Kiongozi wa upinzani Bassirou Diomaye Faye, rais mpya wa Senegal
(last modified Tue, 26 Mar 2024 07:45:56 GMT )
Mar 26, 2024 07:45 UTC
  • Kiongozi wa upinzani Bassirou Diomaye Faye, rais mpya wa  Senegal

Kiongozi wa upinzani nchini Senegal, Bassirou Diomaye Faye, mwenye umri wa miaka 44, jana aliarifishwa kuwa rais ajaye wa nchi hiyo ikiwa ni chini ya wiki mbili baada ya kuachiwa huru kutoka gerezani ili kushiriki katika uchaguzi.

Huku matokeo rasmi ya uchaguzi wa Rais wa Senegal yakiwa bado hayajatangazwa; Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo ambaye alikuwa mgombea katika kinyang'anyiro hicho huku akiungwa mkono na Rais aliyemaliza muda wake Macky Sall amekubali kushindwa na mgombea wa upinzani kufuatia matokeo ya awali. Macky Sall pia amempongeza Bassiru Diomaye Faye na kumtaja kuwa mshindi. 

Macky Sall, rais wa Senegal aliyemaliza muda wake 

Ushindi wa Faye umeakisi matatizo na masaibu yanayowakabili vijana wengi wasio na ajira na kuhusu uongozi wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Katika hotuba yake ya kwanza, aliyoitoa jana jioni kama rais mteule mkaguzi huyo wa zamani wa masuala ya kodi ameahidi kuanza ukurasa mpya kufuatia miezi kadhaa ya ghasia, mivutano ya kisiasa na kutiwa nguvuni wanasiasa wa upinzani masuala yaliyopelekea kufanyika uchaguzi huu tajwa wa rais. 

Faye ameahidi kuiongoza Senegal kwa utu na uwazi na kupambana na ufisadi katika ngazi zote. 

Uchaguzi wa Jumapili huko Senegal ulifuatia miezi kadhaa ya machafuko yaliyochochewa na kukamatwa kwa Faye na Sonko mwaka jana, na wasiwasi kwamba rais atawania muhula wa tatu madarakani licha ya kufikia ukomo mihula yake ya uongozi kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.