Kusitisha serikali ya Mali utoaji visa kwa raia wa Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i101070-kusitisha_serikali_ya_mali_utoaji_visa_kwa_raia_wa_ufaransa
Mvutano kati ya nchi za ukanda wa Sahel ya Afrika na Ufaransa unazidi kuongezeka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 14, 2023 22:56 UTC
  • Kusitisha serikali ya Mali utoaji visa kwa raia wa Ufaransa

Mvutano kati ya nchi za ukanda wa Sahel ya Afrika na Ufaransa unazidi kuongezeka.

Kuhusiana na hilo, serikali ya Mali katika hatua ya kukabiliana na Ufaransa, imesitisha kutoa visa kwa raia wa taifa hilo la Ulaya wanaotaka kwenda Mali.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Mali imetangaza kuwa, imesimamisha utoaji wa visa kwa raia wa Ufaransa kwa muda usiojulikana. Hapo awali, serikali ya Ufaransa iliiweka Mali katika "eneo jekundu" kwa kisingizio cha mvutano wa kikanda.

Kufuatia mapinduzi ya Niger, kwa mara nyingine tena hisia dhidi ya Wafaransa zimeongezeka katika baadhi ya nchi za eneo la Sahel; kiasi kwamba huko Niger, wananchi wa nchi hiyo wameunga mkono wanajeshi waliofanya mapinduzi yaliyopelekea kuondolewa madarakani Rais Muhammad Bazoum muitifaki wa Ufaransa na Marekani.

Hii ni katika hali ambayo baadhi ya nchi za Afrika, wakiwemo baadhi ya wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) wamelaani mapinduzi ya Niger na kutangaza vita dhidi ya waliopanga mapinduzi hayo.

Katika fremu hiyo, maafisa wa Ufaransa pia wamekaribisha kwa mikono miwili uamuzi wa mataifa hayo kiasi kwamba, Amadou Abdelrahman, msemaji wa Baraza la Kijeshi la Niger, amesema kwamba, Ufaransa ilifanya mkutano na baadhi ya washirika wake wa ndani ili kuchunguza na kutathmini mchakato wa kuingilia kijeshi nchini Niger.

Hii ni hali ambayyo, Mali na Burkina Faso zilitangaza kwamba zitalitambua shambulio lolote dhidi ya Niger kama tangazo la vita dhidi yao na zitakabiliana nalo.

 

Sambamba na hayo, mazingira hayo yaameongeza uwezekano wa vita katika eneo hilo. Ukweli wa mambo ni kuwa, Niger inahesabiwa kuwa mmoja wa washirika wakuu wa Ufaransa, na hivi sasa inaonekana kuwa, maslahi ya taifa hilo la Ulaya yapo hatarini zaidi kuliko hapo awali. Ni kutokana na hilo, ndio maana, Ufaransa ilionyesha radiamali dhidi ya mataifa ambayo, hayakuunga mkono shambulio la kijeshi huko Niger ikiwemo Mali, na kuziweka katika orodha nyekundu.

Kabla ya hapo, nchini Mali na Burkina Faso, hisia dhidi ya Ufaransa zilisababisha nchi hizo kukata uhusiano wao wa kisiasa na Ufaransa.

Ukweli wa mambo ni kuwa, Ufaransa imekuwa na mahudhurio amilifu kwa makumi ya miongo katika mataifa ya Ukanda wa Sahel Afrika ikiwemo Mali na mataifa jirani kwa madai ya kusaidia kupambana na ugaidi na kupiga jeki juhudi za kurejesha usalama barani Afrika. Lakini ukweli wa mambo ni kuwa, Ufaransa imekuwa ikiendesha shughuli zake kwa mbinu ya ukoloni mpya katika eneo hilo.

Wanajeshi wa Ufaransa walikuweko katika mataifa ya Sahel Afrika hususan Mali katika fremu ya Operesheni ya "Barkhane" kwa madai ya kutoa msaada. Hata hivyo ripoti zinaonyesha kuwa, wanajeshi wa Ufaransa hawakuwa na mafanikio yoyote katika operesheni dhidi ya ugaidi na hata katika baadhi ya matukio waliwalenga kwa mashambulio raia wa nchi hiyo.

Kuhusiana hilo, Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati ya Afrika kilitangaza katika ripoti yake kwamba, kufuatia uingiliaji wa kigeni barani Afrika, idadi ya matukio ya vurugu yanayohusiana na vikundi vya kigaidi imeongezeka kwa asilimia 70 katika nchi za Sahel Afrika.

Assimi Goita Rais wa mpito wa Mali

 

Katika uga wa kiuchumi, moyo wa kikoloni wa Ufaransa umezifanya nchi hizo daima zizingatiwe daima na Ufaransa. Nchi hizo ambazo zina migodi yenye madini mengi ya urani na dhahabu na migodi mingineyo ni miongoni mwa wasambazaji wakuu wa mahitaji ya Ufaransa ikiwemo vinu vya nyuklia vya nchi hiyo.

Katika miaka ya hivi karibuni sera za Ufaransa barani Afrika zimekabiliwa na maandamano na malalamiko mengi kutoka kwa raia wa nchi mbalimbali za bara hilo. Kimsingi ni kuwa, kukua kwa mwamko na kutokea mageuzi ya kisiasa na kijiografia katika uga wa siasa za kimataifa, kumezifanya nchi za Afrika hususan za Ukanda wa Sahel Afrika zifanye juhudi za kujiondoa chini ukandamizaji na ubabe wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja wa Ufaransa.

Abd al-Rahman bin Shareit, mchambuzi wa masuala ya kisiasa sambamba na kubainisha kwamba, pamoja na kuwa makundi yote ya bara la Afrika yamechoshwa na sera ya Ufaransa, amesisitiza kuwa, sera hizo zimeegemezwa kwenye misingi ya utumiaji mabavu katika eneo katika eneo na kuwaweka madarakani viongozi wanaofanya kazi kwa ajili ya madhara kwa mataifa ya Afrika na kwa manufaa ya Paris.

Ufaransa imepoteza mshirika wake wa mwisho kwenye Ukanda wa Sahel Afrika pamoja na kuwa bado haijafahamika ni matukio gani yatatokea katika eneo hili. Lakini inaonekana wazi kuwa kuanzia sasa Ufaransa na nchi nyingine za kikoloni zitakabiliwa na vizingiti zaidi katika kusukuma mbele gurudumu la malengo yao katika eneo la nchi za Sahel.