Nov 11, 2018 09:16 UTC
  • Vita vya kiuchumi vya Marekani na Iran inayoendelea kusonga mbele kiustawi

Rais Donald Trump wa Marekani anaamini kuwa, awamu ya pili ya vikwazo dhidi ya Iran ni aina kali zaidi ya vikwazo itakavyo vihimili Iran. Awamu hiyo ya pili ya vikwazo vya serikali ya Washington ilianza kutekelezwa tarehe 5 Novemba; vikwazo ambavyo vinawaathiri moja kwa moja raia wa kawaida wa Iran.

Uchukuaji hatua wa Trump wa kuvuka mipaka ya sheria

Baada ya kuanza kutekelezwa awamu ya pili ya vikwazo vya Marekani, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema: "Ilichofanya Marekani ni kuwawekea mbinyo wananchi tu, si kumwekea mbinyo mtu mwengine yeyote yule. Lakini pia kwa watu wengine, mataifa mengine, mashirika mengine na serikali za nchi zingine. Leo si Iran peke yake iliyokasirishwa na siasa za Marekani; hata mashirika na serikali za nchi za Ulaya pia zimekasirishwa na siasa za Marekani."

Vikwazo vipya vya Marekani vimeilenga sekta ya mafuta pamoja na mabadilishano ya kibenki na kibiashara ya Iran. Maana ya kuweka vikwazo hivyo ni kuukata ushirikiano baina ya uchumi wa dunia na Iran. Marekani inajaribu kufanya kila njia kuishinikiza kiuchumi Iran ili hatimaye, kwa mawazo yake, iilazimishe kusaini makubaliano mapya kuhusiana na mpango wake wa nyuklia. Katika kuizungumzia nukta hiyo, Mohammad Kazem Sajjadpur, mkuu wa kituo cha taaluma za kisiasa na kimataifa cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alitamka haya yafuatayo alipohutubia Chatham House, kituo cha Masuala ya Kimataifa cha Uingereza, huko mjini London: "Iran haikubali vitisho vya Marekani; na wala haiwezekani kuilazimisha Tehran ifanye mazungumzo mapya kwa kuiwekea vikwazo."

Mnamo tarehe 8 Mei mwaka huu, wakati Donald Trump alipojitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, alidai kwamba, makubaliano hayo yanainufaisha Iran peke yake na yana madhara kwa Marekani; hivyo lazima yasainiwe makubaliano mengine mapya. Inacholenga Marekani kuhusu makubaliano mapya ni kutaka kuingiza masuala mengine kwenye makubaliano hayo, ambayo hayana uhusiano wowote na kadhia ya nyuklia. Uwepo imara wa Iran katika eneo pamoja na mpango wake wa makombora ni mihimili miwili muhimu ya uwezo na nguvu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na Marekani imekuwa ikijaribu kutumia kila njia ili kutia mkono wake kwenye masuala hayo. Harakati na uwepo athirifu wa Iran katika Mashariki ya Kati na uwezo wake wa makombora, ambapo sehemu ya uwezo huo ilionekana hivi karibuni katika manuva ya pamoja ya ulinzi wa anga yaliyopewa jina la Velayat-97, umeifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dola lenye sauti ya juu katika mlingano wa nguvu katika eneo hili. Kombora la ardhini kwa angani la Shalamche na mfumo wa makombora ya masafa ya kati wa Tabas, vilifanyiwa majaribio kwa mafanikio katika mazoezi hayo ya kijeshi ya ulinzi wa anga ya Velayat-97. Kuhusiana na suala hilo, Adimeri Msaidizi Mahmoud Mosavi, msemaji wa manuva hayo, alisema, jaribio la ufyatuaji kombora la Shalamche na mfumo wa makombora ya masafa ya kati lilifanyika kwa mafanikio na akafafanua kwamba: "Kuundwa na kufanyiwa kazi zana hizi kwa kutumia teknolojia za kisasa kunaonyesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inao uwezo wa kujikidhia mahitaji yake kwa kutegemea uwezo wa ndani."  

Tajiriba yenye taathira ya taifa la Iran

Vikwazo vya Marekani vimetangazwa na kuanza kutekelezwa kwa shangwe na propaganda tele, ilhali kwa wananchi wa Iran, vikwazo hivyo si kitu kipya kwao bali vimekuwepo kwa muda wote tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Katika hotuba aliyotoa mbele ya hadhara ya maelfu ya wanafunzi na wanachuo kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka huu ya Aban 13, yaani Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei alisisitizia nukta hiyo kwa kusema: "Moja ya harakati za (viongozi wa) Marekani katika miaka hii 40 ni kutumia (silaha ya) vita vya kiuchumi. Hii kusema kwao kwamba, vikwazo ni hatua mpya dhidi ya Iran, kwa kweli ni kujihadaa nafsi zao au kuwahadaa wananchi wa Marekani, kwa sababu kadhia ya vikwazo imekuwepo tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu."  

Bila ya shaka taathira za vikwazo zitahisika katika maisha ya wananchi wa Iran, hata hivyo hata huko nyuma pia, na katika nyakati tofauti, wananchi hao waliweza kuvivuka vipindi vigumu vya vikwazo kwa istiqama na uvumilivu. Umoja, mshikamano na kupanga mipango yenye malengo ni sharti la lazima kwa ajili ya kuivuka awamu mpya ya vikwazo vya Marekani. Lengo moja kuu la serikali ya Trump katika kutekeleza vikwazo ni kuwatenganisha wananchi na viongozi wao; lakini katika hilo pia Marekani imeambulia patupu katika muda wote huu wa miaka 40.

Maandamano ya mwaka huu ya Aban 13 ya Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari yalithibitisha umoja na mshikamano uliopo kati ya wananchi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu; na katika azimio la mwishoni mwa maandamano hayo ilielezwa kinagaubaga kuwa, wananchi wa Iran wataendelea kupambana na ukoloni na ubeberu wa Marekani. Mahudhurio ya hamasa ya mamilioni ya Wairani katika maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari yaliakisiwa kwa wingi na vyombo mbalimbali vya habari duniani, ambavyo vilisisitiza kwamba, sambamba na kuanza kutekelezwa vikwazo vipana vya Marekani, wananchi wa Iran walijitokeza barabarani na kulaani siasa za Marekani.

Kuhalifu ahadi kwa Marekani

Kujitoa Marekani katika JCPOA na kisha kuvirejesha tena vikwazo vyote vya nyuklia dhidi ya Iran katika awamu mbili (Agosti 7 na Novemba 5, 2018) ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na kutojali Marekani mikataba ya makubaliano. Muelekeo aliofuata Trump katika kukabiliana na Iran hauilengi Jamhuri ya Kiislamu pekee, lakini dharau aliyoonyesha kwa sheria za kimataifa ina taathira pia kwa ulimwengu na nchi zote. Sera za serikali ya Trump ni za kuutwisha ulimwengu matakwa yake na kutaka kufanikisha malengo na maslahi yake kwa njia yoyote ile iwezekanayo. Katika hali kama hiyo ni jambo la dharura kwa nchi zote duniani kusimama kidete kukabiliana na Marekani.

Japokuwa wanachama waliosalia katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hawakubaliani na muelekeo wa serikali ya Trump na wanasisitiza kwamba wanapinga vikwazo vya nje ya mipaka ya sheria vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Iran, lakini matarajio yaliyopo ni kuchukuliwa hatua za kivitendo juu ya suala hilo. Kuhusiana na nukta hiyo, waziri wa uchumi na fedha wa Ufaransa, Bruno Le Maire, amependekeza kuongezwa utumiaji wa sarafu ya yuro kwa ajili ya kukabiliana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran. Le Maire amesema: "Radiamali na mjibizo wa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran inapasa ujumuishe pia hatua za kuimarisha sarafu ya yuro katika miamala ya kimataifa."

Kabla ya hapo, nchi kadhaa wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) zilisisitiza pia kupitia taarifa yao ya pamoja kwamba, zimeazimia kuendelea kushirikiana na Russia na China pamoja na mataifa mengine ili kudumisha mabadilishano yao ya kifedha na Iran bila kujali vikwazo vya Marekani.

Harakati ya Iran katika mkondo wa ustawi

Alaa kulli hal, kinachoonekana katika uhalisia wa mambo ni kwamba, Iran inapiga hatua kuelekea kwenye vilele vya ustawi na maendeleo licha ya mbinyo na mashinikizo ya kiuchumi ya Marekani. Juhudi zinazoendelea kufanywa kila leo na vijana wenye vipawa nchini katika kuzalisha sayansi mpya ya Nano, utajiri wa maliasili lilionao taifa hili na kuendelezwa uzalishaji wa ndani ili kufikia lengo la kujitosheleza na kujitegemea, zote hizo ni ishara za mafanikio na utegemeaji wa uwezo wa ndani kwa ajili ya kuyavuka matatizo ya nje.

Tajiriba ya miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu inaonyesha kuwa hakuna tatizo lisiloweza kutatuka. Kwa hima na bidii zaidi zitakazofanywa na wananchi na serikali, vigingi na vizuizi hivi vigumu vya sasa pia vitavukwa kwa mafanikio na kwa manufaa ya taifa la Iran. Ni kwa kuzingatia tajiriba hiyo, ndipo Waziri wa Mambo ya Nje Mohammad Javad Zarif akasisitiza katika ujumbe wake kwa wananchi wa Iran mara baada ya kuanza kutekelezwa awamu ya pili ya vikwazo vya Marekani kwamba: Marekani itajuta kwa hatua ilizochukua dhidi ya Iran. Kuhusiana na nukta hiyohiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei amesema, lengo la Marekani la vita na vikwazo vya kiuchumi ilivyoweka katika kipindi cha miaka 40 iliyopita hadi sasa ni kuisambaratisha Iran na kuifanya ibaki nyuma kimaendeleo. Hata hivyo amesisitiza kuwa: Katika vita vya kiuchumi pia, kilichotokea ni kinyume na ilivyotaka Marekani, kwa sababu harakati ya kuelekea kwenye kujitegemea na kujitosheleza pamoja na uzalishaji wa ndani imeshika kasi, na leo hii mamia ya makundi amilifu na ya uchapakazi ya vijana wabunifu wa vyuo vikuu yanaendesha harakati na kuchapa kazi muhimu nchini. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia hali na nafasi ya Marekani duniani na kusisitiza kuwa: “Katika mtazamo mpana zaidi, nguvu, uwezo na haiba ya Marekani duniani vinaelekea kufifia na kutoweka; na Marekani ya leo ni dhaifu zaidi mara kadhaa kuliko Marekani ya miongo minne kabla yake".../

 

 

 

Tags