May 24, 2023 15:27 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 907 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 43 ya Az-Zukhruf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 79 na 80 za sura hiyo ambazo zinasema:

أَمْ أَبْرَمُوا أَمْرًا فَإِنَّا مُبْرِمُونَ

Au wameweza kukata shauri? Bali ni Sisi ndio tunao pitisha.

أَمْ يَحْسَبُونَ أَنَّا لَا نَسْمَعُ سِرَّهُمْ وَنَجْوَاهُم ۚ بَلَىٰ وَرُسُلُنَا لَدَيْهِمْ يَكْتُبُونَ

Au wanadhani kwamba hatusikii siri zao na minong'ono yao? Wapi! Na wajumbe wetu wapo karibu nao, wanayaandika.

Katika sehemu ya mwisho ya darsa iliyopita walizungumziwa makafiri na washirikina, ambao waliichukia haki na hawakuwa tayari kuikubali na kuifuata. Aya hizi tulizosoma zinasema, wao hawakuichukia tu haki na kujiweka mbali nayo, lakini walisimama pia kuipinga na kuipiga vita. Walipanga mipango mbalimbali kwa lengo la kuidhoofisha haki na kuizima nuru yake na wakafanya kila aina ya njama kufikia lengo lao hilo. Wao walidhamiria kwa dhati kuishinda na kuiangamiza haki. Lakini hawakutambua kwamba wanayekabiliana naye ni Allah SWT, na kwamba irada ya Mola iko juu ya irada na matakwa yao; na si kama wanavyodhani, kwamba lolote wanalodhamiria na wanalotaka, litakuwa tu. Wapinzani hao waliokula njama dhidi ya haki walikuwa wakidhani kwamba, Allah SWT hana habari za vikao na mazungumzo yao ya siri; yaani hawaoni wao wala hayasikii wayasemayo! Ilhali Yeye Mola alikuwa akiyasikia yale waliyokuwa wakiambizana kwa sauti ya chini au hata kunong'onezana masikioni kwenye vikao hivyo vya faragha. Sababu ni kuwa, ya siri na ya dhahiri ni mamoja tu na yana hali sawa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Isitoshe, malaika wa Mwenyezi Mungu pia wako kila mahali, na muda wote wanashughulika kuyanakili na kuyahifadhi yote yasemwayo na yatendwayo na watu hata kwenye faragha na kwa minong'ono, na hakuna chochote kinachofichikana kwao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, uamuzi wowote utakaopitishwa na watu, hata waukamie kwa namna na uzito wowote ule, hauwezi kukiuka irada ya Allah SWT na hautaweza kutekelezeka bila ya idhini yake Yeye Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wapinzani wa haki wasidhani kwamba Mwenyezi Mungu hana habari ya mambo wayafanyayo kwa siri; kwa sababu chochote akifanyacho mtu kinasajiliwa na kuhifadhiwa kwenye daftari la amali zake na hakuna chochote kinachofichika kwa malaika, ambao ni watumishi maalumu wa Mwenyezi Mungu wa kusajili na kuhifadhi amali za waja.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 81 na 82 ambazo zinasema:

قُلْ إِن كَانَ لِلرَّحْمَٰنِ وَلَدٌ فَأَنَا أَوَّلُ الْعَابِدِينَ

Sema: Ingeli kuwa Mwingi wa rehema ana mwana, basi mimi ningeli kuwa wa kwanza kumuabudu.

سُبْحَانَ رَبِّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبِّ الْعَرْشِ عَمَّا يَصِفُونَ

Ametakasika Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, Mola Mlezi wa A'rshi, na hayo wanayo msifia.

Katika aya za awali za sura hii ya Az-Zukhruf iliashiriwa itikadi ya washirikina ya kuwachukulia malaika kuwa ni mabanati wa Mwenyezi Mungu; kisha katika aya za baada yake ikazungumziwa pia imani ya Wakristo ya kumuitakidi Nabii Isa Masih (as) kuwa ni mwana wa Mungu. Aya hizi zinazipinga imani na itikadi hizo potofu na batili na kueleza kwamba, kama Mwenyezi Mungu angekuwa na mwana, ambaye angepasa kuabudiwa, basi Mitume wangekuwa watu wa mwanzo kumwabudu mwana huyo. Lakini mosi ni kwamba, Mwenyezi Mungu ametakasika na kuwa na mke na mwana; na pili, Yeye Mola hajaamrisha kuabudiwa yeyote katika viumbe wake, wawe ni malaika au watu. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba, Mungu aliye mmiliki na mwendeshaji wa mbingu na ardhi na Mola wa Arshi adhimu na yenye adhama, hahitaji kuwa na mwana. Yeye ni mwepo asiye na ukomo wala mwisho na ameuzunguka na kuuhodhi ulimwengu wote. Ilivyo hasa ni kwamba, mtoto huwa ana ulazima kwa mtu kwa ajili ya kuendeleza kizazi chake, au mtu anapozeeka na akawa hajiwezi tena, huhitaji msaada na usaidizi wa watoto wake. Nukta nyingine ni kuwa, maana ya kuwepo kwa mwana, ni mzazi wake kuwa na kiwiliwili na kuwepo na kuishi kwenye zama fulani na mahala maalumu. Hali ya kuwa Mungu aliyeuumba ulimwengu na akauendesha pamoja na vyote vilivyomo ndani yake ametakasika na yote hayo na si mhitaji wa chochote wala yeyote, akiwemo mwana. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, inapasa kuwa na uchukulivu katika kujadiliana na wapinzani na kuwafahamisha kwa hekima kwamba, kama tutajaalia kuwa mtazamo walio nao wao ni sahihi, nini yatakuwa matokeo yake, ili waweze kubaini wao wenyewe upotofu wa imani yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, hapana shaka Mwenyezi Mungu Mtukufu ametakasika na kila kasoro, uhitaji au kuwa na mshabaha na mwanadamu. Kwa hivyo inatupasa kila wakati tujitenge na kujiweka mbali na miungu wa jinsia za watu, kwa sababu miungu wa aina hiyo ni matokeo ya udhanifu wa mwanadamu na ujinga wake wa kutozifahamu sifa za Mwenyezi Mungu, ambaye hakuna wa pili baada ya Yeye, wala yeyote anayefanana naye kwa chochote. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, pamoja na adhama kubwa zilizonazo, mbingu na ardhi zinaendeshwa kwa tadbiri ya Allah SWT na kwa hali moja na wakati mmoja.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 83 na 84 ambazo zinasema:

فَذَرْهُمْ يَخُوضُوا وَيَلْعَبُوا حَتَّىٰ يُلَاقُوا يَوْمَهُمُ الَّذِي يُوعَدُونَ

Basi waache wapige porojo wakicheza mpaka wakutwe na hiyo siku yao wanayo ahidiwa. 

وَهُوَ الَّذِي فِي السَّمَاءِ إِلَٰهٌ وَفِي الْأَرْضِ إِلَٰهٌ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْعَلِيمُ

Na Yeye ndiye Mungu mbinguni, na ndiye Mungu katika ardhi. Naye ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi.

Mitume ni watu waliotumwa kuja kuwaelekeza watu kufuata uongofu. Waja hao wateule waliifanya kazi hiyo kwa uwezo wao wote; na kutokana na namna walivyokuwa wakiwahurumia na kuwaonea uchungu watu wao, walitumia njia mbalimbali ili kuwaokoa na dhalala na upotofu. Aya tulizosoma zinasema: pamoja na hayo, huko kuwatakia kheri na kuwaonea uchungu watu, ilibidi kuwe na kipimo na mpaka, kwa sababu wakati watu wenyewe wanapokuwa hawataki kuifuata njia ya haki na kuifikia saada na fanaka, haiwezekani kuwalazimisha na kuwateza nguvu; bali inabidi waachiwe wenyewe ili wajionee matokeo ya kuchagua kwao njia isiyo sahihi na kujitumbukiza kwenye lindi la upotofu na batili. Labda kwa kufanya hivyo watabaini kosa lao na kurudi kwenye njia ya haki. Lakini yamkini pia wakaamua wasirudi, wakabaki kwenye njia ya upotofu mpaka mwisho wa maisha yao na hatimaye wakaenda kufufuliwa Siku ya Kiyama wakiwa katika hali hiyo; na hapo ndipo watakapochuma matunda machungu ya fikra na amali zao chafu na ovu. Kisha aya zinabainisha kuwa, Mwenyezi Mungu si mhitaji wa kuamini na kusilimu watu na kusisitiza kwamba, makafiri wasidhani kuwa Allah SWT ni mhitaji wa ibada zao na wala wasifikirie kama kukufuru na kuasi kwao kutaudhuru kwa namna yoyote ile Uola wake; kwa sababu Yeye ni Mungu wa mbingu na Mungu wa ardhi na Mwabudiwa wa viumbe vyote. Kwa maneno mengine ni kwamba, mwabudiwa halisi na wa kweli ni yule aliye msimamiaji na mwendeshaji wa ulimwengu. Kwa hivyo si yeyote wala si chochote kati ya malaika, masanamu na vitu vya maumbile kama jua, mwezi na nyota kinachostahiki kuabudiwa. Vyote hivyo ni viumbe na mahuluku wa Mwenyezi Mungu; na uwepo wao unamtegemea Yeye Mola. Sehemu ya mwisho ya aya hizi inaeleza kwamba, Allah SWT ana habari za mambo yote; na anauendesha ulimwengu kwa ujuzi wake usio na mpaka na hekima yake isiyo na ukomo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Mitume walipewa jukumu la kuwalingania na kuwaonyesha watu mwongozo wa haki, si kuwalazimisha na kuwateza nguvu, wala kuwabembeleza na kuwatafadhalisha. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, katika masuala ya itikadi na baada ya kuwabainishia watu burhani na kuwawekea wazi hoja zote kwa ukamilifu, haitakiwi tena kuwabana na kuwashinikiza, bali tuwaache wenyewe wachague kwa uhuru njia wanayotaka kufuata. Halikadhalika, tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Mwenyezi Mungu si mhitaji kwa mtu yeyote yule, sembuse ahitajie t'aa na ibada zao watu. Yeye alikuwa Mungu wakati sisi sote tulipokuwa hatupo; na atakuwa Mungu pia wakati sote tutakapokuwa tumeondoka hapa duniani. Yeye ni Mungu wa mbingu na ardhi na viumbe vyote vya ulimwengu. Vilevile aya hizi zinatutaka tujue kuwa, anayestahiki na kufaa kuabudiwa ni yule mwenye ujuzi usio na mpaka na hekima isiyo na ukomo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 907 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah, atuepushe na kila aina ya shirki, kubwa na ndogo, ya dhahiri na iliyojificha na atuwafikishe kuifahamu haki na kuifuata hadi mwisho wa uhai wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/