Kuwa karibu na Mwenyezi Mungu
(last modified Mon, 18 Apr 2022 09:58:13 GMT )
Apr 18, 2022 09:58 UTC
  • Kuwa karibu na Mwenyezi Mungu

Hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tuna furaka kukukaribisheni kusikiliza kipindi hiki maalumu ambacho tumekuandalieni kwa mnasaba wa kukaribia nyusiku tukufu na takatifu za Lailatul Qadr.

Katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao Mwenyezi Mungu ameufanya kuwa meza ya chakula kwa ajili ya waja ambao amewataja kuwa ni wageni wake ili wapate kunufaika na wingi wa rehema na maghfira yake, kuna usiku mmoja mtukufu ambao ni mithili ya rubi zenye thamani kubwa zinazong'ara kwenye usiku wenye kiza kikuu. Usiku wa Leilatul Qadr kama yanavyosema maandiko matakatifu ya Qur'ani ni usiku ulio bora kuliko miaka elfu moja. Huu ni usiku ambao kwa kwa mujibu wa Aya za Qur'ani Tukufu na riwaya za Kiislamu, ni moyo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ambapo Malaika pia huwa na hamu kubwa ya kunufaika na utukufu wake. Katika usiku huu na kwenye karamu kubwa ambayo Mwenyezi Mungu huwa amewaandalia waja wake, Malaika pia huteremka ardhini kwa makundi kutoka mbinguni ili nao wapate kunufaika na minong'ono na dua za dhati za waja ambao huwa wanamwomba Muumba wao katika usiku huo mtukufu, awasamehe madhambi, awatimizie haja zao na kuwakinga na mabalaa. Kisha Malaika hao hurejea kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kumuwasilishia machozi na toba ambazo waja huwa wameomba katika usiku mtukufu wa Lailatul Qadr.

Katika usiku huu, sauti husikika ikisema: 'Enyi waja wa Mwenyezi Mungu! Ziondoeni nyoyo zenu kutoka kwenye minyororo ya matamanio ya shetani na kuzielekeza kwa Mwenyzi Mungu mwenye huruma na ambaye anasubiri kupokea toba zenu. 'Ni kana kwamba katika usiku wa Lailatul Qadr njia huwa ni rahisi kwa ajili ya waja kuelekea kwenye Pepo, njia ambayo hurahisika zaidi kupitia dua, kesha na toba ya dhati ya waumini.

Usiku wa Lailatul Qadr kama tulivyotangulia kusema umetajwa kuwa ni moyo wa Ramadhani.

Imam Swadiq (as) anasema: "Inafahamika kutokana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Qur'ani) kwamba idadi ya miezi katika mwaka mbele ya Mwenyezi Mungu ni 12 na mwezi bora zaidi kati ya miezi hiyo ni mwezi wa Ramadhani ambao moyo wake ni Leilatul Qadr."

Kwa mujibu wa riwaya za Kiislamu, Lailatul Qadr inaangukia katika moja ya nyusiku tukufu za tarehe 19, 21 na sana sana katika usiku wa kuamkia tarehe 23 za mwezi wa Ramadhani.

Inatosha kutambua kuwa moja ya utukufu wa usiku huu ni kwamba kitabu kitakatifu cha Qur'ani na ambacho ni kitabu jumuishi zaidi, kilichokamilika zaidi na chenye kudumu zaidi kati ya vitabu vyote vya mbinguni, kiliteremka mara moja kwenye moyo wa mtukufu Mtume (saw) katika usiku huu mtakatifu. Ukweli huu unabinishwa wazi na Qur'ani yenyewe ambayo inasema: "Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani."

Inasema katika Aya nyingine ambayo ni ya 3 ya Surat Dukhan: "Hakika tumekiteremsha katika usiku uliobarikiwa." Kusudio la usiku huo uliojaa baraka ni Lailatul Qadr.

Inaonekana kuwa kuna siri kubwa kati ya Ramadhani na Qur'ani na Lailatul Qadr na Qur'ani. Kitabu kitakatifu cha Qur'ani ni kitabu chenye thamani kubwa zaidi na kilicho na mpangilio bora na madhubuti zaidi wa kumdhaminia mwanadamu saada na ukamilifu wa kibinadamu. Pamoja na hayo, ni wazi kuwa iwapo mwanadamu hatakuwa na mawasiliano mazuri na sahihi na kitabu hiki kitakatifu, hawezi kunufaika nacho vizuri.

Katika sifa na fadhila za usiku wa Lailatul Qadr ni kwamba thamani yake ni bora kuliko ya miezi elfu moja. Suala hilo limeashiriwa wazi katika Qur'ani yenyewe ambayo inasema katika Surat al-Qadr: "Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu." Hii ina maana kwamba thamani kubwa ya ibada, amali na dua inapatikana katika usiku wa Lailatul Qadr. Kwa msingi huo mja anapasa kufahamu na kufanya juhudi za kunufaika kwa njia bora zaidi na fursa inayojitokeza katika usiku huu mtukufu na wenye thamani kubwa, kwa ajili ya kupata radhi za Muumba wake, fursa ambayo hutokea mara moja tu kwa mwaka.

Je, wako wapi waja wenye majuto? Wako wapi wanaotafuta toba? Wako wapi wanaomtafuta Mwenyzi Mungu na ambao wamefika ukingoni na wala hawana njia nyingine ya kujinusuru? Huu ni usiku wa Lailatul Qadr ambamo ndani yake milango yote ya rehema ya Mwenyezi Mungu imefunguliwa kwa ajili ya waja wake wakosefu na watenda dhambi walio na nia njema ya kutubia madhambi zao na kurejea kwenye njia sahihi ya kutii amri na makatazo ya Muumba wao. Katika usiku huu, Mwenyezi Mungu amefungua wazi mikono yake kuliko wakati mwingine wwote, kwa ajili ya kuwapokea, na anasubiri wafike mbele yake ili wapate kunufaika na chemichemi za usiku wa Lailatul Qadr katika kusafishia kutu za madhambi yaliyonasa kwenye nyoyo zao na vilevile kufungua minyororo ya dhambi kutoka kwenye miguu ya nyoyo zao na hivyo kuweza kutembea kwenye mabustani safi na ya kuvutia ya maghfira ya Mwenyezi Mungu.

Kuomba toba, kumwaga machozi, kukumbuka madhambi na kumuomba Mwenyezi Mungu akusamehe madhambi yako katika usiku huu mtukufu ndiyo njia ya wongofu. Riwaya pia zinasisitiza kwamba kuna fursa nzuri ya kusamehewa madhambi katika usiku huu kuliko nyusiku na siku nyingine zote za mwaka. Mtume Mtukufu (saw) anasema: "Kila mja anayekesha akifanya ibada usiku wa Lailatul Qadr huku akiwa na imani ya kupata thawabu za Mwenyezi Mungu, madhambi yake yaliyopita husamehewa."

Inasemekana kuwa Nabii Musa (as) alimwambia Mwenyezi Mungu: "Ewe Mwenyezi Mungu! Ninataka kuwa karibu nawe. Mungu akamjibu: Hunikaribia yule anayekuwa macho usiku wa Lailatul Qadr. Akasema tena: Ewe Mwenyezi Mungu! Ninataka kupata rehema zako. Akamjibu: Rehema zangu huzipata yule anayewarehemu masikini katika usiku wa Lailatul Qadr. Akasema: Ewe Mwenyezi Mungu! Ninakuomba kibali (idhini) cha kupita kwa mafanikio kwenye njia nyembamba ya Siraat. Akamjibu: Atakipata kibali hicho yule anayetoa sadaka katika usiku wa Qadr. Nabii Musa (as) akasema: Eeh Mwenyezi Mungu! Ninakuomba miti ya Peponi na matunda yake. Akamjibu Mwenyezi Mungu: Ataipata mja ambaye anafanya tasbihi katika usiku wa Qadr. Akasema Nabii Musa (as): Eeh Mwenyezi Mungu! Niepushe na Jahannam. Mwenyezi Mungu akamjibu: Hilo atalipata yule anayefanya istighfar katika usiku wa Qadar. Nabii Musa (as) akasema tena: Ewe Mwenyezi Mungu! Ninataka kupata radhi zako. Mwenyezi Mungu akamjibu: Radhi zangu atazipata yule mja anayeswali rakaa mbili katika usiku wa Qadr."


Usiku wa Lailatul Qadr umearifishwa kwa namna ambayo mbali na utukufu wake usio na mwisho, unahesabiwa pia kuwa ni usiku ambao ndani yake Mwenyezi Mungu huainisha na kuwakadiria wanadamu, wawe ni Waislamu au wasiokuwa Waislamu, masuala yao katika kipindi cha mwaka mzima. Suala hilo linabainishwa wazi katika Aya za 3 na 4 za Surat as-Dukhan ambazo zinasema: 'Hakika tumekiteremsha katika usiku ulio barikiwa. Hakika Sisi ni waonyaji. Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima.'

Yaani katika usiku huu uliojaa utukufu, masuala yote ya shari na heri yanayowahusu wanadamu, ikiwa ni pamoja na kuzaliwa, kifo, riziki, hija, ibada, dhambi na kwa ufupi kila tukio linalotokea katika kipindi chote cha mwaka kuhusiana na matendo ya mja huainishwa na Mwenyezi Mungu katika usiku huu mtukufu. Takdiri ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake pia hutimia kwa mujibu wa ustahiki, uwezo, imani, takwa na usafi wa nia zao. Kwa maana kwamba humukadiria mambo kwa mujibu wa uwezo na ustahiki wake na juhudi anazofanya  katika kuandaa mazingira ya kukadiriwa mambo na Muumba wake.

Kuna ibada na amali nyingi zilizojaa nuru na fadhila ambazo zinapaswa kutekelezwa kwenye usiku huu mtukufu na ambazo zimepokelewa na kuusiwa na Maimamu watoharifu (as). Baadhi ya amali zinahusiana na nyusiku zote tatu za Qadr ilihali nyingine ni maalumu kwa kila moja ya nyusiku hizo. Amali za pamoja zinazopaswa kutekelezwa katika nyusiku hizo ni pamoja na kuoga, kukesha (kuwa macho hadi wakati wa adhana ya alfajiri), rakaa mbili za swala ( ambapo katika kila rakaa baada ya kusoma Surat al-Hamd, unasoma Surat Tauheed mara saba na baada ya kukamilisha swala, unasoma; اَسْتَغْفِرُ اللّهَ وَاَتُوبُ اِلَیْهِ Astaghfirullah wa Atubu Ileih mara 70). Mtume Mtukufu (saw) amepokelewa akisema kuwa mtu anayeswali swala hii, huwa hanyanyuki kutoka sehemu aliyotekelezea swala hiyo ila Mwenyezi Mungu humsamehe yeye, baba na mama yake dhambi zao.

Kusoma dua ya Jaushan Kabir, Iftitaah, kuomba toba, kusoma Qur'ani, Ziara ya Imam Hussein (as) na dua ya Faraj ya Imam wa Zama (af) na kuweka Qur'ani kichwani ni baadhi ya amali nyingine ambazo zimeusiwa kutekelezwa katika usiku huu wa Lailatul Qadr, uliojaa nuru na utukufu.

Allama Mahlisi anaandika katika kitabu cha Bihar kwamba: "Amali bora zaidi za kutekelezwa katika nyusiku hizi ni kuomba toba na dua kwa ajili ya kukidhiwa haja zako za humu duniani na Akhera na vile vile za baba na mama yako, jamaa, ndugu na dada zako katika imani, wawe wangali wako hai au wameaga dunia, na kusoma dhikri pamoja na kumswalia Mtume Mtukufu (as) na Aali zake (as) kadiri utakavyoweza."

Wassalaam Alaykum.......