Haki za binadamu, kuanzia nara hadi matendo
Jumatatu ya tarehe 10 Disemba wiki hii dunia iliadhimisha Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu. Hii leo suala la Haki za binadamu limekuwa miongoni mwa mijadala muhimu zaidi katika fikra za walimwengu na kwenye duru mbalimbali za kimataifa.
Suala hilo lilipewa umuhimu mkubwa sana kiasi kwamba, miaka mitatu tu baada ya kuasisiwa Umoja wa Mataifa, Baraza Kuu la Umoja huo lilipasisha Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu. Azimio hilo lenye lengo la kudhamini usawa wa haki na uhuru kwa wanadamu wote, lilipasishwa tarehe 10 Disemba mwaka 1948 na miaka ya baadaye siku hiyo ilitambuliwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu. Lengo kuu la kutangazwa siku hiyo ni kuwataka walimwengu wote watilie maanani na kujali haki zote za kiumbe huyo.
Kifungu cha kwanza kabisa cha Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu kinasema: Wanadamu wote wanazaliwa wakiwa watu huru na wana hadhi, utukufu na haki sawa. Miaka iliyofuata ulionekana udharura wa kuzidishwa vipengele kadhaa katika Azimio la Kimataifa Haki za Binadamu ikiwa ni pamoja na kuwatambua mateka wa vita, wakimbizi, wanawake, wapinzani wa vita, wahanga wa mateso na watoto kuwa ni wanadamu wanaostahiki kudhaminiwa haki za kimsingi za mwanadamu. Haki hizo zilisajiliwa katika nyaraka za kimataifa, na Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu likatambuliwa kuwa ni miongoni mwa nyaraka muhimu zaidi za dunia. Azimio hilo limetumiwa na nchi nyingi duniani kama kigezo katika kubuni na kutunga sheria na katiba zao za kitaifa.
Kifungu nambari tano cha Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu kinasema: Kila mtu ana haki ya kudhaminiwa hali bora ya kiafya na maisha mazuri yeye na familia yake hususan katika upande wa chakula, mavazi, makazi na kupewa huduma za tiba na huduma nyingine muhimu za kijamii. Kifungu nambari 20 cha azimio hilo pia kinasisitiza kuwa, kila mwanadamu ana haki ya kupata kazi na ajira.
Hata hivyo na licha ya nchi nyingi duniani kutia saini azimio hilo lakini nchi hizo hizo zinakanyaga na kukiuka haki nyingi za binadamu. Inasikitisha kuona kwamba, idadi kubwa ya wanadamu wanaaga dunia kila siku duniani kutokana na njaa na kukosa huduma za tiba, na mamilioni wanasumbuliwa na matatizo ya kukosa ajira. Wanadamu wengi pia hii leo na licha ya maendeleo makubwa ya teknolojia ya mawasiliano, hawajui haki zao za kibinadamu. Vilevile tunaweza kusema kuwa, hakuna nchi inayoweza kudai kwamba, imetekeleza kikamilifu haki zote za binadamu.
Mikutano na makongamano mengi yamekuwa yakifanyika mara kwa mara katika nchi mblimbali kuhusu haki za binadamu lakini inasikitisha kuwa, mikutano hiyo imekuwa majukwaa ya kueneza propaganda na kaulimbiu zisizo tekelezeka. Hii leo pia haki za binadamu zimekuwa wenzo unaotumiwa na nchi kubwa kwa ajili ya kutimiza malengo yao ya kisiasa na hata ya kikoloni. Kama mfano tu tunaweza kuashiria mienendo ya Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya katika uwanja huu. Robert Fantina ambaye ni mwanaharakati na mtafiti wa masuala ya amani na uadilifu wa kijamii anazungumzia sera za kinduwakuwili za Marekani kuhusu haki za binadamu akisema: Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu lililotangazwa tarehe 10 Disemba mwaka 1948 na kutiwa saini na nchi nyingi ikiwemo Marekani, limeainisha haki za kimsingi za binadamu zinazopaswa kulindwa na kuheshimiwa na nchi zote. Lakini inasikitisha kwamba, Marekani haiheshimu na kutekeleza azimio hilo.”
Ukiukwaji mkubwa wa haki za Wamarekani weusi, dhulma ya kihistoria ya Wahindi Wekundu huko Marekani na uungaji mkono na misaada ya serikali ya Washington kwa tawala zinazoua watoto na wanawake za Saudi Arabia na Israel ni sehemu ndogo ya faili jeusi la haki za binadamu la Marekani.
Miongoni mwa vielelezo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na dola linalodai kuwa kinara wa kulinda na kutetea haki za binadamu la Marekani ni sera za kutowastahamili wahajiri za Rais Donald Trump wa nchi hiyo. Serikali ya sasa ya Marekani haikutosheka na hayo bali imekwenda mbali zaidi na kuamua kujiondoa katika Baraza la Haki za Bindamu la Umoja wa Mataifa ili kupata uhuru kamili wa kudumisha ukiukaji wake mkubwa wa haki za binadamu bila ya kusailiwa au kubanwa na sheria yoyote ya kimataifa. Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein anasema kuhusu hatua hiyo ya Marekani kujiondoa katika Baraza la Haki za Binadamu la UN kwamba: “Ni habari inayokatisha tamaa lakini si ya kustaajabisha kuchukuliwa na Marekani. Hata hivyo ilitarajiwa kuwa, nchi hiyo itapiga hatua kwenda mbele na si kurudi nyuma katika masuala ya haki za binadamu”.
Vita vya Yemen na misaada ya hali na mali ya Marekani kwa utawala unaoua watoto wa Saudi Arabia ni mfano mwingine wa mtazamo na sera za kindumakuwili za haki za binadamu za Marekani. Ripoti za Umoja wa Mataifa zinasema kuwa, mashambulizi ya Saudi Arabia huko Yemen na gharama kubwa ya fedha zinazotumiwa kutekeleza mpango wa kuiangamiza nchi hiyo vimechangia sana katika maafa ya kutisha yanayowasibu raia wa Yemen. Ripoti hizo zinasema mmoja kati ya kila watu watano wanaouliwa kwa mashambulizi ya Saudia nchini Yemen ni mtoto mdogo. Tarehe 9 Agosti mwaka huu peke yake ndege za kivita za Saudi Arabia zilishambulia basi la wanafunzi na kuua raia 51 ambao 40 miongoni mwao walikuwa watoto wadogo.
Mkurugenzi wa kikanda wa Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) Geert Cappelaere ametahadharisa kuhusu taathira mbaya za vita kwa mamilioni ya watoto wa Yemen na kusema kuwa, mgogoro wa nchi hiyo ni miongoni mwa maafa makubwa zaidi ya binadamu yaliyowahi kushuhudiwa duniani.
Maafisa wa shirka la Save The Children pia wanasema kuhusu haki za binadamu za watoto wa Yemen kwamba: Maelfu ya watoto wa nchi hiyo wamepoteza uwezo wa kuzungumza, kutikisa mikono yao au kutembea kutokana na athari mbaya za sauti za milipuko ya mabomu na makombora ya Saudia.
Kimsingi siasa za ndani za Marekani zinaamiliana na haki za binadamu kwa mtazamo wa kibaguzi na sera za kindumakuwili. Mfano wa ukweli huo ni wasifu ulioandikwa mwaka 2015 wa afisa wa jeshi la Marekani, Chris Kyle aliyeua wanaume, wanawake na watoto wasiopungua 160 wasio na hatia wa Iraq. Kutokana na ukatili huo Chris Kyle amekuwa mashuhuri nchini Marekani kwa jina la “Shetani wa Ramadi” (The Davil of Ramadi). Wasifu wa shetani huyo wa jeshi la Marekani sasa umefanywa filamu na yeye mwenyewe amefanywa shujaa wa taifa wa Marekani. Sasa hebu fikiria ingekuwaje lau nchi za Vietnam, Iraq, Aghanistan, Palestina, Yemen, Syria na nchi nyingine zilizowahi kuvamiwa na Marekani zingetengeneza filamu kuhusu shujaa wa kitaifa aliyeua Wamarekani 160 baada ya Marekani kuvamia nchi hiyo? Je nchi hizo zinaweza kutengeneza filamu kama hiyo na kuzionesha kwenye kumbi zao za sinema bila ya kuandamwa na madola ya Magharibi na kubambikiziwa tuhuma za aina mbalimbali? Hii ndiyo hali ya kusikitisha ya sera za kindumakuwili za Marekani na nchi nyingi za Maghaibi kuhusu haki za binadamu na ubaguzi mkubwa unaoshuhudiwa kuhusu haki hizo. Hali imefikia kiwango cha kuyatambua mauaji yanayofanywa na askari wa Marekani dhidi ya raia wa kawaida wa nchi nyingine kuwa ni haki yao ya kibinadamu na haki ya kujihami lakini hatua kama hiyo ikichukuliwa na nchi nyingine inatambuliwa kuwa ni jinai dhidi ya binadamu.
Tunamalizia kwa kusema kuwa, japokuwa Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu lilibuniwa kwa kutilia maana hadhi na utukufu wa kiumbe huyo lakini inasikitisha kwamba, hadi sasa azimio hilo halijapewa haki yake na kutekelezwa ipasavyo, bali kinyume chake, limefanywa wenzo wa kisaisa wa nchi za Magharibi kwa ajili ya kutimizia malego yao.