Wanajeshi 17 wa Niger wauawa katika shambulizi la kigaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i101146-wanajeshi_17_wa_niger_wauawa_katika_shambulizi_la_kigaidi
Kwa akali wanajeshi 17 wa Niger wameuawa katika shambulizi la kuvizia linaloripotiwa kufanywa na magaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 16, 2023 23:44 UTC
  • Wanajeshi 17 wa Niger wauawa katika shambulizi la kigaidi

Kwa akali wanajeshi 17 wa Niger wameuawa katika shambulizi la kuvizia linaloripotiwa kufanywa na magaidi.

Wizara ya Ulinzi ya Niger ilisema hayo jana Jumatano na kuongeza kuwa, askari wa Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo walizingirwa na kushambuliwa na magaidi karibu na eneo la Koutougou, baina ya maeneo ya Boni na Torodi.

Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa, wanajeshi wengine 20 wamejeruhiwa kwenye hujuma hiyo ya Jumanne, sita miongoni mwao wakiwa katika hali mbaya. Habari zaidi zinasema kuwa, majeruhi hao wamehamishiwa Niamey, mji mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Wizara ya Ulinzi ya Niger imesema magaidi karibu 100 wameangamizwa katika operesheni ya kulipiza kisasi, mbali na kuharibiwa pikipiki 50 zilizokuwa zikitumiwa na magaidi hao.

Haya yanajiri wakati huu ambapo hali ya taharuki imetanda nchini humo kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwishoni mwa mwezi uliopita, huku kukiwa na wasiwasi wa nchi hiyo kuingiliwa kijeshi na maajinabi.

Magaidi Niger

Ikumbukwe kuwa, Jumatano ya tarehe Julai 26, jeshi la Niger lilifanya mapinduzi na baadaye kumuweka kizuizini rais wa nchi hiyo, Mohammed Bazoum. 

Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) imetishia kuishambuliwa kijeshi nchi hiyo ili kurejesha kile ilichokiita utawala wa kikatiba. Hata hivyo baadhi ya nchi wananchama haziungi mkono suala hilo la kutumia nguvu dhidi ya Niger.