Mar 28, 2024 07:09 UTC
  • Tovuti ya Marekani: Kuna mauaji ya kimbari yaliyofichwa nchini Ethiopia

Tovuti ya Marekani ya Counter Punch imechapisha ripoti inayosema kuwa Ethiopia, chini ya utawala wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed na chama chake tawala (Chama cha Mafanikio), imekuwa sehemu ya giza na ya kutisha, ambapo mtu yeyote anayepinga serikali yuko katika hatari ya kukabiliwa na ukatili na kukamatwa.

Ripoti hiyo imesema kwamba ukandamizaji wa utawala wa Ethiopia kwa sasa unalenga kaumu ya Amhara, na kwamba mauaji ya wanaume, wanawake na watoto wa kabila hili yamekuwa tukio la kila siku na yanaweza kutambuliwa kuwa ni sawa na mauaji ya kimbari.

Ripoti ya Counter Punch imesema makundi ya watu wanaovaa sare rasmi za serikali ya shirikisho na majimbo, pamoja na wanamgambo wa Oromo (Jeshi la Ukombozi la Oromo) wanachinja raia wa Amhara mitaani wanaokuwa katika shughuli zao za kimaisha. Limesema pia kuwa pande zisizojulikana zinatumia ndege zsizo na rubani kuwashambulia raia hawa.

Mwandishi wa ripoti hiyo amesema, hofu kubwa imekuwa ikiwakumba watu wa Amhara katika vijiji na miji, ambapo wanalengwa kwa kuzingatia utambulisho wao, na kwamba katika miaka mitano iliyofuatia kuwasili kwa Abiy Ahmed na wenzake madarakani, makumi ya maelfu ya watu wa kabila la Amhara wameuawa na mamilioni yao walihamishwa kutoka Oromia, eneo kubwa zaidi nchini, ambapo walikuwa na mali zao. 

Wakulima wakisubiri msaada wa chakula eneo la Amhara

Ripoti hiyo imeongeza kuwa utawala wa Abiy Ahmed unatekeleza operesheni za kuwakamata mamia kwa maelfu ya watu wa kabila la Amhara na wafuasi wa upinzani wa Oromo, na kuwanyonga wafungwa wengi.

Vilevile imeleeza kuwa magereza nchini Ethiopia yamejaa wafungwa kikamilifu katika maeneo yasiyojulikana, na kuna ripoti za wafungwa kudungwa sindano za magonjwa hatari na ya kuambukiza na kuwatelekeza hadi wanakufa.