Wananchi wa Zimbabwe wapiga kura kuchagua rais na wabunge
(last modified Wed, 23 Aug 2023 10:20:23 GMT )
Aug 23, 2023 10:20 UTC
  • Wananchi wa Zimbabwe wapiga kura kuchagua rais na wabunge

Wananchi wa Zimbabwe waliotimiza masharti ya kupiga kura, mapema leo Jumatano wamelekea katika vituo vya kupigia kura kushiriki uchaguzi utakaoamua iwapo Rais wa sasa Emmerson Mnangagwa atashinda muhula wake wa pili na wa mwisho au la.

Kuna wagombea 11 wa urais katika uchaguzi wa leo, ingawaje mchuano mkali unatazamiwa kuwa baina ya Rais Mnangagwa anayewania kupitia chama tawala ZANU-PF na Nelson Chamisa wa Muungano wa Wananchi kwa ajili ya Mabadiliko (CCC).

Rais wa Zimbabwe mwenye umri wa miaka 80, alitoa wito kwa wananchi kutojihusisha na vurugu kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa leo. Chamisa mwenye miaka 45, alishindwa kwa mwanya mdogo na Mnangagwa katika uchaguzi wa rais uliopita, miaka mitano nyuma.

Katika uchaguzi huo wa mwaka 2018, Mnangangwa anayefahamika kwa jina la utani kama 'Mamba' alizoa kura milioni 2.4 (50.8%), mbele ya Chamisa aliyepata kura milioni 2.1 (44.3%).

Kuna wapigakura zaidi ya milioni 6.6 waliosajiliwa nchini humo, na walioenea katika maeneobunge yote 210, ambayo pia yanawachagua wabunge. Aidha wananchi wa Zimbabwe wanawachagua maseneta na madiwani katika uchaguzi wa leo.

Uchaguzi Zimbabwe

Emmerson Mnangagwa ambaye ameshindwa kuboresha hali ya uchumi iliyodorora kwa miaka ishirini sasa licha ya ahadi alizotoa, analaumiwa na wananchi kwa hali ngumu iliyonayo Zimbabwe. 

Aidha chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe kinamtuhumu Rais Mnangagwa kuwa anawakandamiza wapinzani wa kisiasa. Katika wiki za hivi karibuni kuelekea uchaguzi wa leo, mikutano ya upinzani ilizuiwa huku viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge wakitiwa nguvuni.