Oct 15, 2022 11:57 UTC
  • Tafakuri katika matukio ya hivi karibuni nchini Iran (nafasi ya vijana katika ushindi na kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu)

Matukio na machafuko ya hivi karibuni katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yamewapa maadui wa Iran fursa ya kuzidisha hujuma za kipropaganda na kisiasa na kutoa tathmini za kupotosha na kupindua hakika na ukweli wa mambo.

Katika kipindi chetu hiki cha kwanza kwenye mfululizo huu unaojadili kadhia hiyo tutazungumzia nafasi ya vijana katika ushindi na kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kutilia maanani machafuko ya hivi karibuni na vita vya kisaikolojia na vya vyombo vya habari vya Marekani, washirika wake wa Ulaya na baadhi ya nchi za Kiarabu katika eneo la Ghuba ya Uajemi kwa ajili ya kuvuruga usalama nchini Iran.  

Kama tulivyosema punde kidogo, matukio ya wiki chache zilizopita nchini Iran yameipa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya fursa ya kufanya hujuma zaidi za kipropaganda na kisiasa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Kama kawaida, maadui wa Iran wa kikanda na nje ya kanda hii walifanya tathmini ya haraka na ya kijuu juu tu ya matukio ya hivi karibuni na kuwachochea baadhi ya vijana ambao hawaridhishwi na mapungufu na baadhi ya sera za serikali. Maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamekuwa wakitumia nyenzo, fursa na majukwaa yote kuishambulia Iran katika kipindi cha zaidi ya miongo minne ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Marekani na waitifaki wake wa Ulaya na wa kikanda wamekuwa katika mzozo na mivutano ya mara kwa mara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Njama na majaribio ya kuupindua mfumo wa wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu imekuwa sera ya kudumu ya Marekani na baadhi ya washirika wake wa Ulaya. Nyayo na mkono wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya hususan Uingereza na baadhi ya nchi za Kiarabu, vinaweza kuonekana katika kipindi chote cha miaka 44 ya uhai wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika migogoro na machafuko yote na hujuma za kigaidi na vilevile katika uvamizi wa Saddam Hussein dhidi ya ardhi ya Iran mwezi Septemba 1980 na kuanzisha vita vya miaka minane. Wakati serikali za Ulaya zilipotambua kwamba hazingeweza kufikia malengo yao ya kuyaangusha Mapinduzi ya Kiislamu kwa silaha za vikwazo vya kiuchumi, uvamizi wa kijeshi na mauaji ya takriban watu elfu 17 wa kawaida, waungaji mkono wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi shakhsia wa juu kabisa wa kisiasa, walianzisha vita vya kisaikolojia na vya vyombo vya habari ili kuibua migogoro nchini Iran kutokea kwa ndani. Suala hili linashuhudiwa kwa sasa ambapo parapanda za vyombo vya habari vya Magharibi vinaeneza uvumi vikidai Mapinduzi ya Kiislamu yamefikia mwisho!

Kwa vyovyote vile, maandamano na machafuko ya kupinga au kulalamikia utendaji na sera za serikali vinashuhudiwa katika karibu nchi zote. Hata hivyo kuna nchi chache sana kama Iran ambako serikali za Marekani na nchi za Ulaya huingilia kati na kuendeleza au kuchochea machafuko kwa kutumia vita na hujuma za vyombo vya habari, kueneza uvumi na propaganda chafu. Kiasi kwamba, matukio ya Iran yamefanywa habari ya kwanza duniani, katika kipindi hichohicho ambacho kilishuhudia mauaji ya kutisha ya wanawake na watoto nchini Afghanistan, lakini suala hilo halikuzingatiwa wala kupewa umuhimu wa aina yoyote katika vyombo vya habari vya nchi za Magharibi.

Brian Hook, kkuu wa kundi la hatua dhidi ya Iran katik Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, amekiri kwamba Washington imehusika katika machafuko ya karibuni nchini Iran

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu amesema katika hotuba yake kuhusu matukio ya wiki za hivi karibuni nchini Iran kwamba: "Machafuko mengi yanatukia duniani. Tazama, huko Ulaya, huko Ufaransa, kila baada ya muda ghasia kubwa huibuka katika mitaa ya Paris. Nauliza swali kwamba je, mumekwishaona au kusikia Rais wa Marekani na Baraza la Wawakilishi la nchi hiyo (Congress) wakiwaunga mkono watu wanaofanya ghasia huko Ufaransa na barani Ulaya? Je, imewahi kushuhudiwa wakituma ujumbe wa kuwaambia watu anaofanya ghasia kwamba tuko pamoja nanyi? Je, mumewahi kuona vyombo vya habari na mawasiliano ya umma vya mabepari wa Marekani, serikali ya Washington, vibaraka wao kama baadhi ya nchi za kanda hii ya Mmagharibi mwa Asia, ikiwemo serikali ya Saudi Arabia, vikijitosa kwenye uwanja ya kuwaunga mkono watu wanaofanya ghasia na fujo? Je jambo kama hili limewahi kushuhudiwa? Je, mumewahi kuona wakitangaza kuwa tutawapa watu wanaofanya fujo na ghasia zana za kiufundi na kiteknolojia za intaneti ili waweze kuwasiliana na kufanya kazi zao kwa urahisi? Je, jambo kama hilo limewahi kushuhudiwa popote duniani, katika nchi yoyote? Lakini limetokea hapa nchini; Sio mara moja, sio mara mbili, mara nyingi." 

Maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu wanawekeza zaidi katika kizazi cha vijana na chenye nguvu cha Iran. Tabaka la vijana katika jamii yoyote linaweza kuwa na nafasi na mchango muhimu katika mustakabali wa jamii na nchi hiyo kutokana na uwezo, nguvu na vipaji vyao vingi, na vijana katika jamii yoyote ile wanahesabiwa kuwa ni rasilimali kubwa wa jamii husika, ambayo inaweza kutayarisha mazingira bora zaidi ya ustawi na maendeleo ya jamii katika nyanja mbalimbali za sayansi, utamaduni, uchumi, siasa, sanaa, michezo n.k. 

Nchini Iran, kizazi cha vijana kimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi, na tumeshuhudia mahudhurio makubwa ya vijana katika nyanja mbalimbali tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, sira ya maisha ya kivitendo ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) na Imam Ali bin Abi Twalib (as) inaonyesha kwamba vijana kama kizazi chenye taathira kubwa, nguvu na chipukizi, hawapaswi kusahaulika na kupuuzwa, na wao ndio waliokuwa wakilengwa zaidi kwa wahyi na ujumbe wa Uislamu kuliko tabaka lingine la jamii. Ni kwa msaada wa vijana ambapo dini iliingia katika jamii na kuathiri hatima ya taifa la Iran. Kiongozi mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Ruhullah Khomeini (ra), alitambua vyema umuhimu wa rasilimali hiyo kubwa na akaitumia vyema katika kuhudumia Uislamu na kupindua utawala wa kifalme nchini Iran, na kamwe hakuacha kutumia kila fursa kwa ajili ya kuendeleza na kukuza vipaji vya kiroho na kifikra vya tabaka la vijana. Mhandisi huyo wa Mapinduzi ya Kiislamu alitangaza tangu mwanzoni kabisa mwa harakati ya Kiislamu mwaka 1963 kwamba atakabiliana na maadui wa dini ya Mwenyezi Mungu kwa kutegemea uwezo wa Allah SW na msaada wa vijana. Imam Khomeini alinyanyua juu bendera ya Iran huru na yenye nguvu wakati wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na baada yake na wakati wa vita vya kulazimishwa vya miaka 8 vilivyoanzishwa na utawala wa Saddam katika miaka ya 1980 kwa kutumia na kuwahamasisha vijana na kwa kutegemea ushiriki wao mkubwa. 

Imam Khomeini na vijana

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyaona matakwa ya kupata heshima ya vijana wa Kiirani kuwa ni jambo lisilopingika, na alizingatia na kulipa umuhimu suala la kuendeleza kaulimbiu mbili muhimu yaani "uhuru" na "kujitawala" katika hatua za vijana. Kwa msingi huo, wananchi wa Iran, hususan tabaka la vijana, hawakuacha juhudi za kutimiza nara na kaulimbiu hizo muhimu katika jitihada zao za kuimarisha Jamhuri ya Kiislamu, na hawakuwa tayari kuacha harakati hiyo kwa gharama yoyote ile. Imam Khomeini alitambua mchango mkubwa na muhimu wa vijana katika ushindi wa Mapinduzi ya Kislamu na anasema katika mojawapo ya hotuba zake katika uwanja huo kwamba: "Ni hima yenu kubwa nyinyi vijana ndiyo iliyotuwezesha kupata ushindi na kung'oa kwa kiasi fulani mizizi ya ufisadi nchini Iran. Ni kujitolea kwenye nyinyi vijana ndiko kulikouokoa Uislamu mbele ya hujuma za ajnabi na maadui, na nyinyi mtakaoweza kuuokoa Uislamu kutoka kwenye mikono ya watawala wasaliti kwa umoja na nguvu yenu."  

Vijana pia ndio waliokua mstari wa mbele katika vita vya kukabiliana na uvamizi Saddam Hussein dhidi ya Iran. Katika kipindi hicho cha vita vijana walionesha hamasa kubwa na kuacha historia itakayokumbukwa kwa miaka mingi ijayo. Baada ya kumalizika vita hivyo vya miaka 8 pia, vijana wa Iran wakiwa na moyo huo huo wa kishujaa na hamasa kubwa, walipiga hatua za kustaajabisha katika medani za sayansi, uchumi na kadhalika kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Jamhuri ya Kiislamu. Iran ya Kiislamu imeweza kupata mafanikio makubwa kama elimu ya kuzalisha fueli ya vinu vya nishati ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya amani kwa kutumia vipawa na elimu ya vijana wake ambao aghlabu yao walikuwa katika muongo wao wa tatu. Kwa hivyo, utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani ziliweka ajenda ya mauaji ya wanasayansi wa nyuklia wa Iran ili kuzuia ustawi zaidi wa maarifa na teknolojia ya nyuklia hapa nchini. Ayatullah Ali Khamenei anasema, moja kati ya sababu za hatua za Marekani na maadui wa taifa la Iran za kuzusha migogoro na machafuko nchini Iran ni kutaka kuzuia ustawi na maendeleo ya nchi hii. Anasema: "Ninachofikiria mimi ni kwamba, wanaona nchi yetu inapiga hatua za maendeleo ya kupata nguvu katika pande zote, suala ambalo hawawezi kulistahamili. Wanaona kwamba, kwa baraka zake Allah, baadhi ya matatizo ya zamani yanatatuliwa. Ni kweli kwamba, nchi yetu ina matatizo mengi, na baadhi ya matatizo yapo kwa miaka mingi; hata hivyo kuna harakati kubwa ya kutatua na kuondoa matatizo yaliyopo. Wanashuhudia harakati ya maendeleo inayokwenda kwa kasi. Huu ni uhakika usiopingika. Kunashuhudiwa harakati ya maendeleo inayokwenda kwa kasi kubwa katika kila sekta hapa nchini. Wao pia wanashuhudia harakati hiyo na hawataki jambo hilo litimie. Wanaona viwanda vilivyokuwa vimedorora vikipata uhai mpya, wanaona harakati kubwa ya sayansi na elimu, wanashuhudia uzalishaji wa vifaa vya kisasa katika sekta za viwanda, wanaona kukifanyika kazi kubwa ambazo zitazima na kubatilisha vikwazo vyao ambavyo ndiyo silaha pekee ya adui kwa sasa. Wanaona haya yote hapa nchini na wameamua kuketi pamoja kuweka mikakati ya jinsi ya kusimamisha harakati hiyo." 

Kwa hivyo, inaonekana kuwa juhudi za maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kuanzisha machafuko ya hivi karibuni ili kutenganisha kizazi cha vijana na Jamhuri ya Kiislamu zimefeli na zitaendelea kufeli. Katika kipindi chetu kijacho tutatupitia jicho sehemu nyingine ya njama zilizofeli za maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika machafuko ya hivi karibuni hapa nchini. 

Tags