Sura ya Muhammad, aya ya 21-24 (Darsa ya 932)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 932 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 47 ya Muhammad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 21 ya sura hiyo ambayo inasema:
طَاعَةٌ وَقَوْلٌ مَّعْرُوفٌ ۚ فَإِذَا عَزَمَ الْأَمْرُ فَلَوْ صَدَقُوا اللَّهَ لَكَانَ خَيْرًا لَّهُمْ
Ut'iifu na kauli njema (ni bora kwao). Na amri (ya Jihadi) ikisha azimiwa, basi wakiwa wakweli kwa Mwenyezi Mungu (kuhusu kupigana Jihadi), bila ya shaka itakuwa bora kwao.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya iliyowazungumzia watu wenye imani dhaifu na wanafiki, ambao walikuwa wakiomba kwa ndimi zao iteremshwe sura ya kuwapa ruhusa ya kupigana Jihadi, lakini wakati Allah SWT alipoteremsha aya za kuamrisha Jihadi, walikwepa kutekeleza faradhi hiyo ya dini kwa visingizio mbalimbali. Aya hii ya 21 tuliyosoma inawahutubu watu hao ya kwamba: mantiki ya kuwa na imani ya kweli ni kuwa tayari kutii amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kuacha kutoa kauli za ubabaishaji na visingizio visivyo na maana; kwa sababu kauli zenu hizo zitawadhoofisha na kuwavunja moyo waumini na kuwafanya wasijitokeze kwenye medani ya Jihadi kukabiliana na maadui wanaopinga na kuipiga vita haki. Kisha aya inaendelea kueleza kwamba: kama watu wa kundi hili la wenye imani dhaifu ni wakweli kwa hayo wanaoyodai kwamba wameamini, basi inapasa washiriki katika Jihadi ya kubariziana na maadui, kwa sababu kufanya hivyo kutawapa wao nguvu na izza hapa duniani na kulipwa malipo mema na Allah huko akhera. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, sharti la kuwa muumini wa kweli ni kusema maneno mema na ya kheri na kufanya mambo kulingana na maamrisho ya Mwenyezi Mungu; isiwe ni kujisemea lolote lile tupendalo na kujifanyia chochote kile tutakacho. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, Jihadi ya kubariziana na maadui ni mojawapo ya amri za Allah SWT. Inatupasa tuwe wakweli katika utekelezaji wake na kujiepusha na utoaji kisingizio chochote kile, kwa sababu kupigana Jihadi na kuwa wakweli ni kwa manufaa ya mtu mwenyewe.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 22 na 23 za sura yetu ya Muhammad ambazo zinasema:
فَهَلْ عَسَيْتُمْ إِن تَوَلَّيْتُمْ أَن تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ وَتُقَطِّعُوا أَرْحَامَكُمْ
Basi mkishageuka yanatarajiwa kwenu (mengine) isipokuwa mfisidi katika nchi na kuukata udugu wenu?
أُولَٰئِكَ الَّذِينَ لَعَنَهُمُ اللَّهُ فَأَصَمَّهُمْ وَأَعْمَىٰ أَبْصَارَهُمْ
Hao ndio Mwenyezi Mungu amewalaani, na akawatia uziwi, na akawapofusha macho yao.
Aya hizi zinaendeleza yale yaliyozungumziwa katika aya iliyotangulia kuhusu watu wenye imani dhifu na kueleza kwamba: kama mtakengeuka kutii amri ya Mwenyezi Mungu kuhusu Jihadi, jueni kwamba washirikina watakushindeni na mtaishia kurudi kwenye mila za kijahilia. Mila ambazo zinachochea kuenea ufisadi na uharibifu katika jamii, mauaji na umwagaji damu kwa sababu ya taasubi na ukereketwa wa kikabila na yumkini hata mkarudi kwenye enzi za kuwatoa roho watoto wa kike kwa kuwazika huku wakiwa hai. Kisha Qur'ani inaendelea kueleza kwamba, tabia ya kukwepa kwenda kupigana Jihadi na kutoa vijisababu na visingizio visivyo na msingi kutayafanya masikio na macho ya watu hao wenye imani dhaifu na wanafiki wasiisikie wala wasiione haki na kukosa kujua hakika na ukweli. Na ni wazi kwamba, mtu asiyeweza kuisikia na kuiona haki sawasawa na kwa usahihi husimama dhidi yake kuipinga na kuishia kukosa rehma za Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kwa mtazamo wa Qur'ani, kuiacha Jihadi kunaandaa mazingira ya kuenea ufisadi na umwagaji wa damu kidhulma. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuyapa mgongo mafundisho ya dini, kunapelekea kudhoofika mafungamano ya kifamilia, udugu na ujamaa. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, watu wanaochochea ufisadi katika jamii na kuvuruga nidhamu ya familia, sio tu wanabaidishwa na kuwekwa mbali na rehma za Mwenyezi Mungu, bali wanalaaniwa pia na Yeye Mola. Wa aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba, kuwa na masikio na macho tu hakutoshi. Lililo muhimu zaidi ni kuvitumia viungo hivyo kwa njia sahihi. Kwani si hasha watu wakawa na masikio lakini wasiwe tayari kuisikiliza haki, au wakawa na macho lakini wasiwe tayari kuiona na kuitazama.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 24 ambayo inasema:
أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ أَمْ عَلَىٰ قُلُوبٍ أَقْفَالُهَا
Je! Hawaizingatii Qur'ani? Au kwenye nyoyo (zao) kuna kufuli?
Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia iliyotaja sifa za watu wenye imani dhaifu na kueleza kwamba: chanzo cha matatizo yote ya watu hawa ni ama hawatafakari na kutaamali katika kuzifahamu aya za Qur'ani, au kutokana na kuabudu hawaa na matamanio ya nafsi zao, hawayakubali na wanaamua kuyapiga vita yale waliyoyafahamu kutokana na aya hizo. Japokuwa aya hii inawazungumzia watu wenye imani dhaifu, lakini aya ya 29 ya Suratu-Saad inaonyesha kuwa kutafakari na kutaamali aya za Qur'ani ni jukumu la waumini wote iliposema: "Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili". Ni kwa sababu hii, ndio maana Siku ya Kiyama, Bwana Mtume Muhammad SAW atamshtakia Allah SWT juu ya kuhamwa kwa Qur'ani, kosa ambalo linaujumuisha umma wote wa Kiislamu, ikiwa ni ishara ya sisi Waislamu kutokipa uzito na umuhimu kinaostahiki Kitabu hicho kitukufu cha mbinguni. Ni kama inavyoeleza aya ya 30 ya Suratul-Furqan ya kwamba: "Na Mtume alikuwa akisema: Ee Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur'ani ni kihame". Upuuzaji huo tunaoufanya ni wa hali tatu: Hali ya kwanza ni ya Waislamu ambao hawaisomi kabisa Qur'ani. Hali ya pili ni ya wale ambao wanaisoma, lakini hawatafakari wala kuzingatia maana ya aya zake. Na hali ya tatu inawahusu Waislamu ambao, licha ya kuisoma Qur'ani, kutafakari na kutambua maana ya aya zake, lakini hawayafuati wala hawayatekelezi kivitendo mafundisho yake. Kwa hivyo ufahamu na uelewa sahihi wa mafundisho ya Qur'ani, inapasa uwe msingi wa tabia na matendo ya umma wa Kiislamu ili rehma za Allah SWT zienee katika jamii za Waislamu na kuwasahilishia mambo yao. Kinyume na hivyo, ni nyoyo za watu kwanza, kufungika kama zilizotiwa kufuli, na kisha jamii yenyewe ya Waislamu kukumbwa na matatizo na masaibu kadha wa kadha, ambayo hupelekea kufungika njia ya kufikia saada na uokovu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, Qur'ani haikuteremshwa kwa ajili ya kusomwa tu; ni kitabu cha kutafakari na kutaamali; na kusomwa kwake inatakiwa uwe ni utangulizi wa kuzingatia na kuzitafakari aya zake. Kwa hivyo watu wasioyatafakari yaliyomo ndani ya Qur'ani, wanakemewa na Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, Waislamu wote wana wajibu wa kuzifahamu na kuzielewa aya za Qur'ani na kisha kutaamali na kuyatafakari yaliyomo ndani yake; na kufanya hivyo hakulihusu kundi fulani tu la watu miongoni mwao. Na vilevile aya hii inatutaka tufahamu kwamba, kuacha kutaamali na kutafakari tunaposoma Qur'ani kunautia kufuli moyo na roho ya mtu; na nyoyo zilizotiwa kufuli hushindwa kutaamali na kutafakari aya za Qur'ani na kukosa neema na faida za maneno hayo matukufu ya Allah. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 932 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah aijaalie Qur'ani sababu ya uthabiti wa imani zetu, kuongezeka taqwa ndani ya nyoyo zetu na Siku ya Kiyama kuja kuwa muombezi wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/