Rais Magufuli: Polisi ongezeni juhudi kiutendaji kumaliza ujambazi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10000-rais_magufuli_polisi_ongezeni_juhudi_kiutendaji_kumaliza_ujambazi
Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania amewataka polisi wa nchi hiyo kuongeza juhudi katika utendaji kazi wao ili kukabiliana na uhalifu nchini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 26, 2016 03:30 UTC
  • Rais Magufuli: Polisi ongezeni juhudi kiutendaji kumaliza ujambazi

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania amewataka polisi wa nchi hiyo kuongeza juhudi katika utendaji kazi wao ili kukabiliana na uhalifu nchini.

Rais Magufuli amesema, polisi ya nchi hiyo inatakiwa kuongeza juhudi zake bila kusubiri majambazi kufikia hatua ya kuwanyang’anya silaha katika vituo vyao au kuvamia nyumba, watu na kuwanyang’anya mali zao. Aidha, Rais Magufuli amesema, umefikia wakati polisi kusimama kidete na kutosita kukabiliana na majambazi kukiwemo kuwanyang’anya silaha zao kwa kutumia mbinu zao za medani. Ameongeza kuwa, wananchi wamechoshwa na wimbi la ujambazi uliokithiri nchini ambapo wamekuwa wakiibiwa mali zao kila uchao. Rais Magufuli alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua mpango wa usalama wa raia katika kuboresha utendaji kazi kwa kutumia mfumo wa (BRN) awamu ya pili utakaoanza kutekelezwa Julai Mosi mwaka huu jijini Dar es Salaam na kuenezwa nchi nzima baada ya miaka mitatu katika kupunguza uhalifu. Uzinduzi wa mpango huo ulihudhuriwa pia na Jakaya Kikwete rais mstaafu wa awamu ya Nne wa nchi hiyo. Rais Magufuli alisema na hapa ninamnukuu: “Naomba niwe mkweli na muwazi kwa sababu sitaki kuwa mnafiki kwani yapo mambo yalikuwa yakinikereketa na kuniudhi hasa pale unapoona jambazi anavamia kituo cha Polisi na kuua polisi kisha anaondoka na silaha au anakwenda kuiba mahali na ana silaha anaondoka hivi hivi, hili limekuwa linanipa wasiwasi." Mwisho wa kunukuu. Tanzania imekuwa ikishuhudia wimbi la ujambazi ambapo mbali na kupora, majambazi huwa wanafanya mauaji pia.