Adabu za kusema na kuzungumza na watu
(last modified Mon, 06 Dec 2021 13:24:28 GMT )
Dec 06, 2021 13:24 UTC
  • Adabu za kusema na kuzungumza na watu

Sisi sote tunaelewa kwamba, shakhsia na hali ya ndani ya nafsi ya wanadamu huwa na taathira ya moja kwa moja katika mwenendo wake na jinsi ya kusema na kuzungumza kwake na wanadamu wenzake.

Kwa msingi huo maneno mazuri ya mtu na jinsi anavyochunga adabu za kuzungumza na wenzake vinaweza kuonesha kiwango cha ustawi na kuchanua kwa shakhsia na hadhi yake (personality) na vilevile hali ya ndani ya nafsi ya msemaji au mzungumzaji. Wakati huo huo kukua na kuchanua kwa shakhsia na hadhi ya mtu huwa sababu ya kulinda na kuchunga maadili ya kijamii ikiwa ni pamoja na adabu za kusema na kuzungumza. Watu wenye shakhsia kubwa na maadili mema kamwe hawasemi jambo lisilooana na hadhi zao, hata pale wanapokuwa katika mazingira magumu na mabaya. Mtume wetu mtukufu, Muhammad Mwaminifu ametuusia tusicheke, kutembea na kuzungumza bila ya adabu pasipo mahala pale. Anasema:

  إِیَّاکَ أَنْ تَضْحَکَ مِنْ غَیْرِ عَجَبٍ أَوْ تَمْشِیَ وَ تَتَکَلَّمَ فِی غَیْرِ أَدَبٍ؛

"Jiepushe kucheka bila ya kuwepo kioja na sababu, na jiepushe kutembea na kusema bila ya adabu."

Adabu za kusema na kuzungumza na watu zimesisitizwa sana katika mafundisho ya Uislamu. Miongoni mwa adabu hizo ni kuanza maneno na mazungumzo kwa salamu na kuamkia unaozungumza nao. Hii ina maana kwamba, unapotaka kuanza mazungumzo unampa heshima na taadhima unayezungumza naye, na kuanza kuzungumza kwa kumtakia amani na baraka za Mwenyezi Mungu. Kuanza mazungumzo kwa salamu huwa na maana ya kuonesha upendo na mahaba kwa mtu unayezungumza naye, na kutayarisha hisia zake kwa ajili ya kusikiliza na kukubali unayoyasema. Mbinu hii ya kutayarisha nafsi ya mtu unayetaka kuzungumza naye kwa ajili ya kusikia na kukubali maneno yako kupitia njia ya kutoa salamu, ilitumiwa na Malaika wa Mwenyezi Mungu waliokuwa wakitumwa kwa Mitume wake, kama inavyoashiriwa katika aya ya 69 ya Suratu Hud inayosema:

وَلَقَدْ جَاءَتْ رُسُلُنَا إِبْرَاهِیمَ بِالْبُشْرَى قَالُواْ سَلامًا قَالَ سَلامٌ فَمَا لَبِثَ أَن جَاءَ بِعِجْلٍ حَنِیذٍ

Na wajumbe wetu walimjia Ibrahim kwa bishara njema, wakasema: Salama! Naye akasema: Salama! Hakukaa ila mara akaleta ndama wa kuchoma.

Vilevile Aya ya 52 ya Suratul Hijr inasema:

إِذْ دَخَلُواْ عَلَیْهِ فَقَالُواْ سَلامًا قَالَ إِنَّا مِنکُمْ وَجِلُونَ

Walipoingia kwake na wakasema: Salama! Yeye akasema: Hakika sisi tunakuogopeni.

 Taathira ya salamu kwa unaozungumza nao ni kubwa mno kiasi kwamba, Mtume Muhammad (saw) aliusiwa na Mola wake Jalali kutanguliza salamu na maamkizi mema wakati anapowasiliana na kuzungumza na watu.     

- Kuanza maneno na mazungumzo kwa jina la Mwenyezi Mungu ni suna na ada nyingine nzuri iliyotajwa katika Qur'ani Tukufu na iliyokuwa ikitumiwa na Mtume (saw) na Ahlubaiti wake watoharifu. Kutaja jina la Mwenyezi Mungu mwanzoni mwa mazungumzo, lakini kwa kutilia maanani mazingira ya zama na eneo husika, huzidisha thamani na hadhi ya mazungumzo na maneno yanayosemwa. Tumesema "mazingira ya zama na eneo husika" tukimaanisha kwamba, si lazima kutaja jina la Mwenyezi Mungu mwanzoni mwa mazungumzo ya kila siku ya kawaida baina ya watu.

- Nukta nyingine ya kuashiriwa katika adabu za mazungumzo ni kuchunga wastani na kiwango cha kuzungumza. Kuwa na kipimo katika kuzungumza humlinda mzungumzaji kutumbukia katika makosa au kuteleza ulimi; na kwa upande mwingine humfanya msikilizaji asichoshwe na maneno ya mzungumzaji. Imam Ali bin Abi Twalib (as) anasema: "Maneno mengi humtelezesha mwenye hikima, na kumchosha mwenye subira."

- Miongoni mwa mambo yasiyofaa katika kusema na kuzungumza na watu ni tabia ya kuteta na kusengenya, kwa maana ya kusema mabaya ya watu bila ya wao wenyewe kuwapo. Qur'ani Tukufu imepambana vikali dhidi ya tabia hiyo mbaya ya kijahilia ambayo ingali imeenea kwa wingi baina ya wanadamu. Kitabu hicho kitukufu kinakutaja kusengenya kuwa ni sawa na kula nyama ya maiti ya ndugu yako. Aya ya 12 ya Suratul Hujurat inasema:

وَلا تَجَسَّسُوا وَلا یَغْتَب بَّعْضُکُم بَعْضًا أَیُحِبُّ أَحَدُکُمْ أَن یَأْکُلَ لَحْمَ أَخِیهِ مَیْتًا فَکَرِهْتُمُوهُ وَاتَّقُوا اللَّهَ إِنَّ اللَّهَ تَوَّابٌ رَّحِیمٌ

Wala msifanye ujasusi wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi, je anapenda mmoja wenu kula nyama ya nduguye aliyekufa? Mnalichukia hilo. Na mcheni Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kukubali toba, Mrehemevu.

Chanzo cha kusengenya ni kujasisi na kuchokonoa chokonoa mambo ya watu wengine; kwa msingi huo, kwanza Qur'ani Tukufu inatukataza kujasisi na kupeleleza mambo ya ndani ya watu, kisha inaharamisha na kukataza kusengenya. Kufanya ujasusi kwa ajili ya kuweka wazi na kuanika aibu za watu wengine ni jambo baya sana ambalo pia huzusha hali ya kutoaminiana na kudhaniana vibaya baina ya watu katika jamii. Kwa msingi huo kujiepusha na tabia hiyo chafu kumesisitizwa sana katika mtindo wa maisha wa Kiislamu.

Katika adabu za Kiislamu, kila maneno yana sehemu na wakati wake. Mazungumzo na maneno mengi hayapaswi kusemwa katika baadhi ya maeneo. Ukweli huu unasisitizwa katika methali isemayo: "Mwana wa Adamu hujifunza kusema katika kipindi cha miaka miwili baada ya kuzaliwa, lakini huchukua miaka thalathini kujifunza jinsi na wakati unaofaa wa kusema." Tunapaswa kukubali kwamba, mtu anayezungumza wakati na mahala pasipofaa huwa mithili ya jogoo anayesahau kuwika alfajiri mapema na kuwakera watu kwa kuwika wakati usiofaa.

- Kueleweka kwa maneno yanayozungumzwa ni miongoni mwa adabu za kusema na kuzungumza. Msemaji anapaswa kueleza muradi wake kwa njia inayoeleweka na kufahamika kwa watu wanaolengwa. Vilevile msemaji anapaswa kuyapamba maneno yake na kuyasema kwa njia inayomvutia msikilizaji. Maneno kama hayo huwa na taathira kubwa zaidi na huzidisha hadhi na heshima ya mzungumzaji. Mzungumzaji mwenye ilimu lakini anayeshindwa kufikisha muradi na maana ya maneno yake kwa wasikilizaji, huwachosha na kuwatia uzembe na ugoigoi.

- Ulaini wa maneno na kujiepusha na maneno makali ni katika adabu za kusema na kuzungumza zilizosisitizwa katika mafundisho ya Kiislamu.  La kuvutia zaidi ni kuwa, mbinu hiyo ya kutumia maneno laini na mazuri inasisitizwa na dini ya Uislamu hata pale unapokuwa unazungumza na watu makatili, waovu na waasi wakubwa. Wakati Mwenyezi Mungu SW alipomtuma Nabii Mussa na ndugu yake, Harouna, kwa Firauni alimwambia:

فَقُولا لَهُ قَوْلا لَّیِّنًا لَّعَلَّهُ یَتَذَکَّرُ أَوْ یَخْشَى

Mwambieni maneno laini, huwenda akazingatia au akaongoka. (Twaha:44)

Katika upande mwingine wakati maneno yanapokuwa makali na marefu si tu kwamba huwa kielelezo cha ya utovu wa adabu, bali pia huudhi masikio ya wasikilizaji na kuwaelekeza upande mwingine. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Imam Ali bin Abi Twalib (as) anatuusia akisema: "Sizoesheni ndimi zenu kwa maneno laini na kutoa salamu ili mupate marafiki wengi na muwe na maadui wachache."