Mgogoro wa Mapinduzi ya Kijeshi nchini Niger
Mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini Niger umeendelea kutawala habari za eneo la Magharibi mwa Afrika.
Mgogoro huo sasa unaonekana kuingia katika awamu nyingine baada ya wawakilishi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, (ECOWAS) kuondoka Niamey bila kukutana na kiongozi wa mapinduzi ya nchi hiyo, Jenerali Abdourahmane Tchiani.
Ripoti kutoka mji mkuu wa Niger, Niamey, zinasema kwamba ujumbe wa ECOWAS ulikutana na wawakilishi kadhaa wa baraza tawala la kijeshi, lakini haukukutana na kiongozi wa mapinduzi ya Niger, Jenerali Abdourahmane Tchiani, na sababu za suala hilo bado hazijafahamika.
Awali jumuiya ya ECOWAS ilikuwa imetishia kuwa itatumia nguvu za kijeshi dhidi ya watawala wapya wa Niamey iwapo hawatamwachia huru rais wa zamani wa Niger, Mohamed Bazoum na kurejesha utawala wa katiba.
Baada ya kushika madaraka ya nchi, Jenerali Abdourahmane Tchiani alisema kuwa lengo la mapinduzi hayo ni kukata mikono ya Wafaransa katika nchi hiyo na pia kuzidisha hali ya usalama. Sambamba na hayo wananchi wa Niger wanaendelea kufanya maandamano ya kuunga mkono mapinduzi yaliyofanywa na Kikosi cha Gadi ya Rais wakipiga nara za "Mauti kwa Ufaransa."

Katika upande mwingine nchi za Magharibi, hususan Ufaransa, bado zinajaribu kuweka shinikizo kwa serikali ya mapinduzi ya Niger na kuilazimisha kumwachilia huru na kumrejesha madarakani rais aliyependuliwa wa nchi hiyo, Mohammad Bazoum. Katika muktadha huu, Muhammad Bazoum anayeshikiliwa na wanajeshi, ameliambia gazeti la Washington Post kwamba: Ikiwa mapinduzi hayo yatafanikiwa, yatakuwa na madhara kwa nchi yangu, eneo na dunia nzima.
Bazoum ni mshirika mkubwa wa nchi za Magharibi, hasa Ufaransa, na anadhamini sehemu kubwa ya mahitaji ya Ufaransa, hususan madini ya uranium yanayohitajika katika vinu vya nyuklia vya nchi hiyo; kwa sababu hiyo sasa Ufaransa, inataka "kulipa fadhili" kwa mshirika wake huyo mkubwa na inazungumzia uwezekano wa kuingilia kijeshi na kuishambulia nchi hiyo ya Afrika. Wanajeshi waliofanya mapinduzi wamesema watajibu mashambulizi yoyote ya kijeshi kutoka nje ya nchi. Nchi jirani za Mali, Burkina Faso na Guinea Conakry zimeunga mkono mapinduzi ya kijeshi ya Niger na kusema kuwa, mashambulizi yoyote dhidi ya nchi hiyo ni tishio la tangazo la vita dhidi ya nchi hizo.
Wakati huo huo baadhi ya nchi za Ulaya pia zimepinga suala la kuishambulia kijeshi Niger kwa kisingizio cha mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini humo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia amezionya nchi za Magharibi zisithubutu kuingilia kijeshi nchini Niger.
Akizungumzia ripoti za uwezekano wa Ufaransa kuishambulia nchi ya Niger, Antonio Tajani, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Italia, ameonya kwamba nchi za Magharibi zinapaswa kujiepusha kuingilia kijeshi nchini Niger kwa sababu suala hilo litaonekana kama wimbi jipya la ukoloni mamboleo wa nchi za Magharibi.
Hali ya mambo nchini Niger inaonekana kuwa mbaya zaidi licha ya utajiri mkubwa wa maliasili na rasilimali za nchi hiyo. Niger ambayo ilikuwa koloni la Ufaransa kwa kipindi cha karibu karne nzima, inasumbuliwa na umaskini mkubwa na inashika nafasi ya mwisho kati ya nchi 189 katika mtazamo wa vigezo vya ustawi wa binadamu. Zaidi ya nusu ya watu wa nchi hiyo wanaishi chini ya mstari wa umaskini na karibu nusu ya watoto wenye umri wa kwenda shule hawaendi shuleni. Vilevile kuwepo nchi hiyo katika ukanda wa harakati za kigaidi kama Boko Haram, al Qaida na kadhalika na makundi ya wanamgambo yanayofanya harakati katika eneo la Sahel Afrika, kunazidisha matatizo ya kisiasa na kiusalama ya nchi hiyo.
Niger ni nchi ya tatu ya ukanda wa Maghaibi mwa Afrika baada ya Mali na Burkina Faso, iliyokumbwa na mapinduzi ya kijeshi. Nchi zote hizo zimekuwa chini ya ukoloni mamboleo wa Ufaransa kwa miaka mingi, na vikosi vya majeshi ya serikali ya Paris vimekuwa katika nchi hizo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Hata hivyo kuwepo kwa majeshi hayo hakukusaidia lolote zaidi ya kuzidisha hali mbaya na ukosefu wa amani. Hii ni licha ya kwamba, Ufaransa inahesabiwa kuwa mshirika mkubwa wa kibiashara wa nchi hizo hasa katika kuchimba madini ya uranium.
Katika muktadhaa huu, Rais wa Burkina Faso, Ibrahim Traore anasema: Kwa nini Afrika ambayo inasifika kwa kuwa na utajiri wa maliasili na rasilimali nyingi inaendelea kuwa eneo maskini zaidi duniani? Tunauliza maswali kama haya lakini hatupati jibu? Nchi za Afrika zimeteseka sana na ukatili wa kutisha wa ukoloni na ubeberu ambao unaweza kuitwa kuwa ni utumwa mamboleo.
Inaonekana kuwa, mapinduzi ya sasa nchini Niger ni mwendelezo wa harakati za kujikomboa kutoka kwenye ukoloni mamboleo wa nchi za Magharibi kama Ufaransa. Watu wa nchi za ukanda wa Sahel Afrika wanataka demokrasia ya kweli, kuboreshwa uchumi na hali zao za kimaisha na kiusalama, na ndiyo maana wameunga mkono mapinduzi ya kijeshi yanayoziondoa madarakani serikali na tawala tegemezi kwa nchi za kikoloni.