Askari kadhaa wa Somalia wauawa katika mripuko wa bomu Mogadishu
Wanajeshi kadhaa wa Somalia wamepoteza maisha baada ya gari lililokuwa limewabeba kukanyaga bomu katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.
Radio Shabelle imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, tukio hilo lilitokea jana Alkhamisi baada ya gari lililokuwa limebeba wanajeshi wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kupita juu bomu la kutegwa ardhini katika barabara ya Darussalam.
Idhaa hiyo imenukuu duru za kiusalama zikisema kuwa, askari wote sita wa Jeshi la Taifa la Somalia waliokuwa kwenye gari hilo wamepoteza maisha.
Shambulio hilo la jana limejiri siku moja baada ya raia sita kupoteza maisha baada ya gari lao kukanyaga bomu na kuripuka katika eneo lililoko baina ya wilaya za Marka na Qoryooley.
Mohamed Ibrahim, Gavana wa jimbo la Lower Shabelle ameliambia shirika rasmi la habari la Somalia kwamba, waliolengwa kwenye hujuma hiyo ya Jumatano walikuwa wafanyabiashara.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab limekuwa likitega mabomu katika barabara muhimu za nchi hiyo ili kuua raia na maafisa usalama wa nchi hiyo.
Hii ni katika hali ambayo, makumi ya wanachama wa kundi hilo la kigaidi la Somalia wameangamizwa wakiwemo makamanda wao wa ngazi za juu ndani ya siku chache zilizopita katika operesheni za vikosi vya Somalia.
Jeshi la Somalia limetangaza kuwa, wanachama wasiopungua 25 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wameuawa katika operesheni ya jeshi hilo katika mji wa Hiran Jumatano ya juzi.