Jun 12, 2023 14:51 UTC
  • Mchango wa Maulamaa (71)

Assalaam alaykum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote pale yanapokufikieni matangazo haya kutoka hapa mjini Tehran.

 

Karibuni kutegea sikio sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili tuweze kupekua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu, bila kusahau athari na vitabu vyao. Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Jahangir Khan Ghashghaei, mmoja wa wasomi na wanafalsafa mahiri ambaye alianza kusoma akiwa na umri wa miaka 40. Tuliona jinsi alimu huyu alivyofanya hima ya kusoma falsafa katika zama ambazo taaluma hii ilitambuliwa kuwa ni ukafiri na akafanikiwa kulea wanafunzi wengi sambamba na kubadilisha mtazamo watu na hata wasomi mbalimbali kuhusiana na elimu ya falsafa. Mmoja wa wanafunzi wake ni Muhammad Hussein Fadhil Toni ambaye tutamzungumzia katika kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 71 ya mfululizo huu. Nina wingi wa matumaini kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Muhammad Hussein Fadhil Toni alizaliwa usiku wa 25 Muharram 1298 Hijria sawa na tarehe 28 Disemba 1880 Miladia. Alizaliwa katika moja ya maeneo ya Khorasan Kusini kwa jina la Ton ambalo leo hii linajulikana kwa jina la Ferdows. Baba yake ni Mulla Abdul-Adhim ambaye alikuwa mtoa waadhi mashuhuri katika mji huo na alikuwa na umashuhuri huku akipendwa mno na watu wa eneo hilo. Baba huyo alifahamu na kutambua haraka mno kipaji alichokuwa nacho mtoto wake. Kabla ya Muhammad Hussein kufikia umri wa masomo, alimchukua na kumpeleka katika maktaba ya nyumbani.

Tangu mwanzoni tu uwezo wake wa kuhifadhi mambo na kasi ya kujifunza mambo ilikuwa kubwa kiasi kwamba, hilo liliwashangaza watu wote. Alijifunza kusoma kwa muda mfupi sana na baada ya miezi michache pia akaanza kufanya mazoezi ya kuandika. Baada ya hapo akaanza kusoma utangulizi wa masomo ya Kiarabu na kisha akawa amehifadhi Qur’ani yote.  Haukupita muda wa miaka mitatu au minne tangu aanze kusoma ambapo alipomteza baba yake aliyefariki dunia. Hata hivyo hilo halikupunguza katu huba na shauku yake ya pamoja na bidii ya kutafuta elimu.

Muhammad Hussein Fadhil Toni

 

Baada ya muda, baadhi ya watu wakawa wakiwapeleka watoto wao kwa Muhammad Hussein Fadhil Toni ili awafundishe. Alipofikisha umri wa miaka 17 alisafiri na kwenda katika mji wa Mash’had Iran kwa ajili ya kuhudhuria masomo ya walimu wakubwa na mahiri katika zama hizo. Alipowasili Mash’had alianza kuhudhuria masomo katika shule ya Navvab na kuhudhuria masomo yaliyokuwa yakifundishwa na marehemu Adib Neyshabouri wa kwanza. Ni katika miaka hii ambapo mwalimu wake alimpa lakabu ya Fadhil kutokana na kipaji na umahiri katika elimu na kuanzia hapo ndipo watu wote wakawa wakimtambua kwa lakabu ya Fadhil Toni.

 

Fadhil Toni, kinyume na wanafunzi wengine wa masomo ya dini alikuwa na uzingatiaji maalumu na suala la kujifunza elimu za kiakili kama hisabati, jiometri na nujumu, na katika kipindi ambacho alikuwa katika mji wa Mash’had kwa ajili ya kusoma masomo ya dini alifuatilia na kusoma kwa bidii pia elimu hizo na kuwa mwalimu na ustadhi mahiri katika elimu na taaluma zote hizo.

 Fadhil Toni alibakia katika mji wa Mash’had kwa muda wa miaka 6 na baada ya hapo akiwa pamoja na mwanafunzi mwengine ambaye baadaye alifahamika kwa jina la Sheikh Muhammad Hakim alielekea katika mji wa Isfahan, Iran.

Katika zama hizo mji wa Isfahan ulikuwa kitovu cha elimu na maarifa na soko la elimu za dini na falsafa lilinawiri katika mji huo. Katika siku za awali tu za kuweko kwake katika mji wa Isfahan Fadhil Toni alianza kushiriki darsa ya falsafa iliyokuwa ikifundishwa na Jahangir Khan Ghashghaei na hakukosa hata siku moja katika masomo hayo yaliyodumu kwa takribani miaka 6.

Allama Fadhil Toni alibakia katika mji wa Isfahan kwa muda wa miaka 11. Katika miaka hiyo mbali na kusoma na kutafuta elimu na kufanya mijadala na kufundisha, alikuwa akilipa umuhimu mno suala la ibada na kulea nafsi. Pamoja na kuwa katika miaka hiyo kwa upande wa kifedha na uwezo wa kimaada, ilikuwa miaka migumu sana kwa Fadhil Toni na iliyoambatana na taabu na mashaka ya kimaisha, ambapo kuna wakati mwingi ilikuwa ikitokea kwamba, hana fedha ya kununulia chakula, lakini daima alikuwa akikitaja kipindi hiki kuwa miaka mbora kabisa ya umri wake.

 

Akili na maarifa ya hali ya juu aliyokuwa nayo ambayo yalionekana kuwa ni ya kushangaza sambamba na hamu na shauku yake kubwa ya kusoma na kutafuta elimu na maarifa ni mambo ambayo kwa hakika yalikuwa na msukumo na kumfanya abadilike na kuwa ustadh mahiri na kamili. Alikuwa na hima na bidii isiyochoka na isiyo na kikomo katika uwanja huo.

 

Kipindi fulani alikuwa akifundisha katika chuo mashuhuri cha Dar al-Funun. Mwaka 1313 Hijria ambapo kuliasisiwa kitivo cha teolojia na maarifa ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Tehran, Fadhil Toni aliitwa kwa ajili ya kwenda kufundisha falsafa, teolojia na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Kwa utaratibu huo, kwa miaka mingi wakaondokea maelfu ya wanafunzi waliosoma kwake na kuleleka katika darsa na masomo yake.

Inaelezwa kuwa, wakati wa kufundisha Fadhil Toni mbali na kubadilisha kikamilifu uzungumzaji wake, alikuwa na umahiri wa aina yake ambapo alikuwa akieleza maudhui za masomo kwa ufasaha wa hali ya juu ambapo hata jambo gumu kiasi gani alikuwa akilifafanua kwa lugha nyepesi na kwa mbinu ya kumfanya mwanafunzi afahamu.  Sifa yake kuu katika ufundishaji inatajwa kuwa ni nguvu yake ya kubainisha mambo kwa lugha nyepesi na ya kueleweka.

Wakati wa kufundisha mbali na kubainisha maudhui za masomo akiwa na nia ya kuwafanya wanafunzi wasichoke na somo alikuwa akitumia mbinu ya kubainisha baadhi ya visa na mambo ya kufurahisha na ilikuwa mara chache sana afundishe na kusiweko na visa vya mzaha na vya kufurahisha. Hili liliwafanya wanafunzi kuwa na shauku na somo lake na wakati huo huo kutochoka wakiwa darasani.

Ayatullah Hassanzadeh Amoli

 

Kuna wanafunzi wengi waliosoma kwa Fadhil Toni. Baadhi ya wanafunzi hao ni Allama Ayatullah Hassanzadeh Amoli na Ayatullah Abdallah Jawad Amoli ambapo wawili hao walikuwa miongoni mwa watu wachache katika zama zao waliokuwa mahiri katika elimu na maarifa. Mwanafunzi mwingine wa Fadhil Toni ni Dakta Dhabihullah Safa, anayejulikana kwa jina la baba wa elimu ya historia ya fasihi ya lugha ya Iran.

Fadhil Toni aliaga dunia 1961 akiwa na umri wa miaka 82 na kuzikwa katika mji wa Qom katika makaburi ya Sheikhan, umbali wa mita kadhaa kutoka katika haram ya bibi Fatma Maasuma (as).

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umemalizika. Msikose kujiunga nami tena juma lijalo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh