Niger yavunja mkataba wa ushirikiano wa kijeshi na Marekani
Serikali ya Niger imetangaza kwamba "bila kupoteza muda" inavunja makubaliano yake ya ushirikiano wa kijeshi na Marekani.

Kwa mujibu wa Kanali Abdramane, Niger imesikitishwa na nia iliyoonyeshwa na ujumbe wa Marekani ya kuwanyima watu huru wa Niger haki ya kuchagua washirika wao na aina ya ushirikiano wenye uwezo wa kuwasaidia kikwelikweli kupambana na ugaidi, na akaongeza kuwa Wamarekani hawakufuata itifaki ya kidiplomasia walipoelekea Niger na hata hawakuwafahamisha wenyeji wao kuhusu ajenda ya mazungumzo na tarehe ya kuwasili kwao.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alifanya ziara ya nadra nchini Niger mwaka mmoja uliopita kwa matumaini ya kutoa msukumo kwa rais Mohamed Bazoum, mshirika mkubwa wa nchi za Magharibi katika kampeni ya kinachoitwa juhudi za kiusalama za kupambana na watu wenye itikadi na misimamo mikali.
Miezi minne tu baada ya ziara hiyo ya Blinken, jeshi lilimwondoa Bazoum madarakani na kumweka kwenye kizuizi cha nyumbani.
Baada ya kushika hatamu za uongozi wa nchi, watawala wa kijeshi nchini Niger walichukua msimamo mkali dhidi ya mkoloni wa zamani wa nchi hiyo Ufaransa, na kulazimisha kuondolewa wanajeshi wa nchi hiyo waliokuwepo Niger kwa karibu muongo mmoja.
Huko nyuma, Jeshi la Niger lilifanya kazi kwa karibu na Marekani.
Lakini sasa limeonyesha hamu ya kuwa na ushirikiano na Russia, lakini bila ya kuwa na ukuruba kamili na Moscow kama ilivyo kwa majirani zake wa Mali na Burkina Faso zinazoongozwa pia na tawala za kijeshi.../