Apr 28, 2024 04:28 UTC
  • Watu 70 waaga dunia nchini Kenya kwa mafuriko

Kwa akali watu 70 wanaripotiwa kufariki dunia nchini Kenya kufuatia maafa ya mafuriko.

Ripoti zinasema, mvua kubwa na mafuriko vimesababisha vifo vya watu wasiopungua 70 nchini Kenya kuanzia katikati mwa mwezi uliopita wa Machi.

Hayo yameelezwa na msemaji wa serikali Isaac Mwaura, ikiwa ni idadi mara mbili ya ile iliyoripotiwa mapema wiki hii.

Hata hivyo Mwaura alikanusha madai kwamba mamia ya watu wamekufa kufuatia mafuriko yanayoendelea nchini humo na kutoa idadi hiyo rasmi ya vifo.

Kwa wiki kadhaa sasa, nchi hiyo ya Afrika Mashariki imekuwa ikishuhudia mvua kubwa iliyosababisha mafuriko katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, na pia katika mikoa ya magharibi na kati.

 

Kenya imesajili mvua kubwa tangu katikati ya mwezi uliopita wa Machi, lakini mvua imezidi kunyesha wiki iliyopita, na kusababisha mafuriko makubwa. Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya linasema kuwa, limefanya uokoaji zaidi ya 188 tangu kuanza mwezi Machi.

Aidha katika nchi jirani ya Tanzania, takriban watu 155 wamefariki dunia nchini humo kutokana na mvua kubwa inayoambatana na El Nino na hivyo kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi.