Mali yaonya kuhusu 'maafa' ECOWAS ikiishambulia kijeshi Niger
Uingiliaji wa kijeshi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) nchini Niger kwa ajili ya kumrejesha madarakani Rais Mohamed Bazoum aliyepinduliwa Julai 26 unaweza kuibua maafa na maangamivu makubwa.
Indhari hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop ambaye amesisitiza kuwa, "Vikosi vya kieneo havijatumika dhidi ya nchi nyingine ili tuweze kukadiria matokeo, itakuwa maafa."
Amesema haelewi ni kwa nini ECOWAS inataka kutuma majeshi Niger eti kurejesha utawala uliopinduliwa, lakini imeshindwa kutuma vikosi katika nchi za eneo la Sahel vikapige jeki vita dhidi ya magenge ya kigaidi.
Matamshi ya mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Mali yametolewa huku viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi wakiitisha mkutano mwingine wa dharura Alkhamisi ijayo kushughulikia mzozo huo wa kisiasa nchini Niger, baada ya viongozi wa kijeshi kupuuza makataa ya kuachia madaraka.
ECOWAS iliwataka wanajeshi waliompindua Mohamed Bazoum kumrejesha madarakani rais huyo wa Niger ndani ya siku saba - kipindi ambacho kilimalizika Jumapili - au kukabiliwa na uingiliaji kati wa kijeshi ili kurejesha 'utawala wa kikatiba'.
Nchi za Afrika Magharibi zimegawanyika kuhusu suala hilo la kuishambulia kijeshi Niger ili kumrejesha madarakani Rais Bazoum ambaye anaendelea kuzuiliwa na wanajeshi wafanya mapinduzi.
Katika hatua nyingine, baraza la mpito la kijeshi la Niger limemteua mchumi Ali Mahamane Lamine Zeine kuwa Waziri Mkuu wa muda wa nchi hiyo.
Zeine ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo Afrika nchini Chad, amewahi kuwa Waziri wa Fedha wa Niger wakati wa utawala wa Mamadou Tandja, kuanzia mwaka 1999 hadi 2010.