Polisi wapambana na waandamanaji Senegal wanaolalamikia kuakhirishwa uchaguzi wa rais
Wafuasi wa vyama vya upinzani na polisi wamepambana katika mji mkuu wa Senegal Dakar baada ya Rais Macky Sall kutangaza kuakhirisha kwa muda usiojulikana uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika Februari 25, na hivyo kuzusha wasiwasi kimataifa.

"Nitaanzisha mazungumzo ya wazi ya kitaifa ili kuleta pamoja masharti ya uchaguzi huru, wa wazi na shirikishi," alieleza Rais Sall siku ya Jumamosi bila kutaja tarehe mpya ya uchaguzi huo.
Wagombea urais wamesema watazindua kampeni zao siku ya Jumapili kukhalifu agizo rasmi la kuahirishwa uchaguzi.
Chama cha upinzani cha RFM kimesema kinapinga "kiutaratibu" kuakhirishwa kwa uchaguzi wa rais.
"Tutaonana na watu wote wa Senegal Jumapili hii kwa maandamano," ameeleza msemaji wa chama hicho Cheikh Tidiane Youm.
Habib Sy, mmoja wa wagombea 20 amesema vyama vya upinzani vimekutana na kukubaliana kuzindua kampeni zao za uchaguzi pamoja.
Mpinzani mwingine, meya wa zamani wa Dakar Khalifa Sall, yeye ametoa wito kwa nguvu za kidemokrasia kuungana.
"Senegal yote lazima isimame pamoja," amesema Sall mbele ya waandishi wa habari.
Sall, ambaye hana uhusiano wa nasaba na rais wa nchi hiyo, ameshutumu kile alichokiita "mapinduzi ya kikatiba" ya kiongozi ambaye "ana ndoto za kubaki milele".
Marekani, Umoja wa Ulaya na Ufaransa zimetoa miito ya kutaka tarehe mpya ya uchaguzi iwe ya mapema zaidi kadiri iwezekanavyo.
Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS imeeleza kutiwa "wasiwasi' na uamuzi huo wa Rais Sall na kutoa wito wa kufanyika mazungumzo.../