Jun 29, 2016 13:16 UTC
  • UNICEF yatahadharisha kuhusiana na vifo vya watoto nchini Uganda

Mwakilishi wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF ametahadharisha kuhusiana na vifo vya watoto nchini Uganda.

Aida Girma amesema hayo katika ripoti iliyopewa jina la "Hali ya Watoto Duniani Katika Mwaka 2016" na kusisitiza kwamba, katika hali ya hivi sasa watoto 127 hufariki dunia kila siku nchini Uganda kutokana na maradhi mbalimbali kama malaria.

Amesema kuna haja ya kufanyika juhudi maradufu na kwa kutumia suhula zilizopo nchini humo ili kuboresha hali ya mamia ya maelfu ya watoto wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Mwakilishi wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF amesisitiza kuwa, shirika hilo linafanya juhudi kuhakikisha kwamba, Uganda iwe ni nchi ambayo watoto wake wanapata haki za awali na za kimsingi, kusiweko na watoto wanaokabiliwa na njaa nchini humo na mtoto yeyote asipoteza maisha kutokana na maradhi ambayo yanaweza kutibika.

Takwimu zinaonesha kuwa, kuna takribani watoto milioni nane nchini Uganda ambao wanaishi katika umasikini na kwamba, kuna haja ya kuwekwa mikakati ya kuwaokoa watoto hao katika kipindi cha miaka 25 ijayo.

Aidha kwa mujibu wa sensa ya hivi karibuni kabisa, Uganda ina wakazi karibu milioni 38 ambapo nusu yao wana umri wa chini ya miaka 15.

Tags