Maswali Kuhusu Tukio la Ashura (12)
(last modified Sat, 27 Oct 2018 11:10:11 GMT )
Oct 27, 2018 11:10 UTC
  • Maswali Kuhusu Tukio la Ashura (12)

Haram na makaburi matakatifu ya Mtume Muhammad (saw) na Maimamu maasumu wa nyumba yake tukufu (as) katika kipindi chote cha historia ya Uislamu ya zaidi ya miaka 1400, yamekuwa kimbilio la nyoyo zenye hamu kubwa za waumini na wafuasi wao.

Pamoja na hayo katika kipindi cha karne mbili zilizopita, Mawahabi wameharamisha ujenzi wa majengo juu ya makaburi hayo kwa hoja isiyo na msingi kwamba jambo hilo linapelekea kushirikishwa Mwenyezi Mungu kwenye ibada. Katika kipindi cha juma hili tutazungumzia madai hayo yasiyo na msingi na mgongano wake wa moja kwa moja na mafundisho ya Qur'ani Tukufu pamoja na Sunna za Mtume (saw) na Maimamu wa nyumba yake tukufu (saw), karibuni.

Haram ya Imam Hussein AS, Karbala Iraq

 

Hatua ya kwanza iliyochukuliwa na viongozi wa Mawahabi ilikuwa ni kubomoa na kuharibu kaburi la Imam Hussein (as) mwaka 1216 Hijiria na miaka mitano baadaye wakachukua hatua nyingine kama hiyo ya kuharibu makuba ya makaburi ya Maimamu katika makaburi ya Baqee'. Makaburi hayo yalikarabatiwa tena na Waislamu lakini yakaharibiwa tena na Mawahabi hao waovu mwaka 1344 Hijiria. Baada ya matukio hayo, suala la ujenzi juu ya makaburi likageuka kuwa changamoto muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu. Kinyume na itikadi ya Mawahabi, Waislamu wengine wote wanaamini kuwa ujenzi juu ya makaburi, iwe ni kujenga jengo, kuba, msikiti au madrasa ni jambo linalokubalika na kuruhusiwa na dini. Licha ya kuwa kuna wanazuoni wachache wa Kisuni wanaosema kuwa jambo hilo ni makruhu katika baadhi ya sehemu lakini wengi wanasema kuwa ujenzi wa majengo juu ya makaburi ya Manabii, Mashahidi na waja wengine wema wa Mwenyezi Mungu ni mustahab, kwa maana kuwa ni jambo linalopendekezwa kufanywa. Mashia katika kipindi chote cha historia ya Uislamu wamekuwa wakiupa umuhimu maalumu ujenzi wa majengo na haram juu ya makaburi ya Maimamu wao watukufu na kuhimiza wafuasi wao watembelee na kufanya ziara kwenye makaburi hayo. Bila shaka Waislamu wana hoja na dalili za Kiqur'ani, kiakili na kihistoria kuhusu jambo hilo, ambapo muda si mrefu tutazungumzia baadhi ya dalili hizo.

 

Katika Sura ya Kahf, Qur'ani Tukufu inazunghumzia kisa cha Watu wa Pango na kuashiria hitilafu iliyozuka kati ya Wakristo na Mushrikina kuhusiana na maiti za watu hao. Inasema baadhi yao walitaka ukuta ujengwe mbele ya pango ambako miili yao ilikuwa na kundi jingine likataka msikiti na sehemu ya kufanyia ibada ijengwe juu ya makaburi yao. Kwa mujibu wa Aya ya 21 ya Surat al-Kahf, waumini walishinda na hatimaye kufanikiwa kujenga msikiti na sehemu ya kufanyia ibada juu ya makaburi ya watu hao wa pango, na hapo pakawa mahali pa kudhikiri na kufanyia ibada ya Mwenyezi Mungu. Qur'ani Tukufu inaelezea kisa hicho bila ya kuashiria kuwa kilikuwa ni kitendo cha shirki. Ni wazi kwamba kama kitendo hicho cha kujenga jengo au msikiti juu ya makaburi kingekuwa ni cha shirki bila shaka Qur'ani ingekiashiria na kukikemea.

Kitendo cha kujenga kwenye makaburi kina historia ndefu ambayo inarejea nyuma hadi mwanzoni mwa kudhihiri Uislamu. Mtume Mtukufu (saw) alimzika Fatimah bint Asad, mama yake Imam Ali (as) katika sehemu ya msikiti, na sehemu hiyo ikaja kujilikana katika historia ya Uislamu kama Kaburi la Fatimah. Baada ya kuaga dunia, Mtume Mtukufu (saw) alizikwa ndani ya nyumba yake, na tokea hapo Waislamu na makhalifu walikuwa wakilinda na kuikarabati nyumba hiyo na hata mara nyingine wakiipamba na kuirembesha. Katika karne ya saba, kuba la kwanza lilijengwa juu ya kaburi hilo la Mtume (saw) ambapo makahalifa wa Bani Abbas na Othamania walikuwa wakikarabati na kuijenga upya Haram hiyo ya Mtume (saw).

 

Kujenga makuba juu ya makaburi ya Maimamu maasumu (as) ni matukio ya kihistoria ambayo Mashia wamekuwa wakiyazingatia sana. Haram ya Imam Ali (as) ina kuba na jengo kubwa ambalo lilijengwa katika karne ya pili Hijiria. Makaburi ya Maimau wa Baqee', watukufu na masahaba wengine pia yalikuwa yamejengewa majengo na makuba. Katika karne zilizofuata, makaburi ya viongozi wa madhehebu tofauti ya Kisuni pia yalijengwa juu yake majengo na makuba. Kaburi la Abu Hanifa, kiongozi wa Mahanafi mjini Baghdad, Kaburi la Malik bin Anas, Kiongozi wa Mamalik katika makaburi ya Baqee' na Kaburi la Ahmad bin Hambal, kiongozi wa Mahambal mjini Baghdad, yote hayo yalikuwa na makuba na majengo.

Kama mnavyoona, tokea zama za Mtume (saw) hadi mamia ya miaka baada yake, kuna mifano mingi ya majengo na makuba yaliyojengwa juu ya makaburi. Suala hilo lilitekelezwa kwa karne nyingi mbele ya macho ya Waislamu na wala hakuna wanazuoni wowote wa Kiislamu wawe ni wa Kishia au wa Kisuni waliolalamikia jambo hilo. Hakuna mtu yeyote aliyeamini kwamba ujenzi wa aina hiyo ulikuwa shirki au kuwatuhumu Waislamu waliotekeleza jambo hilo kuwa walikuwa mushirikina, waabudu masanamu au kufanya ibada ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Hivyo madai ya Mawahabi kwamba kujenga haram za Maimamu na waja wengine wema wa Mwenyezi Mungu ni bida' na haramu ni jambo linalopingwa vikali na wanahistoria na kwa kuzingatia uthibitisho wa historia tunaweza kusema wazi kwamba kitendo cha Mawahabi cha kuvunjia heshima na kubomoa makaburi ya mawalii wa Mwenyezi Mungu ndio bida' inayokwenda kinyume mienendo na suna za Mtume pamoja na mafundisho sahihi ya Uislamu.

 

Mbali na ujenzi wa makaburi, kuyazuru makaburi hayo lilikuwa  jambo la kawaida kabisa katika zama za Mtume Mtukufu (saw) kwa kadiri kwamba kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika vya Masuni na Mashia, baada ya kukombolewa mji mtakatifu wa Makka na akiwa njiani kurejea mjini Madina, Mtume (saw) alienda kulizuru kaburi la mama yake, Bibi Amina na kusema: "Hili ni kaburi la mama yangu. Nilimuomba Mwenyezi Mungu anijaalie fursa ya kulizuru naye akanijaalia fursa hiyo." Baada ya kuuawa shahidi Hadhrat Hamza (as) katika vita vya Uhud, Bibi Fatimat az-Zahra (as) binti ya Mtume (saw) alikuwa akilizuru kaburi lake kila siku ya Ijumaa na wala Mtume hakuwa akimzuia kufanya hivyo.

Kuna Riwaya na mapokezi mengi ya kihistoria katika vitabu vya Ahlu Suna ambayo yanaonyesha kwamba kuzuru makaburi ni jambo linalokubaliwa na kupendekezwa pia na Masuni. Imeandikwa katika vitabu kadhaa vya kuaminika vya Masuni vikiwemo vya Sahih Muslim na Sunan Abi Dawoud ambapo Mtume (saw) amenukuliwa akisema: "Zamani nilikuwa nikikukatazeni kuyazuru makaburi lakini sasa yazuruni kwa sababu yanakukumbusheni Akhera na kukuzidishieni heri yenu. Hivyo kila mtu anayetaka kuyazuru na ayazuru, ila tu asiseme maneno yasiyofaa na ya batili." Baada ya kuaga dunia Mtume (saw). Masahaba na Waislamu wengine wote walikuwa wakilizuru kaburi lake, na hadi leo wote, wawe ni Mashia au Masuni, wangali wanalizuru kaburi hilo tukufu la Mtume (saw) katika mji mtakatifu wa Madina, kutokana na Hadithi nyingi za Kiislamu kusisitiza juu ya fadhila na umuhimu mkubwa wa jambo hilo.

Arubaini ya Imam Hussein AS Karbala, Iraq

 

Vitabu vya kuaminika vya Masuni vinasema kwamba Mtume (saw) amesema: "Kila mtu anayezuru kaburi langu, shufaa yangu kwake itakuwa ni ya wajibu." Vitabu hivyo vinasema kuwa kila mara khalifa wa pili alipoingia katika mji wa Madina alikuwa akilitolea salamu kaburi la Mtume (saw). Hata imepokelewa kwamba masahaba walikuwa wakilizuru kaburi la Bilal al Habashi, Muadhini wa Mtume (saw) na kuomba hapo dua.

Kinyume na wanavyodai Mawahabi, kuzuru makaburi matakatifu ya mawalii wa Mwenyezi Mungu si utangulizi wa shirki hata kidogo bali ni uimarishaji wa Tauhidi ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na pia ni aina fulani ya mapambano ya kiitikadi katika njia hiyo. Matini za dua na ziara zinazosomwa na wafanyaziara pembeni ya makaburi ya mashujaa wa upwekeshaji huo katika historia, zimejaa mafundisho aali ya Tauhidi, Maad (Ufufuo), Utume na kujitolea mhanga katika njia ya Mwenyezi Mungu Mmoja. Anaposoma ziara hizo, mfayaziara huwa anashuhudia na kukiri juu ya utume wa Mitume wote wa Mwenyezi Mungu tokea Nabii Adam hadi Mtume wa Mwisho, Muhammad (saw), na kusifu pamoja na kuenzi juhudi kubwa na kujitolea walikofanya watukufu hao katika njia ya kunyanyua Tauhidi. Akiwa katika haram za Maimamu watoharifu (as) wa Nyumba ya Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu (saw), mfanyaziara huwa na mawasiliano ya moyoni na mashujaa wa ibada ya Mwenyezi Mungu na kwa kuzingatia fadhila zao, hufanya juhudi za kufuata mifano ya watukufu hao waliokamilika kiutu. Hivyo, madai ya kwamba kuwazuru mawalii wa Mwenyezi Mungu ni kuwaabudu, ni madai batili, ghalati na yasiyo na msingi wowote wa kimantiki.