Sura ya Az-Zukhruf, aya ya 85-89 (Darsa ya 908)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 908 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 43 ya Az-Zukhruf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 85 ya sura hiyo ambayo inasema:
وَتَبَارَكَ الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا وَعِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ
Na ametukuka Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo ndani yake. Na uko kwake ujuzi wa Saa ya Kiyama, na kwake Yeye mtarudishwa.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia Uola wa Allah SWT, ambaye katika ulimwengu huu, hakuna mtu au kitu chochote kinachostahiki kuabudiwa ghairi yake Yeye. Mwabudiwa halisi wa malaika mbinguni na wanadamu ardhini ni Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu peke yake. Baada ya maelezo hayo, aya hii tuliyosoma inasema: sababu ya kumtii na kumwabudu Allah SWT ni kwamba ulimwengu wote uko kwenye mamlaka yake. Anaziendesha mbingu na ardhi na vilivyomo baina ya viwili hivyo; na hakuna yeyote ghairi yake Yeye aliye na mamlaka ya utawala na uendeshaji wa ulimwengu huu. Yeye ni Muumba wa vitu vyote pamoja na sharia na kanuni zinazotawala vitu hivyo. Na si hii dunia tu, bali mamlaka ya Siku ya Kiyama pia yako mikononi mwake. Ni Yeye pekee ndiye ajuaye wakati wa kujiri Kiyama. Baada ya kufa, nyote mtarejea kwake na Yeye ndiye atakayekuhukumuni. Basi kama mtu anaitaka saada na kufuzu duniani na akhera aishike na kuifuata njia aliyoiainisha Yeye Allah, afanye yale yanayomridhisha Yeye Muumba wake na ajiepushe na kujiweka mbali na yale yanayopelekea kupatwa na adhabu na ghadhabu zake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, asili ya dunia yetu na marejeo ya akhera yetu sisi wanadamu yako kwa Mwenyezi Mungu, Mola pekee wa haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, hakuna yeyote mwenye ujuzi wa lini utakuwa mwisho wa dunia na wakati gani kitasimama Kiyama isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake.
Ifuatayo sasa ni aya ya 86 ya sura yetu ya Az-Zukhruf ambayo inasema:
وَلَا يَمْلِكُ الَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِهِ الشَّفَاعَةَ إِلَّا مَن شَهِدَ بِالْحَقِّ وَهُمْ يَعْلَمُونَ
Wala hao wanao waomba badala yake Yeye hawana uweza wa uombezi, isipo kuwa anaye shuhudia kwa haki, na wao wanajua.
Moja ya mambo yanayochochea shirki ni kutokea baadhi ya watu wanaodhani kwamba vitu au watu fulani wanao uwezo wa kuwaombea na kuwashufaia kwa Mwenyezi Mungu na kuwafanya wapate rehma za Mola. Ni kwa sababu hiyo ndipo huamua kuvielekea na kuviomba msaada vitu na watu hao. Aya hii tuliyosoma inasema, uombezi utakuwepo katika mahakama ya Mwenyezi Mungu, lakini hautafanywa na wale mnaowadhania nyinyi. Hao hawana uwezo wa kuombea kwa namna yoyote ile. Uombezi kwa Mwenyezi Mungu utafanywa kwa idhini yake Yeye tu Mola. Kwa hakika haki ya kushufaia watakuwa nayo watu ambao maneno na matendo yao yanaendana na haki; na wao ni ruwaza na kigezo bora cha kuigwa na kufuatwa na wafuasi wa njia ya haki. Watu walioikubali tauhidi na Upekee wa Mwenyezi Mungu wanajisalimisha na kuitii haki kwa ukamilifu wake; na hawafuati njia nyingine isipokuwa aliyoiainisha Allah SWT kwa ajili ya saada na fanaka ya waja wake. Watu hao wanayafahamu masharti ya wanaoshufaia na wanajua ni watu gani watapewa idhini ya kuwaombea. Wao watawaombea kwa idhini ya Allah SWT watu watakaostahiki kushufaiwa na kuwa sababu ya kurehemewa na Mola. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kama ilivyo toba ambayo ni njia ya kurudi kwa Mwenyezi Mungu na kupokewa na Yeye Mola, shufaa ni njia ya kurudi kwake Yeye pia, lakini ni kwa kupitia mawalii wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, watu wanaofuata njia ya haki wanatakiwa wawashike mkono na wenzao pia ili waongozane nao katika njia hiyo; na hiyo ndio shufaa na uombezi halisi.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 87 ambayo inasema:
وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَهُمْ لَيَقُولُنَّ اللَّهُ ۖ فَأَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ
Na ukiwauliza ni nani aliye waumba? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu! Basi ni wapi wanako geuziwa?
Baada ya aya iliyotangulia kuzungumzia mwenendo wa washirikina wa kutaka wapatiwe shufaa na uombezi na asiyekuwa Mwenyezi Mungu, aya hii inawakemea na kuwahoji watu hao kwa kuwauliza: Nyinyi, ambao mnakubali kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wenu na Muumba wa ulimwengu pia, kwa nini mnaomba msaada kwa wasiokuwa Yeye na hata kwa namna fulani kuwaabudu pia? Ilhali, kuabudiwa kunamstahikia yule tu aliyeuumba na anayeuendesha huu ulimwengu. Ni upotofu wa aina gani huo uliokupateni? Vipi mnavinyenyekea vitu au watu ambao hawana hadhi yoyote; na mnamwacha Mwenyezi Mungu na kuwaendea huku mkiwatarajia wawe wasita na kiunganishi cha kupatia uombezi mbele yake Yeye Mola? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, hata washirikina, wanaikubali sifa ya Mwenyezi Mungu ya uumbaji. Tatizo kuu ni katika kuwa kwake Mola Mlezi na Mwendeshaji wa masuala ya wanadamu, ambapo washirikina huyanasibisha hayo na vitu visivyo na uhai au huamini kwamba kuna na wengine wanaochangia pia katika hayo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, upotofu wa aina yoyote katika tauhidi ya Uola na Ulezi wa Allah SWT kwa waja wake ni kupotoka mtu katika fitra na maumbile ya ubinadamu wake.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 88 na 89 ambazo ndizo aya za mwisho za Suratu-Zukhruf zisemazo:
وَقِيلِهِ يَا رَبِّ إِنَّ هَٰؤُلَاءِ قَوْمٌ لَّا يُؤْمِنُونَ
Na usemi wake (Mtume) ni: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hawa ni watu wasio amini.
فَاصْفَحْ عَنْهُمْ وَقُلْ سَلَامٌ ۚ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ
Basi waache, na uwambie maneno ya salama. Watakuja jua.
Aya hizi, ambazo kama tulivyotangulia kueleza, ndizo aya za mwisho za Suratu-Zukhruf zinahitimisha maudhui ya tauhidi na shirki kwa kueleza kwamba, licha ya jitihada za kutwa kucha, na usiku na mchana anazofanya Bwana Mtume Muhammad SAW na mazungumzo yake na washirikina ya kuwaelekeza kwenye uongofu, lakini baadhi yao hawasilimu na wala hawana nia ya kufanya hivyo. Japokuwa haki wameifahamu, lakini mawaidha na maneno wadhiha, ya kweli na ya haki ya Mtume wa Allah hayaziathiri kivyovyote vile nyoyo zao yabisi; na wao hawako tayari kuyakubali maneno hayo kwa sababu yanapingana na maslahi yao ya kidunia na raha na starehe zake za kupita. Na kwa sababu hiyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu anamwambia Mtume wake: baada ya wewe kutimiza dhima yako kwao na kuwafikishia wito wa haki, jitenge nao na waache kama walivyo na mambo yao, ili isije ikawapitikia kudhani kwamba wewe ni mhitaji wa kusilimu kwao au unataka kuwasilimisha kwa nguvu. Agana nao na waachie wafuate njia yoyote waitakayo. Lakini baada ya yote hayo, aya tulizosoma zinawapa indhari kali na yenye maana nzito ili wasije wakahisi Allah SWT hatowafanya chochote; na kwa hivyo inawaambia: karibuni hivi watajua na kutambua nini utakuwa mwisho wao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, viongozi na wafanya tablighi ya dini wasiwe na matarajio kuwa watu wote wataamini na kuikubali haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, baada ya kutimiza dhima ya kuwabainishia haki ipasavyo wapinzani, tusiwabembeleze na kuwatafadhalisha, wala tusiwateze nguvu na kuwalazimisha. Tuwaache kama walivyo wachague kwa hiari yao kufuata wanachotaka. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 908 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azilainishe nyoyo zetu, tuwe tayari kuikubali na kuifuata haki pale inapotuthibitikia na tuwe wepesi kuiacha na kuiepuka batili pale inapotubainikia. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/