AU: Tuna wasiwasi kuhusu kuakhirishwa uchaguzi wa Rais Senegal
-
Moussa Faki Mahamat
Umoja wa Afrika (AU) umesema kuwa unatiwa wasiwasi na hatua ya Senegal ya kuakhirisha uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.
Katika taarifa yake, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat ameitolea wito serikali ya Senegal kuendesha zoezi la uchaguzi huo kwa amani, uwazi na kwa mujibu wa maelewano ya kitaifa.
Rais Macky Sall wa Senegal juzi alitangaza kuwa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 25 mwezi huu wa Februari utaahirishwa kufuatia mvutano uliojitokeza kuhusu orodha ya wagombea.
Kutofanyika uchaguzi huo kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali kumezua taharuki kutoka kwa mrengo wa upinzani nchini Senegal ambao umemshutumu Rais Sall kuwa anataka kuongeza kipindi chake cha kusalia madarakani kwa muda usiojulikana.
Rais wa Senegal ametangaza kuakhirishwa uchaguzi wa rais nchini humo baada ya Baraza la Katiba la nchi hiyo kuwaondoa katika orodha ya wagombea wa kiti cha urais baadhi ya wawakilishi wa vyama vya upinzani. Karim Wade, mwana wa kiume wa rais wa zamani wa Senegal, na mpinzani mashuhuri wa serikali ya sasa ya Senegal, Ousmane Sonko ni miongoni mwa shakhsia walioondolewa kwenye orodha hiyo ya wagombea wa kiti cha urais.

Wafuasi wa vyama vya upinzani jana Jumapili walifanya maandamano makubwa kulaani uamuzi huo wa Rais wa Senegal wa kuakhirisha uchaguzi wa rais. Leo Jumatatu wabunge wa Senegal walitazamia kujadili hatua hiyo ya kuakhirishwa uchaguzi wa rais kwa muda wa miezi sita.