Jul 01, 2016 07:56 UTC
  • Rais Museveni: Waasi wa ADF ndio wanaowaua Wanazuoni wa Kiislamu

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema kundi la waasi la ADF-Nalu, linaloendeleza harakati zake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndilo limehusika na mauaji ya hivi karibuni ya viongozi na wasomi wa Kiislamu nchini Uganda.

Akizungumza katika dhifa ya chakula cha futari katika Ikulu ya Entebbe, Rais Museveni amesema tayari amemuandikia barua Rais Joseph Kabila wa Kongo DR akimtaka alishugulikie suala hilo. Rais Museveni amesema waasi wa ADF-Nalu wamekuwa wakivizia na kuwaua wasomi wa Kiislamu nchini Uganda na kisha kurejea mafichoni katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Aidha amefichua kuwa, vyombo vya usalama vinamshikilia kiongozi wa kundi hilo la waasi anayejulikana kama Jamil Mukulu na uchunguzi dhidi yake unaendelea. Kauli ya Museveni inajiri baada ya Mufti Mkuu wa Uganda Sheikh Shaban Ramadhan Mubajje, kuitaka serikali ya Kampala kufafanua sababu za kuongezeka visa vya kuuawa wanazuoni wa Kiislamu nchini humo katika mazingira ya kutatanisha. Kadhalika Sheikh Mubajje ameitaka serikali kuwafikisha mbele ya vyombo vya mahakama wanaohusika na mauaji ya wasomi wa Kiislamu sambamba na kuharakisha mchakato wa kusikilizwa kesi za wanazuoni wa Kiislamu wanaozuiliwa katika jela za Uganda. Baadhi ya wasomi hao ni pamoja na Sheikh Yunus Kamoga, mkuu wa kikundi cha Tabligh, ambaye pamoja na wenzake wanatuhumiwa kuhusika na mauaji ya hivi karibuni ya Sheikh Mustafa Bahiiga katika eneo la Bwebajja barabara ya Entebbe na Sheikh Abdulkadir Muwaya wa wilaya ya Mayuge. Rais Museveni ametumia jukwaa hilo kusema kuwa, binafsi atawaita viongozi wote wa Kiislamu wa madhehebu tofauti kwenye meza ya mazungumzo karibuni hivi, kwa lengo la kuutafutia ufumbuzi uhasama na mgogoro miongoni mwao. Aidha ameahidi kuwa serikali yake itajenga chuo cha kidini cha kuwapa mafunzo wasomi wa Kiislamu nchini humo.

Tags