Viongozi wa Libya waafikiana kuunda serikali ya umoja
Viongozi watatu muhimu wa Libya wamesisitiza juu ya udharura wa kuunda serikali mpya ya umoja ambao utapewa jukumu la kusimamia uchaguzi ambao umeakhirishwa kwa muda mrefu sasa.
Libya ilishindwa kufanya uchaguzi mkuu mwezi Disemba mwaka 2021 kama ulivyopangwa awali, kutokana na kutoelewana vyama vya nchi hiyo kuhusu sheria za kuendesha zoezi hilo la kidemorasia.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, makubaliano hayo mapya yametiwa saini na viongozi watatu muhimu wa Libya baada ya kufanya mkutano Cairo, mji mkuu wa Misri. Viongozi hao ni mkuu wa Baraza la Urais, Mohamed Menfi, kiongozi wa Baraza Kuu la Dola, Mohamed Takala, (wote wawili wana makao yao Tripoli), na Aguila Saleh, Spika wa Bunge lenye makao yake mjini Benghazi.
Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu pia alishiriki katika mkutano huo uliofanyika jana Cairo, ambapo viongozi hao wameutaka Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kuunga mkono mapendekezo yao.
Kabla ya hapo, makundi ya wanamgambo waliojizatiti kwa silaha na ambayo yamekuwa yakidhibiti Tripoli yalikubali kuondoka katika mji mkuu huo wa Libya. Kwa mujibu wa Imad Trabelsi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa serikal ya Libya inayotambuliwa kimataifa, makundi hayo ya wabeba silaha yameafiki suala la kuondoka Tripoli baada ya kufikiwa makubaliano.
Kwa mujibu wa mapatano hayo, makundi matano ya wanamgambo yanatakiwa yawe yameondoka kikamilifu Tripoli kufikia mwishoni mwa mwezi mtukufu wa Ramadhani (Aprili 9).
Mashirika ya kieneo na kimataifa yamekuwa yakiwataka viongozi wa Libya kuzika tofauti zao na kuzingatia maslahi ya taifa ili kujenga Libya mpya yenye nguvu, umoja, utulivu na mshikamano.
Ikumbukwe kuwa, mapinduzi ya Februari 17 mwaka 2011 yaliung'oa madarakani utawala wa Kanali Muammar Gaddafi, lakini tangu wakati huo, Libya imetumbukia kwenye machafuko ya kisiasa na vita vya wenyewe kwa wenyewe huku nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ikijitahidi kufanya mabadiliko ya kidemokrasia.