May 24, 2023 16:02 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 911 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 44 ya ad-Dukhan. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 19 hadi ya 21 za sura hiyo ambazo zinasema:

وَأَن لَّا تَعْلُوا عَلَى اللَّهِ ۖ إِنِّي آتِيكُم بِسُلْطَانٍ مُّبِينٍ

Na msijitukuze kwa Mwenyezi Mungu; hakika mimi nitakuleteeni uthibitisho ulio wazi.

وَإِنِّي عُذْتُ بِرَبِّي وَرَبِّكُمْ أَن تَرْجُمُونِ

Nami najikinga kwa Mola wangu Mlezi na ndiye Mola wenu Mlezi pia, ili msinipige mawe. 

وَإِن لَّمْ تُؤْمِنُوا لِي فَاعْتَزِلُونِ

Na ikiwa hamniamini, basi jitengeni nami.

Katika darsa iliyopita tulisema, Nabii Musa (as) alitakiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu amwendee Firauni na kumtaka awaachie huru na kuwatoa utumwani watu wake wa kaumu yake ya Bani Israil. Aya tulizosoma zinaendelea kunukuu maneno ya Mtume huyo wa Allah aliposema: Enyi kina Firauni! Mimi nimekuleteeni hoja za wazi na zenye ushahidi na kukuonyesheni pia miujiza kadhaa. Basi jisalimisheni kwa amri za Mwenyezi Mungu na wala msitakabari na kumwasi Yeye Mola. Enyi kina Firauni! Msidhani kama mkinitishia kuniua, nitaiacha njia niliyoichagua. Mimi nimetumwa na Mwenyezi Mungu; ninaomba hifadhi kwake Yeye aniepushe na njama zenu; na kama atataka, atanilinda na shari yenu. Sasa kama nyinyi hamtaki kuniamini na kujisalimisha kwa amri za Mwenyezi Mungu, basi niacheni kama nilivyo, wala msituzuilie mimi na wafuasi wangu kufanya tunayoyataka. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kutakabari na kujikweza mbele ya wanadamu wenzako ni jambo ovu; na uovu mkubwa na mbaya zaidi ni kumfanyia hayo Mwenyezi Mungu ambaye ni Muumba na Mmiliki wa wanadamu wote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wito wa Mitume una mantiki na hoja za wazi ambazo watu wote wanaweza kuzifahamu. Kwa hivyo kukataliwa na wapinzani, hutokana na hulka ya kiburi na ubinafsi waliyonayo wapinzani wenyewe, si kwa sababu ya kutoyaelewa mafundisho hayo ya wajumbe wa Allah. Halikadhalika aya hizi zinatufunza kuwa, mashinikizo, mateso na vitisho vya maadui visitudhoofishe na kutufanya turudi nyuma katika njia ya kulingania wito wa haki. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, baadhi ya wakati na kwa ajili ya kufanikisha malengo ya dini, badala ya kukabiliana na kuvutana na waistikbari, tunatakiwa tujiweke mbali nao ili tuweze kuandaa mazingira ya kufikia malengo yetu hayo.

Tunaendelea na darsa yetu kwa aya ya 22 hadi 24 ambazo zinasema:

‏ فَدَعَا رَبَّهُ أَنَّ هَٰؤُلَاءِ قَوْمٌ مُّجْرِمُونَ

Ndipo akamwomba Mola wake Mlezi, kwamba hawa ni watu waovu.

فَأَسْرِ بِعِبَادِي لَيْلًا إِنَّكُم مُّتَّبَعُونَ

(Mwenyezi Mungu akamwambia): Basi nenda pamoja na waja wangu usiku. Kwa yakini mtafuatwa.

وَاتْرُكِ الْبَحْرَ رَهْوًا ۖ إِنَّهُمْ جُندٌ مُّغْرَقُونَ

Na iache bahari (vivyo hivyo) imetulia, hakika wao ni jeshi litakalo zamishwa.

Baada ya Nabii Musa (as) kutumia kila njia na mbinu ili kuwaonyesha uongofu na kuwapa maonyo Firauni na watu wake bila ya kupata tija yoyote, alimwomba Mwenyezi Mungu awape adhabu watu hao waovu na mafasiki, kwa namna atakavyoona Yeye Mola inafaa. Allah SWT akamwamuru Mtume wake huyo awaweke tayari wakati usiku watu wake wa kaumu ya Bani Israil waliokuwa wakinyongeshwa na Mafirauni, kwa ajili ya kuhama Misri na kuelekea Palestina. Na bila shaka ilitarajiwa pia kwamba Firauni na watu wake wangeamua kuwafuata kwa lengo la kuwadhuru. Lakini Allah SWT akawaahidi kuwa atawafungulia njia na wataweza kupita na kuvuka salama usalimini katika Mto Nile uliokuwa umejaa maji yenye mawimbi makubwa. Kwa hivyo wasiwe na wasiwasi, kwa sababu wakati jeshi la Firauni litakapoingia ndani ya mto huo, litagharikishwa lote kwa amri yake Mola na wala halitaweza kumfikia Nabii Musa (as) na watu wake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, moja ya sababu zinazoyafanya maneno ya Mitume yasiwe na taathira kwa watu na wasiwe tayari kuyakubali maneno hayo, ni watu wenyewe kuwa na nafsi zilizochafuka kwa madhambi na maovu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, bila ya sisi wenyewe kufanya jitihada pia, dua tupu haitoshi na wala haiwi na taathira. Inatupasa tutekeleze wajibu tulionao, sambamba na kumwomba Mola atusaidie kupata natija tuliyokusudia kwa kutufanyia wepesi na urahisi kwenye kila zito na gumu. Wa aidha aya hizi zinatuonyesha kwamba, anapotaka Mwenyezi Mungu, mto mkubwa wa Nile unaweza kuwa njia ya salama na amani kwa Musa na wafuasi wake, lakini ukageuka kuwa shimo la gharika na maangamizi kwa jeshi kubwa na lililojizatiti kwa silaha la Firauni.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 25 hadi 27 za sura yetu ya ad-Dukhan ambazo zinasema:

كَمْ تَرَكُوا مِن جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ

Mabustani mangapi, na chemchem ngapi waliziacha!

وَزُرُوعٍ وَمَقَامٍ كَرِيمٍ

Na mimea na vyeo vitukufu! 

وَنَعْمَةٍ كَانُوا فِيهَا فَاكِهِينَ

Na neema walizo kuwa wakijistareheshea!

Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kuhusu kuzamishwa na kuangamizwa Firauni na jeshi lake katika Mto Nile na kueleza kwamba, Firauni, ambaye alijidai kuwa na sifa ya uungu na akawa hayuko tayari kuukubali wito wa Nabii Musa (as) aliipoteza dunia yake yote na kila kilichokuwa kwenye mamlaka yake; na vyote hivyo vikaingia mikononi mwa Bani Israil. Ni ajabu isiyo na mfano kwa watu ambao hadi muda mchache tu nyuma walikuwa watumwa na wanyonge wanaotumikishwa, sasa wakawa warithi wa utawala wote wa Firauni na watu wake pamoja na makasri, mabustani, mali na utajiri wao wote. Na si makasri, konde na bustani zao tu, lakini vitu vyote vya thamani walivyokuwa wamejiandalia na kutumia Mafirauni kwa ajili ya kuishi maisha ya raha na starehe, viliishia kuwa milki za Bani Israil. Na yeye Firauni na watu wake wakagharikishwa katika Mto Nile; na miili yao ikaishia kuelea na kusukumwa huku na kule na maji ya mto huo. Yote hayo yalitokana na baraka za muujiza wa Mwenyezi Mungu, baada ya Nabii Musa (as) kupiga fimbo yake kwenye maji ya Mto Nile, ambapo maji yalitulia tuli, kisha ikafunguka ndani yake njia ya kupita Bani Israil. Wafuasi hao wa Mtume wa Mwenyezi Mungu waliweza kuvuka salama usalimini, lakini wakati Firauni na jeshi lake walipojaribu nao pia kufanya hivyo, mawimbi makubwa ya maji ya Mto Nile yaliyokuwa yametulia yalitibuka upya, yakawafunika na kuwazamisha wote. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, irada na alitakalo Allah SWT viko juu ya irada nyingine yoyote ile. Kwa irada ya Mwenyezi Mungu, jeshi la Firauni lililokuwa limejizatiti kwa wapanda farasi waliosheheni silaha halikuweza kuwazingira na kuwadhuru Bani Israil waliokuwa wakikimbia kwa miguu bila msaada wa kipando chochote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, suhula na nyenzo za kimaada hazitoi hakikisho la kumuokoa mtu na kumdhaminia amani na usalama. Hakuna kasri wala ngome yoyote ionekanayo imara na madhubuti, yenye uwezo wa kuhimili ghadhabu na rada ya Mwenyezi Mungu SWT. Halidhalika, aya hizi zinatuelimisha kwamba, neema za kidunia zinaweza kwisha na kutoweka wakati wowote ule. Neema ngapi ngapi za mali na utajiri, wamiliki wake wameondoka na kuziacha kama zilivyo! Wa aidha aya hizi zinatutaka tujue kuwa, nguvu za mamlaka na za mali na utajiri si wenzo wa kumuokoa mtu wala kumfanya apate saada na fanaka. Bali si hasha vikawa ndio sababu ya hilaki na maangamizi yake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 911 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, ainusuru dini yetu na atulinde na shari za maadui zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/