May 24, 2023 14:49 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 906 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 43 ya Az-Zukhruf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 70 hadi 73 za sura hiyo ambazo zinasema:

ادْخُلُوا الْجَنَّةَ أَنتُمْ وَأَزْوَاجُكُمْ تُحْبَرُونَ

Ingieni Peponi, nyinyi na wake zenu; katika hali ya furaha.

يُطَافُ عَلَيْهِم بِصِحَافٍ مِّن ذَهَبٍ وَأَكْوَابٍ ۖ وَفِيهَا مَا تَشْتَهِيهِ الْأَنفُسُ وَتَلَذُّ الْأَعْيُنُ ۖ وَأَنتُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

Watakuwa wanapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe; na vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda na macho yanavifurahia, na nyinyi mtakaa humo milele. 

وَتِلْكَ الْجَنَّةُ الَّتِي أُورِثْتُمُوهَا بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

Na hiyo ni Pepo mliyo rithishwa kwa hayo mliyo kuwa mkiyafanya.

لَكُمْ فِيهَا فَاكِهَةٌ كَثِيرَةٌ مِّنْهَا تَأْكُلُونَ

Mnayo humo matunda mengi mtakayo yala.

Katika aya za mwisho tulizosoma katika darsa iliyopita tulieleza kwamba Allah SWT anawapa bishara waja wake wema kwamba Siku ya Kiyama hawatakuwa na hofu, wala hawatahuzunika. Baada ya maelezo hayo, aya tulizosoma zinasema, wale watu ambao hapa duniani walishirikiana na kushikamana pamoja na wake zao katika njia ya kulinda imani ya dini yao na kuvumilia tabu na matatizo yaliyowakabili, Siku ya Kiyama watakuwa pamoja na wake zao hao katika raha na furaha na wala hawatatenganishwa. Watakuwa kwenye hali ya furaha kubwa, ambayo itadhihirika wazi kwenye sura na nyuso zao. Allah SWT atawafidia waumini huko akhera raha na starehe zote ambazo walizikosa na kujinyima hapa duniani kwa ajili ya kulinda imani zao. Watumishi wa peponi wenye sura za kupendeza watawaandalia na kuwapatia waumini aina kwa aina za vyakula na vinywaji vitamu kabisa vilivyotiwa kwenye vyombo bora na vya kuvutia mno. Na neema hizo za peponi hazimaliziki wala hazina kikomo. Watu wa peponi wataishi katika hali ya raha na utulivu bila ya dukuduku wala wasiwasi wowote na wala hawatachoshwa au kupoteza hamu ya raha na starehe za huko. Kisha aya zinaendelea kuashiria neema nyingine mbili za peponi na kusema: huko peponi, kinapatikana chochote kile kinachotamaniwa na moyo na chenye kuburudisha macho. Ni maelezo yenye kutoa mguso na kuupa moyo msisimko wa kipekee! Na ili kuzituliza nyoyo za watu wa peponi zisije zikapitikiwa na hisia za unyonge, wa kufikiria na kuchelea kwisha na kumalizika neema za huko, aya zinawaambia: nyinyi mtabaki huko milele. Baada ya maelezo hayo, aya zinawahutubu watu wa peponi ya kwamba, neema hizo za peponi mtakazorithishwa nyinyi zitatokana na amali mlizokuwa mkifanya duniani. Hii ni nukta inayoashiria kwamba amali zenu, ndio sababu kuu ya nyinyi kufuzu na kuokoka. Na kwa kumalizia, aya zimezungumzia matunda ya peponi na kueleza kwamba miti yake itakuwa imejaa matunda muda wote; na watu wa peponi wataweza kujiburudisha vyovyote wapendavyo na matunda hayo ya aina kwa aina na yenye ladha na utamu wa kipekee. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, huko akhera pia, wanandoa waumini wataendelea kuwa pamoja katika hali ya mke na mume. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wale ambao hapa duniani na kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu waliyaepusha macho yao kuwatazama wasio maharimu zao na kuangalia mambo machafu yaliyoharamishwa, huko akhera watastarehe na kuburudika kwa kuwaangalia na kusuhubiana nao wake wazuri na warembo wa peponi. Tab’an, raha na starehe hizo haziwezi kufananishwa hata chembe na raha za kupita za hapa duniani. Halikadhalika, aya hizi zinatutaka tujue kwamba, raha na starehe za dunia ni zenye mpaka na hazidumu. Kupata raha zote na kila anachokitamani mtu, tena bila kuwa na kikomo wala kumalizika, kunawezekana huko peponi tu. Wa aidha, aya hizi zinatuelimisha kuwa, pepo haipatikani kwa kutamani, inapatikana kwa kuichuma. Kutamani kuingia peponi bila kufanya amali njema, ni sawa na kutaraji jambo muhali na lisilowezekana. Vilevile aya hizi zinatutaka tujue kwamba, moja ya neema za kuburudisha za peponi ni matunda mengi mno na ya aina kwa aina yatakayopatikana huko.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 74 hadi 76 ambazo zinasema:

إِنَّ الْمُجْرِمِينَ فِي عَذَابِ جَهَنَّمَ خَالِدُونَ

 Kwa hakika wakosefu watakaa milele katika adhabu ya Jahannamu.

لَا يُفَتَّرُ عَنْهُمْ وَهُمْ فِيهِ مُبْلِسُونَ

Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa.

وَمَا ظَلَمْنَاهُمْ وَلَٰكِن كَانُوا هُمُ الظَّالِمِينَ

Wala Sisi hatukuwadhulumu, bali wao ndio walio kuwa madhaalimu.

Baada ya kusimuliwa hali za watu wa peponi zitakavyokuwa Siku ya Kiyama, aya hizi zinaashiria hatima ya waovu na wafanya madhambi siku hiyo, ili baada ya kulinganisha hatima za makundi hayo mawili, mtu achague njia sahihi ya kufuata hapa duniani. Kwanza aya zinasema, kama ambavyo watu wema watabaki peponi milele, watu waovu, nao pia watabaki motoni milele. Pamoja na hayo, kwa kuzingatia aya nyingine na Hadithi, si waovu wote watakaobakia motoni milele. Waovu pekee watakaoselelea humo ni wale ambao mwenendo wao katika maisha unaonyesha kuwa, kama wangeendelea kubaki duniani hata kwa miaka elfu mingine, wasingeacha inadi na upinzani dhidi ya haki na wangeendeleza dhulma na uonevu. Ni wazi kwamba watu wakaidi na waovu kama hao hawastahiki kupata rehma za Mwenyezi Mungu za kuwaokoa au kuwahafifishia adhabu, na hawatapata huko njia yoyote ya kuwaokoa na adhabu. Na kwa hiyo watapatwa na majuto na majonzi makubwa. Na ili isije ikadhaniwa kwa namna yoyote ile kwamba Mwenyezi Mungu labda amewadhulumu watu hao kwa kuwapa umri wenye kikomo wa duniani, lakini akawaandalia adhabu ya milele ya akhera, aya zinatanabahisha kwa kueleza kwamba, hatima hiyo iliyowafika walijiandalia wao wenyewe. Sababu ya kufikwa na adhabu hiyo ya milele ni amali za dhulma zilizotangulizwa na mikono yao wenyewe. Katika ulimwengu wa leo pia, kwa mtazamo wa taaluma ya sheria, kuna mlingano na uwiyano baina ya athari za kosa na adhabu yake; na si lazima mlingano huo uendane na muda aliotumia mtu kutenda kosa. Na ndio maana baadhi ya makosa, hata kama mtu atakuwa amefanya katika muda mfupi kabisa, lakini adhabu yake inaweza ikawa ya kifungo cha muda mrefu au hata cha maisha. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, katika misingi ya mafunzo na malezi ya Qur'ani, maonyo na bishara zinakwenda sambamba, ili mtu asije akaingiwa na ghururi zisizo na maana wala hali ya kukata tamaa moja kwa moja. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kama ambavyo amali njema ni sababu itakayomfanya mtu aingie peponi; sababu ya kuingia motoni pia itakuwa ni matendo maovu aliyofanya mtu mwenyewe. Aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, Mwenyezi Mungu hamdhulumu mtu yeyote, lakini atamwadhibu kila dhalimu mfanya maovu.

Tunahitimisha darsa yetu kwa aya ya 77 na 78 za sura yetu ya Az-Zukhruf ambazo zinasema:

‏ وَنَادَوْا يَا مَالِكُ لِيَقْضِ عَلَيْنَا رَبُّكَ ۖ قَالَ إِنَّكُم مَّاكِثُونَ

 Nao watapiga kelele waseme: Ewe Malik! Na atufishe Mola wako Mlezi! Atasema: Hakika nyinyi mtakaa humo humo!

لَقَدْ جِئْنَاكُم بِالْحَقِّ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَكُمْ لِلْحَقِّ كَارِهُونَ ﴿٧٨﴾‏ أَمْ أَبْرَمُوا أَمْرًا فَإِنَّا مُبْرِمُونَ

Kwa yakini tulikuleteeni Haki, lakini wengi katika nyinyi mlikuwa mnaichukia Haki.

Hali za waovu na madhalimu motoni zitakuwa nzito na mbaya na zisizoweza kuhimilika na kuvumilika, kiasi kwamba hawataona njia nyingine ya faraja kwao isipokuwa kuomba mauti; na kwa hivyo watamtaka Malaika wa Motoni awaombee hilo kwa Mwenyezi Mungu ili waweze kuondokana na hali hiyo ya adhabu isiyostahamilika. Hata hivyo jawabu watakayopewa ni kwamba, hilo mnalotamani, haliwezekani; na nyinyi ni wa kuendelea kubaki tu humu milele. Kama hapa duniani mtu anaweza kukatisha maisha yake kwa kujiua, hilo halitawezekana huko akhera. Kwani hata adhabu kali na ya kutisha, ya kuhiliki na kuteketea ndani ya moto wa Jahannam haitawafanya watu wa motoni wapumue kwa kufikwa na mauti. Kisha aya zinakutaja kuipa mgongo na kuipiga vita haki, kuwa ndio sababu muhimu ya waovu kuingizwa motoni na kueleza kwamba, walipokuwa duniani, watu hao hawakuyapenda maneno ya haki, bali waliamua kufuata hawaa, matashi na matamanio ya nafsi zao na ya wenye fikra kama zao. Na si tu walikuwa hawaikubali haki, lakini hawakuwa tayari hata kuusikiliza na kuutafakri wito wake. Hivyo hatima ya kuipiga vita kwao haki imekuwa ni kufikwa na adhabu ya milele. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tujichunge na mienendo na matendo yetu hapa duniani, ili tusije tukalazimika kutamani mauti huko akhera, tamanio ambalo katu halitaweza kuthibiti. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, adhabu ya Mwenyezi Mungu inatolewa baada ya mtu kutimiziwa dhima ya kufikiwa na wito wa haki. Kwa hivyo atakayekuwa mtu wa motoni ni yule ambaye haki aliifahamu, lakini aliamua kukabiliana nayo na kuipiga vita. Vilevile aya hizi zinatuelimsha kwamba, kuikubali haki na kujisalimisha mbele ya haki ndiko kunakomletea mtu saada na fanaka ya duniani na akhera; kama ambavyo kuipiga vita haki hupelekea mtu kuharibikiwa na kuhasirika duniani na akhera. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 906 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/