Sababu zilizoyafanya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yadumu
(last modified Sun, 07 Feb 2021 10:28:30 GMT )
Feb 07, 2021 10:28 UTC
  • Sababu zilizoyafanya Mapinduzi ya Kiislamu  ya Iran yadumu

Kwa mnasaba wa maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ambayo kilele chake ni tarehe 22 Bahman (10 Februari), tumekuandalia makala hii maalumu itakayozungumzia sababu zilizoyafanya mapinduzi hayo yadumu licha ya kupita miongo minne tangu kutokea kwake.

Mapinduzi ya Kiislamu yalikuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa na mapana ndani ya Iran na katika nchi nyingi duniani. Tukio hilo kubwa na la kihistoria lilibadilisha miamala mingi ya kisiasa duniani na katika eneo kwa manufaa ya wanaonyongeshwa na kupelekea kuibuka wimbi kubwa la harakati za ukombozi na kupigania kujitawala duniani kote. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliufanya Uislamu utukuke na kuwa na adhama; na yakahuisha pia utambulisho wa kidini wa Umma wa Kiislamu sambamba na kuwaonyesha walimwengu njia na namna ya kukabiliana na Uistikbari.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliyotokea mwaka 1979, mbali na kuteteresha na kutoa changamoto kwa sera za kibeberu za Marekani na madola mengine makubwa, lakini kutokana na kuendelea kudumu kwa zaidi ya miongo minne sasa, yametoa mafunzo na matamanio ya kupiganiwa na mwanadamu wa leo; mafunzo ambayo si tu hayachakai kutokana na muda kupita, bali mvuto wake kwa mwanadamu wa zama hizi unazidi kuongezeka kila uchao. Moja ya sifa za kipekee za Mapinduzi ya Kiislamu ni kudumu na kuendelea malengo yake ya asili. Jambo hili, na licha ya kupita miaka 42 tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, limeifanya harakati hii ya kukumbukwa milele iendelee kuwa na taathira ndani ya nyoyo na nafsi zenye kiu ya haki na uadilifu.

Mojawapo ya sababu zilizoyafanya Mapinduzi ya Kiislamu yaendelee kuwepo na kudumu ni kushikamana kwake na sira na fikra safi na za asili za viongozi wa Uislamu hususan Mtume wa rehma na huruma Muhammad SAW pamoja na mafunzo ya hamasa kuu za dini hiyo tukufu kama ya Mab’ath, yaani kupewa Utume mtukufu huyo, Ghadir, tukio la kuainishwa Khalifa na Imam wa umma pamoja na hamasa ya Ashura ya tukio la Karbala. Mapinduzi haya yanaendana na malengo matukufu kabisa ya mwanadamu na matarajio yake ya kimaanawi; na yalitokea pale fikra za kiliberali na kisoshalisti zilipokuwa zimepoteza mvuto wao, yakawaletea wanadamu ujumbe wa izza, heshima na uhuru. Ndipo jemadari wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini (MA) akasema: “Uislamu na utawala wa Kiislamu ni shani ya Mwenyezi Mungu, ambayo ikifuatwa inawahakikishia waja wake saada na fanaka ya duniani na akhera ya kiwango cha juu kabisa na ina uwezo wa kuufuta udhalimu, unyang’anyi, ufisadi na uonevu na kuwafikisha watu kwenye ukamilifu wanaohitajia.”

Kwa hiyo ikiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unaofuata dira ya Mapinduzi ya Kiislamu, utaendelea kushikamana na njia sahihi ya Uislamu wa asili na kuwafanya watu waendelee kuwa na moyo wa kuulinda Uislamu na thamani za Kiislamu, hakuna nguvu yoyote itakayoweza kuuzuia usipige hatua kuelekea malengo yake matukufu ya kumjenga mwanadamu.

Kwa hakika ni nguvu na uwezo wa Mwenyezi Mungu unaozielekeza nyoyo kwenye uongofu na kuwasemeza watu kwa lugha ya fitra na maumbile yao; kama ilivyo katika aya ya 63 ya Suratul Anfal, ambapo Mola aliyetukuka anasema, kuunganika kwa nyoyo za waja wake kiupendo kunatokana na Yeye mwenyewe tu na kwamba laiti Bwana Mtume SAW angetumia utajiri wote wa duniani asingeliweza kulifanikisha jambo hilo. Aya hiyo inasema:

وَأَلَّفَ بَیْنَ قُلُوبِهِمْ لَوْ أَنْفَقْتَ مَا فِی الْأَرْضِ جَمِیعًا مَا أَلَّفْتَ بَیْنَ قُلُوبِهِمْ وَلَکِنَّ اللَّهَ أَلَّفَ بَیْنَهُمْ إِنَّهُ عَزِیزٌ حَکِیمٌ

Na akaziunga nyoyo zao. Na lau wewe ungeli toa vyote viliomo duniani usingeli weza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye waunganisha. Hakika Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima. 

Jambo jengine lililoyadumisha Mapinduzi ya Kiislamu ni kuwepo kwake kwa matakwa na irada ya watu wenyewe. Mapambano ya umma mkubwa ulioshikamana pamoja, na harakati yenye mpangilio na lengo maalumu ni mojawapo ya sifa za kipekee za Mapinduzi ya Kiislamu ambayo imeshuhudiwa kwa nadra katika historia.

Nukta muhimu inayopasa kuzingatiwa ni kwamba umoja na mshikamano huo wa watu ulihitaji mwongozo na kiongozi ili kuweza kuwa na tija; na siri ya ushindi wake ilikuwa ni kumfuata kiongozi mmoja tu ambaye alichokitamka yeye ndicho kilichosikilizwa na watu wote katika jamii. Ni kwa sababu ya umuhimu wa jambo hilo, ndipo katika aya ya 31 ya Suratu Aal Imran, Mwenyezi Mungu akawaambia watu wanaosema wanampenda Yeye ya kwamba, kama kweli mnampenda Allah basi mfuateni Mtume wake:

قُلْ إِنْ کُنْتُمْ تُحِبُّونَ اللَّهَ فَاتَّبِعُونِی یُحْبِبْکُمُ اللَّهُ وَیَغْفِرْ لَکُمْ ذُنُوبَکُمْ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَحِیمٌ

Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu.

Hapana shaka kuwa ukweli, uwazi, ushujaa, shakhsia iliyotukuka kielimu na kifiqhi pamoja na maisha ya kawaida kabisa aliyokuwa akiishi Imam Khomeini (MA) vilikuwa na taathira katika kuonyesha mfano wa kuigwa wa kiongozi. Kutokana na mwongozo wa kiongozi huyo mwenye hekima na busara, wananchi wenye mapenzi ya Mwenyezi Mungu katika Iran ya Kiislamu, walifanya muamala na Mola wao, na kwa imani waliyokuwa nayo kwa ahadi ya ushindi aliyowapa Mwenyezi Mungu, waliweza kufanya mapinduzi makubwa. Kwa hiyo utiifu kwa kiongozi, ni sababu nyingine ya kudumu na kubaki imara Mapinduzi ya Kiislamu.

Kwa dhati yake na kutokana na maumbile yake, mwanadamu ni kiumbe anayehitaji kuwa huru; na dini tukufu ya Uislamu inasisitiza kila mara juu ya kukataa Waislamu kudhibitiwa na kutawaliwa na makafiri; kama inavyoeleza sehemu ya mwisho ya aya ya 141 ya Suratu-Nisaa ya kwamba:

وَلَنْ یَجْعَلَ اللَّهُ لِلْکَافِرِینَ عَلَى الْمُؤْمِنِینَ سَبِیلًا

Na wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda Waumini. 

Moja ya misingi mikuu na malengo muhimu katika dini ya Uislamu ni kuhakikisha Waislamu na utawala wa Kiislamu wanabaki kuwa na nguvu, hadhi na nafasi ya juu. Kuwa na nguvu na sauti ya juu maadui ya kuwatawala Waislamu na ardhi za Waislamu hakukubaliki kwa namna yoyote ile; na si sahihi, bali ni marufuku kufanya miamala na mabadilishano na kuwa uhusiano wa aina yoyote ile utakaowafanya maadui na maajinabi wawe na satua ndani ya jamii za Kiislamu. Imam Khomeini (MA), ambaye alikuwa mfuasi wa kweli wa chuo cha fikra cha Uislamu, alikuwa katika kila hatua anayochukua, anafuata maelekezo ya aya hiyo, na akiitakidi kwamba, kulingana na kaida na msingi huo, haifai kuacha mwanya wowote utakaowawezesha maadui kudhibiti na kuzitawala jamii za Kiislamu.

Kwa hiyo kupambana na dhulma na uistikbari na kupigania uadilifu na kutetea wanaodhulumiwa ni sababu nyingine iliyoyadumisha Mapinduzi ya Kiislamu na harakati hiyo ya umma. Ni kama alivyotueleza Mwenyezi Mungu, Mola mwenye hekima kwamba, mapambano hayo matakatifu ndilo lengo la kutumwa Mitume na kuteremshwa vitabu vya mbinguni, kama isemavyo aya ya 25 ya Suratu-Hadid:

...لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَیِّنَاتِ وَأَنْزَلْنَا مَعَهُمُ الْکِتَابَ وَالْمِیزَانَ لِیَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ 

Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu…

Fikra ya kupiga vita dhulma, iliyomo ndani ya mfumo wa Kiislamu imepelekea kila mara mabeberu na waistikbari duniani kufanya kila aina ya vitimbi ili kukwamisha kusonga mbele mfumo huu usiweze kufikia malengo yake matukufu. Hata hivyo busara na uelewa umewawezesha wananchi wa Iran kuwatambua maadui zao na kupata ushindi dhidi yao. Kwa hiyo, kwa kupambana na uistikbari, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu umeweza kulinda nguvu na uwezo wake na kutoruhusu ushawishi na satua ya maajinabi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei anasema, miaka zaidi ya arubaini ya njama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, wakati mapinduzi yenyewe yanaendelea kupiga hatua mbele, ni ishara ya kushindwa Marekani kuisimamisha harakati ya taifa la Iran. Ayatullah Khamenei anafafanua zaidi: “Maadui wa Iran azizi, kwa miaka arubaini wametekeleza aina mbalimbali za mashinikizo ya kila upande; ya kisiasa, kiuchumi na kipropaganda dhidi ya taifa, lakini hata siku Jamhuri ya Kiislamu ilipokuwa ingali mwanagenzi, hawakuweza kuwa na uthubutu wa kufanya upuuzi wowote.”

Kwa kutamatisha mazungumzo yetu, nimalizie kwa kukukumbusha kwamba, tuliyoashiria katika mazungumzo yetu ni sababu zilizowezesha kudumu na kuendelea kupiga hatua mbele harakati isiyo na kifani katika historia ya kisiasa duniani, ambazo zimeyapambanua mapinduzi haya na mengine makubwa yaliyotokea ulimwenguni. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalifungua ukurasa mpya wa utambulisho wa kiutamaduni na kihistoria wa nchi hii na kutoa mwanga wa ustaarabu mpya uliojengwa juu ya misingi ya thamani na malengo matakatifu ya dini ya Uislamu. Mfumo ulioasisiwa kutokana na mapinduzi haya umesimama juu ya usuli na misingi ya Kiislamu ambayo chimbuko lake ni fitra na maumbile ya mwanadamu; haichakai kwa kupita wakati, bali inaendelea kuvutia vizazi vya kila zama…/