Apr 28, 2024 04:27 UTC
  • Rwanda yakanusha madai ya DRC dhidi ya kampuni ya Apple

Serikali ya Rwanda imekanusha vikali madai ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo dhidi ya kampuni ya Apple.

Mamlaka nchini Rwanda zimeishtumu serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kile ilichokitaja kuwa madai yasiokuwa na msingi dhidi ya kampuni ya teknolojia ya mawasiliano ya Apple.

Tamko hilo la Rwanda limetolewa baada ya DRC kuishtumu kampuni hiyo kwa kutumia kwenye bidhaa zake, madini yanayosafirishwa kinyume cha sheria kutoka nchini humo. Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo, ameziambia duru za habari kwamba hii ni hatua ya hivi karibuni zaidi ya serikali ya Kinshasa ambayo inajaribu kwa mara nyingine kuiangazia Rwanda kwa tuhuma za uongo.

Wanasheria wa serikali ya Kongo wanaituhumu kampuni kubwa ya teknolojia ya Apple Inc. kuwa inanunua madini yaliyotoroshwa kutoka migodini mashariki mwa Congo ambako waasi wanakiuka haki za binadamu na kisha kuyahamishia madini hayo katika nchi jirani ya Rwanda.

Apple Inc. inatuhumiwa kutorosha madini ya Kongo 

 

Wanasheria wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameitumia kampuni hiyo kubwa ya kiteknolojia ya Marekani notisi rasmi wakiitaka isitishe kujishulisha na ununuaji madini yaliyotoroshwa kutoka Congo DR  na kuonya kuwa huenda wataichukulia hatua za kisheria ikiwa itapuuza onyo hilo.

Madini hayo ni pamoja na bati, tantalum na cobalt ambayo ni muhimu katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za teknolojia ya juu yanayochimbwa na makundi yanayobeba silaha katika maeneo yaliyoathiriwa na machafuko mashariki mwa Congo.