Baraza la kijeshi Niger lakataa mazungumzo na AU, ECOWAS na UN
Serikali ya mpito ya Niger inayoongozwa na wanajeshi waliofanya mapinduzi mnamo Julai 26 imepuuzilia mbali mwito wa kufanya mazungumzo uliotolewa na Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na Umoja wa Matafa (UN).
AU hapo jana ilitaka kutuma timu yenye wajumbe kutoka jumuiya hiyo, ECOWAS na UN kwenda Niger kufanya mazungumzo na wanajeshi, kwa lengo la kumrejesha madarakani Rais Mohamed Bazoum aliyepinduliwa, lakini wafanya mapinduzi hao wakawanyima kibali na kukata kufungua anga ya nchi hiyo.
Wanajeshi hao wa Niger wanasema hawatubali kuburuzwa na kushinikizwa na Wamagharibi wakiongozwa na Marekani na Ufaransa, wanaowataka warejee kambini na wamrejeshe madarakani Rais Bazoum.
Kaimu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani, Victoria Nuland juzi Jumatatu alienda Niamey, lakini hakuruhusiwa pia kuonana na kiongozi wa mapinduzi, Abdourahamane Tchiani wala Rais Bazoum anayezuiliwa na wanajeshi wafanya mapinduzi. Hata hivyo Jumatatu hiyo Tchiani alikutana na kufanya mazungumzo ujumbe wa pamoja kutoka nchi jirani za Mali na Burkina Faso.
Haya yanajiri huku viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi wakiitisha mkutano mwingine wa dharura Alkhamisi ya kesho kushughulikia mzozo huo wa kisiasa nchini Niger, baada ya viongozi wa kijeshi kupuuza makataa ya kuachia madaraka.
ECOWAS iliwataka wanajeshi waliompindua Mohamed Bazoum kumrejesha madarakani rais huyo wa Niger ndani ya siku saba - kipindi ambacho kilimalizika Jumapili iliyopita- au kukabiliwa na uingiliaji kati wa kijeshi ili kurejesha 'utawala wa kikatiba'.
Nchi za Afrika Magharibi zimegawanyika kuhusu suala hilo la kuishambulia kijeshi Niger ili kumrejesha madarakani Rais Bazoum ambaye anaendelea kuzuiliwa na wanajeshi wafanya mapinduzi.