Mar 04, 2024 02:29 UTC
  • Mwendesha mashtaka wa Burkina Faso: Watu 170 waliuawa katika mashambulizi dhidi ya vijiji vitatu

Mwendesha Mashtaka wa serikali ya Burkina Faso jana Jumapili alieleza kuwa watu takriban watu 170 waliuawa katika mashambulizi dhidi ya vijiji vitatu kaskazini mwa nchi hiyo wiki moja iliyopita.

Aly Benjamin Coulibaly jana alieleza kuwa  alipokea ripoti kuhusu kujiri mashambulizi kwenye vijiji vya Komsilga, Nodin na Soroe katika jimbo la Yatenga tarehe 25 mwezi Februari mwaka huu na kwamba takriban watu 170 waliuawa katika mashambulizi hayo. 

Jimbo palipojiri mashambulizi dhidi ya vijiji vitatu huko Burkina Faso 

Aliongeza kuwa, wahalifu waliwajeruhi watu wengine kadhaa na kusababisha pia uharibifu wa mali za raia. Mwendesha Mashtaka wa Burkina Faso amesema kuwa ofisi yake imeagiza kufanyika uchunguzi kuhusu mashambulizi hayo ya wiki iliyopita.  

Wakati huo huo watu walionusurika na mashambulizi dhidi ya vijiji  vitatu kaskazini mwa Burkina Faso wamesema kuwa makumi ya wanawake na watoto wadogo ni miongoni mwa wahanga wa hujuma hiyo. Duru za usalama nchini humo pia zimeeleza kuwa mashambulizi dhidi ya vijiji tajwa ni tofauti na matukio makubwa ya uhalifu yaliyoripotiwa kutekelezwa dhidi ya msikiti katika eneo hilo hilo la kaskazini mwa nchi hiyo wiki moja iliyopita.  

Burkina Faso imekuwa ikikabiliana na uhalifu na machafuko yanayosababishwa na wanamgambo wanaobeba silaha wenye mfungamano na makundi ya kigaidi ya al Qaeda na Daesh ambao walisambaratika kutoka nchi jirani ya Mali mwaka 2015.

 

Tags