kutawasali kuna maana ya kutumia kitu au mtu ili kufikia lengo unalokusudia, na hilo linachukuliwa kuwa njia au chombo tu cha kufikia lengo hilo na wala sio kuchukuliwa kuwa ni jambo au kitu kinachoabudiwa. Kutawasali na Mtume pamoja na Maimamu Maasumina (as) ni kuwatumia kwa ajili ya kupata radhi na kumkurubia Mwenyezi Mungu na wala jambo hilo huwa halitumiwi kama njia ya kuwaabudu watukufu hao. Muumini na Mwislamu anayewaomba waja wema na mawalii wa dini daima huwa anatambua vyema kwamba ni Mwenyezi Mungu pekee ndiye aliye na uwezo wa kujitegemea na mwenye kuathiri kila jambo ulimwenguni bila haja ya msaada wa wengine na kwamba viumbe wengine wote wana uwezo wa kuathiri mambo kwa msaaad na kwa kumtegemea Yeye. Kwa imani hiyo, kutawasali na Mitume na Maimamu watoharifu kamwe hakuwezi kuchukuliwa kuwa ni kutoka kwenye misingi ya dini au kwamba ni kukana upweke wa Mwenyezi Mungu, na wala mtu anayetekeleza jambo hilo hawezi kutuhumiwa kuwa ni mshirikina au kafiri.

Kimsingi dunia tunamoishi ni dunia ya kutawasali na kufikia malengo yetu kupitia mambo tofauti. Hata kama tutamwomba Mwenyezi Mungu moja kwa moja na bila kutawasali na yeyote ili atukidhie haja zetu bila shaka Mwenyezi Mungu atatujibu maombi hayo, kututimizia haja zetu na kututeremshia neema zake kupitia mambo na sababu tofauti. Kwa mfano tukimuomba atuteremshie mvua, bila shaka atatuteremshia mvua hiyo kupitia mawingu. Bila shaka kutumika mawingu kama wasila na njia ya mvua kutufikia sisi wanadamu hakuna maana kwamba huko ni kukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu na uendeshaji wake wa ulimwengu. Mwewnyezi Mungu ambaye ndiye muumba wa ulimwengu na vyote vilivyomo, bila shaka ndiye anayefanya na kusimamia mabadiliko yote yanayotokea humo na ana njia zake mwenyewe ambazo huzitumia kuwafikishia waja wake mahitaji na rehema zake. Kwa msingi huo Mwenyezi Mungu ameainisha njia na wasila zake ambazo ameziweka mbele ya wanadamu na kuwaruhusu wazitumie ili kuweza kumfikia kirahisi, kukidhiwa haja zao na maombi yao kuweza kujibiwa kwa haraka. Katika Qur'ani Tukufu Mwenyezi Mungu ameashiria wazi baadhi ya mambo tunayotakiwa kuyatumia kama wasila na njia ya kuimarisha imani zetu. Anasema katika Aya ya 35 ya Surat al-Maida:

Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu na tafuteni njia ya kumfikilia, mfanye juhudi katika njia Yake ili mpate kufaulu.

Katika Aya hii, neno 'wasila' kwa maana ya njia limetumika bila kuwekwa sharti lolote hivyo kila jambo linalokubalika na kumridhisha Mwenyezi Mungu, linaweza kutumika kwa ajili ya kumkurubia. Jambo hilo huenda likawa ni amali kama vile swala, saumu, hija au Jihadi, au vitu kama al-Kaaba, Jiwe Jeusi, Maqaam Ibrahim na Qur'ani au aina ya watu kama Manabii na Mawalii. Kwa maelezo hayo kila jambo linalotukurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kutufanya tuwe karibu Naye zaidi na kumkumbuka linaweza kuhesabika kama wasila na njia ya kuelekea kwa Mwenyezi Mungu.

Image Caption

***************

Hoja nyingine katika Qur'ani Tukufu inayothibitisha ruhusa ya kutawasali na Mitume na Maimamu (as) katika kukidhiwa haja na Mwenyezi Mungu ni Aya ya 103 ya Surat Aal Imran inayosema: Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane.

Je, umeshawahi kujiuliza swali hili kwamba nini maana ya neno 'Habl Allah' linalotarjumiwa kwenye Aya hii kwa maana ya Kamba ya Mwenyezi Mungu? Bila shaka hili si mojawapo ya majina ya Mwenyezi Mungu na kwa hivyo kuna kitu kingine kinachokusudiwa hapa mbali na Mwenyezi Mungu na ambacho kinapaswa kuchukuliwa kuwa kiunganishi kati ya wanadamu na Muumba wao. Katika Riwaya, Habl Allah imefafanuliwa kuwa ni Kitabu Kitakatifu cha Mwenyezi Mungu yaani Qur';ani na Maimamu watoharifu. Katika kujibu swali la mtu aliyeuliza maana ya neno Habl Allah, Mtume Mtukufu (saw) alimjibu kivitendo kwa kuuweka mkono wake kwenye bega la Imam Ali (as) na kusema: "Huyu ndiye Kamba ya Mwenyezi Mungu." Katika Hadithi nyingine, anaiarifisha Qur'ani Tukufu na Ahlul Bait (as) kwa pamoja kuwa ndio kusudio la Habl Aallah na kusisitiza kuwa viwili hivyo ndio sababu ya wanadamu na waumini kufanikiwa kufuzu katika maisha yao ya humu duniani na huko Akhera.

Image Caption

Tawassul si bidaa, si haramu wala dhidi ya mafundisho ya dini ya Uislamu, bali ni jambo lililopendekezwa na Mwenyezi Mungu, Mtume na Maimamu wetu watoharifu (as). Ni Mwenyezi Mungu mwenyewe ndiye  aliyetaka Mtume na Maimamu (as) wawe waombezi kati Yake na waja Wake. Jambo hili kamwe halina maana ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu wala kumlinganisha na viumbe wake.

Huenda ukasema kwamba, kwa mtazamo wa Mawahabi, kumuomba Mtume au Imamu ambaye hayuko hai ni bidaa na haramu, kwa sababu wanaamini kwamba wafu hawaathiri chochote duniani, na kama ambavyo kuwaombea dua na kuwasomea Qur'ani hakuna maana kwao, hivyo hivyo kuwaomba jambo hakuna maana na ni bidaa katika dini. Ikiwa utajiunga nasi katika kipindi kijacho, bila shaka utapata kunufaika na jibu la swali hili kwa sababu tutalizungumzia kwa urefu kidogo.

Basi hadi wakati huo, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.