Sep 26, 2023 03:06 UTC
  • Baraza la Kitaifa la Niger lasema uwepo wa vikosi vya Ufaransa nchini haukaribishwi

Kuwepo kwa vikosi vya Ufaransa nchini Niger hakukubaliki. Hayo yameelezwa na Baraza la Kitaifa la Kulinda Nchi ya Niger (CNSP) katika kauli yake kuhusu tangazo la Ufaransa la kuondoa askari wake katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Siku ya Jumapili, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema kuwa nchi yake itapanga kuondoka kwa wanajeshi wake kutoka Niger katika wiki au miezi ijayo, na kuongeza kuwa askari wote watakuwa wamerejea nyumbani hadi mwisho wa 2023.

Serikali  ya Niger imesema katika taarifa yake kwamba, "Yeyote anayetishia maslahi ya nchi yetu lazima aondoke katika ardhi ya mababu zetu, wawe wanataka au la. Majeshi ya kibeberu na ya ukoloni mamboleo hayakaribishwi katika eneo letu la kitaifa."

Niger, ambayo ilikuwa koloni la Ufaransa, ilikuwa mshirika wa mwisho wa mataifa ya Magharibi katika Sahel kabla ya mapinduzi ya kijeshi. Ufaransa ina takriban wanajeshi 1,500 nchini Niger, wengi wao wakiwa wamezuiliwa katika kambi ya kijeshi ya nchi hiyo iliyoko Niamey.

Mnamo Julai 26, mapinduzi ya kijeshi yalifanyika nchini Niger, ambapo Rais Mohamed Bazoum alipinduliwa na kuzuiliwa na walinzi wake mwenyewe, wakiongozwa na Jenerali Abdourahmane Tchiani. Kufuatia mapinduzi hayo, Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ilisitisha ushirikiano wote na Niger na kutishia kuingilia kijeshi ikiwa waasi hawatamrejesha Bazoum madarakani.